Waliomwigniza mkenge rais kikwete waadhibiwe!!!hii ni aibu tupu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Waliomwigniza mkenge rais kikwete waadhibiwe!!!hii ni aibu tupu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by sijafulia, Mar 27, 2010.

 1. s

  sijafulia Member

  #1
  Mar 27, 2010
  Joined: Mar 26, 2010
  Messages: 86
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  NINA kila sababu ya kumtukuza Mungu kwa uzima na afya, pia natoa pole kwa Watanzania kwa kuwapoteza ndugu na jamaa zao katika ajali iliyotokea Alhamisi wiki hii eneo la Kibamba, jijini Dar es Salaam ambapo watu wasiopungua 10 walifariki baada ya roli la mafuta kuligonga basi dogo la abiria na baadaye kulifunika.
  Sina nia ya kueleza kwa undani namna ajali ilivyotokea lakini yatosha kuwapa pole na faraja wale wote waliofikwa na msiba huo huku nikiwaomba madereva kuwa makini waendeshapo vyombo vya moto ili kunusuru maisha ya abiria wanaotumia vyombo hivyo.
  Leo ninataka niangazie kasoro zilizoibuliwa katika sheria ya matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi ambayo ilisainiwa kwa mbwembwe mbele ya umati wa watu na Rais Jakaya Kikwete katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 17 mwaka huu.
  Rais Kikwete, alitimiza ahadi yake aliyoitoa jijini Mwanza kuwa atasaini sheria hiyo kwa mbwembwe kwani katika hafla fupi ya kutia saini aliwaalika watu mbalimbali mashuhuri wakiwamo mawaziri, mabalozi, viongozi wa vyama vya siasa, wabunge, viongozi wa dini na wa taasisi za kijamii.
  Najua Rais Kikwete aliona namna muswada wa sheria hiyo ulivyogaragazwa bungeni kiasi cha kuifanya serikali ifanye mabadiliko mengi makubwa tena kwa kutumia turufu ya wingi na nguvu ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndipo ulipopita kwa mbinde.
  Takriban wiki mbili tangu kusainiwa kwa sheria hiyo, umeibuka utata wa kuingizwa kwa baadhi ya vipengele ambavyo inasemekana havikukubaliwa wala kupitishwa na wawakilishi wa wananchi (wabunge) ambao ndiyo wenye mamlaka ya kupitisha miswada ya sheria mbalimbali.
  Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa, ndiye aliyeushtua umma kwa kuweka bayana uchomekeaji mambo huo huku baadhi ya viongozi wakionekana kutojua au kujali chochote juu ya matamshi ya kiongozi huyo wa upinzani.
  Katikati ya wiki hii, Dk. Slaa alivunja ukimya kwa kuweka wazi kuwa ameshangazwa na kilichotokea Ikulu siku ya kusaini sheria hiyo ambapo amebaini kuwa kuna mtu au kikundi cha watu kimejivika ujasiri wa kuchomeka kipengele katika sheria hiyo na kikasainiwa na rais pasi idhini ya Bunge.
  Je, ni kweli kuwa kuna vipengele vilivyoongezwa baada ya kupitishwa kwa muswada wa sheria hiyo na Bunge? Je, kuna kanuni inayoruhusu vipengele kuongezwa pindi Bunge likimaliza majadiliano?
  Kama si ruhusa kufanya hivyo, kina nani wameshiriki kuongeza vipengele hivyo na kwa sababu zipi? Wamepanga kumdhalilisha Rais ili aonekane si msomaji wa jambo analolisaini? Kama jambo hili limetiwa mikono na watu wengine nje ya Bunge basi watendaji wanaomzunguka rais wetu hawamtakii mema yeye na nchi kwa ujumla.
