Waliobwagwa CCM sasa watoboa siri | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Waliobwagwa CCM sasa watoboa siri

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by BAK, Aug 5, 2010.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 5, 2010
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,548
  Likes Received: 81,990
  Trophy Points: 280
  Waandishi Wetu
  Raia Mwema
  Agosti 4, 2010

  [​IMG]Wasema rushwa ilikua nje-nje
  [​IMG]TAKUKURU walizidiwa ujanja
  [​IMG]Nguvu za nje zatumika


  MCHEZO mchafu katika kusaka ushindi wa kura za maoni nafasi ya ubunge katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na matumizi makubwa ya fedha kwa washindani ni kati ya malalamiko ya wagombea vigogo waliobwagwa, imefahamika.

  Katika baadhi ya majimbo imeelezwa kuwa baadhi ya maofisa wa Taasisi ya Kupamba na Kuzua Rushwa (TAKUKURU) walifumbia macho usafirishaji wa fedha taslimu pamoja na mchakato wa kuzigawa katika vituo vya uchaguzi, baadhi ya majimbo ya mkoani Tabora yakitajwa.

  Kutoka katika Jimbo la Nzega, baadhi ya wana-CCM wamezungumza na gazeti hili wakieleza walichokishuhudia, mmojawao akiwa Mbunge wa zamani wa Jimbo hilo kabla ya Mbunge wa sasa aliyemaliza muda wake, Nhindilo Musisa, ambaye ndiye aliyemkabidhi kijiti mbunge aliyepita Lucas Selelii.

  “Pikipiki zilikuwa zikitumika kusafirisha fedha kwenda vijijini kwa ajili ya kugawa fedha katika baadhi ya maeneo. Kuna kadi feki zimesambazwa na wahusika waliweza kupiga kura za maoni bila wasiwasi…tupo tayari kueleza haya kokote,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Nzega, Musisa.

  Raia Mwema pia lilizungumza na Selelii ambaye ameshindwa. Katika mazungumzo hayo ya simu aliunga mkono madai yaliyotolewa na Musisa akiweka bayana kuwa binafsi ameshindwa kwa sababu kuu mbili.

  Alizitaja sababu hizo mbili kuwa ni mosi, hakuwa na maandalizi ya kutosha kwa upande wa fedha na kwamba kwa jinsi hali ya matumizi makubwa ya fedha ilivyokuwa alipaswa kuwa na zaidi ya Sh milioni 100. Sababu ya pili kubwa kwa mujibu wa Selelii ni kuwa wapiga kura wengi waliojiandikisha majina yao kutokuwapo kwenye orodha ya wanaopaswa kupiga kura na wakati huo huo kadi mpya feki nyingi zikiwa zimemwagwa na wenye kadi hizo kuruhusiwa kupiga kura kwanza huku walio na za halali na za zamani wakiwekewa mizengwe.

  “Tawi lenye wanachama 300 waliojiandikisha awali si majina yote yalionekana. Tawi lenye wanachama 300 utakuta ni 100 tu ndiyo waliweza kupiga kura. Hapa Nzega ni kama vile Benki Kuu ilihamia hapa, pikipiki zimetumika kubeba fedha kuelekea vijijini.

  “Nisizungumzie wagombea wenzangu nizungumze yangu…mimi nilikuwa nawalipa mawakala wangu Sh 10,000 kila mmoja, wapo waliokuwa wakiwalipa mawakala wao Sh 5,000 ili walinde na kuhakiki kura zetu vituoni. Lakini baadaye Sh milioni tatu zilipelekwa karibu katika kila kituo, baadhi ya mawakala wakapewa fedha nyingi zaidi, baadhi ya viongozi wa CCM Wilaya walipewa fedha nyingi na hata baadhi ya maofisa wa TAKUKURU nao walipewa migawo.

  “Operesheni za usafirishaji na ugawaji fedha zilifanyika kwa uhuru na uhakika bila kuingiliwa na TAKUKURU. Kadi feki zimemwagwa kama njugu bila bugudha ya viongozi. Ikitokea mwenye kadi ya zamani na mwenye kadi mpya ambayo ni feki wanajitokeza kulalamika ili wapige kura, wale wenye kadi mpya wanaruhusiwa na wenye kadi ya zamani wanakataliwa,” alisema Selelii na kuongeza kuwa;

  “Kwa wasiojua kusoma wala kuandika walidhulumiwa haki na uhuru wao wa kupiga kura ya maoni. Taratibu zinafahamika kwamba asiyejua kusoma na kuandika anapaswa kuja kituoni na mtu wake anayemwamini, lakini huku hawakuruhusiwa kufanya hivyo. Msimamizi wa uchaguzi ndiye katika kituo aliyekuwa akiwasaidia na kuna uwezekano alikuwa akijaza mtu anayempenda yeye na si anayetakiwa na mpigaji kura halisi.