  Haya ni baadhi ya maswali yanayonifanya nikose majibu. Hata hivyo bado nitaendelea kujiuliza kuwa watu hao waliofikia hatua ya kuongeza kinyemela vipengele hivyo walimlenga nani zaidi na kwa faida ya nani? Je kabla ya kusaini sheria hiyo rais alikaa na kuipitia ili kuona kile kilichokubalika bungeni ndicho kilichokuwa mikononi na machoni mwake?
  Najua Rais Kikwete ni miongoni mwa watu waliochangia kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa sheria hiyo kwa sababu alionyesha dhamira ya kukomesha matumizi makubwa ya fedha chafu katika uchaguzi, alifuatilia kwa makini mijadala ya wabunge na kile kilichokuwa mbele yake au ndiyo aliwaamini watendaji wake?
  Hapa ni lazima ifahamike kama kuna kundi limejipanga kwa ajili ya kucheza rafu na kisha kumuingiza rais ‘mkenge’; ni wajibu kuwagundua na kuchukuliwa hatua madhubuti na hata ikibidi wawekwe hadharani ili jamii iweze kuwafahamu.
  Hata hivyo bado tuwaulize wataalam wa masuala ya sheria ambao wakati wote pindi Bunge linapokuwa likijadili hoja nao hushiriki na kufuatilia ili pale penye tatizo waweze kulitatua au kulitolea ufafanuzi; hawa wanatumia fedha za walipakodi lakini walikuwa wapi mpaka muswada ule unatua mikononi mwa rais na kusainiwa?
  Katika sheria aliyosaini rais, Dk. Slaa anasema kuna kifungu cha 7 (3), hakikuwepo kabisa kwenye muswada uliojadiliwa na kupitishwa bungeni. Kwa kweli nimeshangazwa sana kwa sababu rais amedanganywa katika hili.
  Ni kweli Bunge halikusema ni nani anatakiwa kukagua timu ya kampeni ya nani, huku kwenye kipengele ambacho kimo kwenye sheria iliyosainiwa na rais inaonyesha kwamba timu za kampeni za mgombea urais zinatakiwa kuhakikiwa na Msajili.
  Hii kweli ni sheria ya aina yake na ambayo haijawahi kutokea katika nchi yetu hata hivyo inatufanya sasa tuamini kuwa zipo sheria nyingine ambazo zimekuwa zikiongezewa vipengele lakini kutokana na kukosa watu makini wa kufuatilia basi sheria hizo ndiyo huwa vitanzi kwa jamii.
  Kama kweli kuna upotoshaji umefanyika na kuongezeka kwa vipengele ipo haja ya kutafuta watu makini katika siku za usoni watakaomsaidia rais kwa kuwa hao waliokuwepo wamekuwa wakishindwa kufanya kazi ipasavyo.
  Tunakumbuka tukio la rais kutoa gari la wagonjwa katika wilaya moja lakini kwa kuwa alikuwa akikumbuka wilaya aliyoiahidi alifanikiwa kuuzima mchezo ule ambao nao ulikuwa mKenge mmojawapo.
  Sasa sheria hiyo ikirudishwa bungeni ili kuangaliwa upya kuna baadhi ya viongozi watakuwa wamepata ahueni kwa kuwa kwa wakati huu sheria hiyo inawabana kutokana na kushindwa kucheza rafu za kutoa rushwa kwa wazi na kutumia njia za panya ikiwemo kuitisha vikao usiku wa manane na kuongea na viongozi walio karibu na wananchi.
  Je, ni wabunge wangapi ambao wameweza kugundua kuongezwa kwa vipengele hivyo na wameshindwa kutoa kauli iwapo ni kweli kuna mchezo huo? Je, wanastahili kuendelea kuwepo bungeni?
   