  “Hizi ni sehemu tu ya rafu zilizochezwa. Ni rafu ambazo hata shetani hawezi kucheza, lakini nyuma ya rafu hizi wapo watuhumiwa wakuu wa ufisadi wa Richmond, kila mkakati umepangwa na kuratibiwa na kundi hilo.”

  Raia Mwema iliwasiliana wagombea wengine waliobwagwa kusikia kilichojiri kutoka kwao ambao ni pamoja na Profesa Philemon Sarungi aliyekuwa akigombea Jimbo la Rorya, John Malecela Jimbo la Mtera, Joel Bendera, Jimbo la Korogwe Mjini, Dk. James Wanyancha Jimbo la Serengeti na William Shelukindo wa Bumbuli.

  Wengine ambao gazeti hili liliwasiliana ni pamoja na Mgana Msindai wa Iramba Mashariki, Dk. Dalali Kafumu anayegombea Jimbo la Igunga, Dk. Juma Ngasongwa wa Ulanga Magharibi, Magale John Shibuda wa Maswa, Joseph Mungai wa Mufindi Kaskazini, Aloyce Kimaro wa Vunjo na Dk. Guido Sigonda wa Songwe.

  Hata hivyo, katika orodha hiyo ni Joseph Mungai na Kimaro pekee ndio waliokuwa tayari kuzungumza na gazeti hili na wengine wakishindwa kupokea simu zao za mkononi, baadhi simu hazikuwa zikipatikana na wengine walieleza kuwapo kwenye vikao vya tathmini na ikibidi kuchukua hatua au kusubiri mchakato wa CCM kukamilika.

  Katika maelezo yake Mungai alisema: “Ingawa katika Jimbo la Mufindi Kaskazini ninakogombea kulikuwa na matumizi makubwa ya fedha, hilo halikuniathiri sana. Kilichoniathiri sana ni baadhi ya wagombea wenzangu kutokujua taratibu za uchaguzi, wametumia mbinu chafu wakiihusisha TAKUKURU.”

  “Siku mbili kabla ya upigaji kura za maoni, kuna taarifa zilitolewa na kuandikwa na magazeti fulani. Baada ya habari hizo kuandikwa kwamba Mungai amekamatwa na kuhojiwa kwa rushwa, mgombea mmoja alichukua magazeti hayo na kuyasambaza usiku wilaya nzima. Hii iliniathiri sana na TAKUKURU hawakuwahi kunikamata hata siku moja.”

  Hata hivyo, alipoulizwa kama kasoro hizo msingi wake ni chama au wagombea wenzake alijibu; “Kubwa zaidi ni nature ya baadhi ya wagombea na si chama kama taasisi. Ni tabia zisizo za kimaadili za baadhi ya wagombea ndiyo tatizo. Alipoulizwa kuhusu hatua atakazochukua alijibu; “Hizi ni kura za maoni tu, mimi natoa nafasi kwa process ndani ya chama. Naamini bado chama chetu ni makini na kinaweza kufanya uamuzi unaolinda heshima na maadili yake.”

  Naye Kimaro aliyeshindwa kutetea nafasi yake katika Jimbo la Vunjo, alisema kwa njia ya simu kwamba alijua ya kuwa kuna watu watatumia pesa na kweli hilo likafanyika na yeye mwenyewe akaiona nguvu ya pesa ilivyofanya kazi dhidi yake.
  Hata hivyo, alisema kwa vile zoezi hilo lilisimamiwa na viongozi wa CCM, anawaachia viongozi hao kwa vile haitasaidia chochote kwa lolote atakalolifanya.

  ‘Ninachoweza kusema ni kwamba sijutii miaka yangu mitano niliyokuwa bungeni. Nimefanya kazi ya kutosha kwa wananchi wa Vunjo na Tanzania kwa ujumla,” alisema na kuongeza ya kuwa anajivunia kupatikana kwa maji safi katika vijiji 40 na kujenga shule 75 ikiwa ni pamoja na shule pekee katika kijiji anachotoka kiongozi wa chama cha upinzani cha TLP, Augustine Mrema.