 2. s

  sijafulia Member

  #2
  Mar 27, 2010
  Joined: Mar 26, 2010
  Messages: 86
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  KAMA RAIS ANAINGIZWA MKENGE NANI ATAPONA JAMANI??


  BILA shaka sasa tunaelekea kubaya na hata mkuu wetu wa kaya (rais) anafikia mahali pa kuingizwa mkenge na watu aliowateua kumsaidia kuendesha gurudumu la maendeleo ya nchi.
  Sina maneno mengine ya kuwaita watu waliomuingiza mkenge rais wetu kuwa ni majasiri, najua ujasiri ni nguzo muhimu katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja au taifa lakini ni vema tukaangalia namna tunavyoutumia ili usije ukaliangamiza taifa.
  Hebu tujiulize, inakuwaje rais wetu kila mara watendaji wake na watu wengine wanamuingiza mkenge? Si tumeona alivyonusurika kugawa gari la wagonjwa aliloliahidi kwa wilaya isiyotakiwa? Kama si ufahamu wake wa sehemu husika basi leo hii tungekuwa tunasimulia hadithi nyingine.
  Nakumbuka pia kwenye hafla fulani alikabidhi mfano wa hundi inayoonyesha utofauti wa maneno na tarakimu, alipouliza walimuambia ni tatizo dogo la kiufundi na wakaamua kuondoka nao ule mfano, tena kwa aibu kubwa.
  Ipo mifano mbalimbali, leo sina haja ya kuieleza katika safu hii, nimelenga kujikita katika sheria ya gharama za uchaguzi ambayo aliisaini kwa mbwembwe katika viwanja vya Ikulu wiki mbili zilizopita.
  Mimi ni miongoni mwa watu tunaomtakia mema rais wetu, ndiyo maana katika toleo lililopita nilimsihi kuwa ni vema sheria aliyoisaini ikawa na utekelezaji badala ya kuwa ya mbwembwe, bahati mbaya zaidi kabla haijaanza kufanya kazi limeibuka zengwe kuwa kuna vipengele vimeongezwa tofauti na vile vilivyopitishwa bungeni.
  Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ndiye aliyeibua zengwe la kuingizwa mkenge kwa rais kwa kuchomekewa vipengele ambavyo havikuidhinishwa na Bunge.
  Dk. Slaa amekitaja kifungu kilichochomekwa kuwa cha 7 (3), anasema Bunge halikukubaliana kuwa watu watakaokuwamo kwenye timu ya kumsaidia mgombea urais watathibitishwa na msajili, wa kumsaidia mgombea ubunge watathibitishwa na katibu tawala wa wilaya na wale wa udiwani watathibitishwa na katibu tarafa.
  Kilio hicho cha Dk. Slaa, kinaonyesha wazi namna watendaji wetu wasivyofanya kazi kwa umakini au walivyo mstari wa mbele kutetea masilahi ya kundi fulani la watu ambalo hutoa maagizo ambayo mwisho wake si mzuri kwa taifa.
  Hoja kubwa ambayo tunapaswa kujiuliza, kama rais anaweza kuingizwa mkenge, je, mtu wa kawaida atafanyiwa nini na watendaji wasio waaminifu? Nani kawapa nguvu ya kuingiza utashi binafsi au kikundi fulani katika sheria za nchi pasi na kuridhiwa na Bunge?
  Kwanini kila kukicha rais aendelee kudanganywa na watendaji aliowateua? Inawezekana rais si mkali kwa wale walio chini yake kiasi cha kuwafanya wamzoee na kumharibia kazi yake kwa jamii.
  Nina sababu gani ya KUNYAMAZA wakati naona udhalilishaji kwa rais unazidi kushika kasi siku hadi siku? Tukiendelea kumchezea na kumdharau rais wetu watu wa nje watafanya nini?
  Hakuna sababu ya kulindana, ni vema kila aliyehusika na mchezo huu akachukuliwa hatua kali za kinidhamu bila kujali wadhifa wake serikalini au kwenye chama tawala.
  Ninaamini kuwa tukianza kujenga utaratibu wa kuwajibishana, mambo mengi yatanyooka, kwa kuwa baadhi ya watendaji wamekuwa wakitekeleza majukumu yao ya kila siku kwa mazoea badala ya kufuata maadili ya kazi yanavyotaka.
  Nchi hii ni yetu sote, tusivumilie uozo unaofanywa na watu wanaojiona wao ndio wanaojua kila kitu au wanaotumia mwanya wa Watanzania kutokupenda kusoma kupindisha baadhi ya mambo au kutunga sera, sheria, mipango ambayo kwa kiasi kikubwa itayanufaisha makundi fulani.
  Tumsaidie rais wetu kuepukana na aibu kama hii, ambayo kama mambo hayatafunikwafunikwa, kuna kila dalili sheria hiyo ikarejeshwa bungeni na kile kilichochomekwa nje ya Bunge kikanyofolewa, lakini kwa nini tufike huko wakati uwezo wa kuzuia jambo hilo tunao?
  Fedha za walipa kodi zinapaswa zitumike kwa malengo maalumu na hasa katika shughuli za maendeleo, badala ya kuwagharimia wabunge au wataalamu kukaa vikao wa kurekebisha makosa yaliyofanywa kwa makusudi na watu waliopewa dhamana ya kuongoza.
   
Loading...