  Katika matokeo ya awali yaliyokwishakutangazwa mawaziri kadhaa wameangushwa, akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala na Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga.

  Shamsa alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda akifuatiwa na Mjumbe wa NEC na kijana machari Nape Nnauye, lakini matokeo katika Jimbo la Ubungo yalimuibua Hawa Ng’umbi kuwa mshindi na kuwaacha Nape na Shamsa pembeni.

  Jimbo la Kinondoni ambako mbunge anayetetea nafasi yake, Iddi Azan alielekea kuongoza, nako hali haikuwa shwari kwani hadi tunakwenda mitamboni, uongozi wa CCM Wilaya ya Kinondoni ulikuwa ukikusanya matokeo katika matawi yake, hali inayoashiria kuwapo kwa utata mkubwa.

  Mpinzani wa karibu wa Azan mwanamke pekee, Shy-Rose Bhanji, alilalamikia ukiukwaji mkubwa wa taratibu kutokana na mawakala wake kuzuiwa kuingia katika baadhi ya matawi huku wa mpinzani wake wakiruhusiwa, maeneo ambayo ndiko matokeo yalielekea kumsaidia mbunge anayemaliza muda wake.

  Naibu waziri walioanguka ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera huku taarifa zisizothibitishwa zikisema Mwantumu Mahiza wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi naye alikuwa ameanguka .

  Kundi la vigogo walioanguka linamgusa pia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega aliyezidiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Frederick Mwakalebela.

  Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Amina Said Mrisho, naye amebwagwa na Mbunge Benedict ole Nangoro, anayemaliza muda wake katika Jimbo la Kiteto, mkoani Manyara.

  Baadhi ya mawaziri waliotajwa kuwa katika hofu kuanguka akiwamo Profesa Jumanne Maghembe katika jimbo la Mwanga na Profesa David Mwakyusa katika jimbo la Rungwe Magharibi, waliibuka kidedea pamoja na wapinzani wao, Joseph Tadayo na Richard Kasesela kulalamikia ukiukwaji mkubwa wa maadili na taratibu.

  Kutoka mkoani Mwanza, Jimbo la Nyamagana, alishinda Lawrance Masha aliyepata kura 8,627 akifuatiwa na Malogoi Mboje (2,420) na tathmini ikionyesha kuwa matokeo hayakutarajiwa hususan ushindi wa Masha dhidi ya wenzake. Mwaka 2005 Masha alipata upinzani mkali kutoka kwa Omar Mbalamwezi wa CUF ingawa mwaka huu CHADEMA ndiyo inaonekana kuwa na nguvu zaidi.

  Jimbo la Ilemela, Anthony Diallo alishinda kwa kura 6,601 akifuatiwa na Pastory Masota (2,159). Tathmini jimboni humo inabainisha kuwa Diallo ana nafasi kubwa ya kutetea nafasi yake kiti chake katika Uchaguzi Mkuu. Historia ya jimbo hilo haitoi nafasi kwa vyama vya upinzani.

  Dk. Charles Tizeba ameibuka kidedea katika Jimbo la Buchosa kwa kupata kura 11,257 akifuatiwa na Eric Shigongo aliyepata kura 7,578, mbunge anayemaliza muda wake, Samuel Chitalilo ameangushwa jimboni humo na tathmini ikionyesha kuwa Dk Tizeba bado ana nguvu na ndiye aliyeshinda kura za maoni 2005 lakini jina lake halikurudishwa.

  Kutoka Jimbo la Sumve, mbunge aliyemaliza muda Richard Ndassa aliongoza kwa kupata kura 6,047, akifuatiwa na Richard Mchele kwa kura 3,402, wakati Jimbo la Kwimba, mbunge anayemaliza muda wake, Bujiku Sakila ameanguka akipata kura 1,216 na mshindi wa kura hizo za maoni jimboni humo ni Shanifu Mansoor aliyepata kura 7,333.

  Kutoka Ukerewe Getrude Mongella alifanikiwa kutetea nafasi yake kwa kupata kura 6,666 katyika ushindani mkali uliowahusisha pia Chipanda Mtani-1,822, Ernest Kamando-642, Deogratius Lyato - 4,140, Laurent Munyu- 284, Oswald Mwizarubi-2,362, Nyandiga Msafiri-3,530, Deus Tungaraza-967, na Pastory Mwibule Kazi- 104.


  Tathmini inaonyesha kuwa Balozi Mongela amefanya kazi ya ziada kutetea nafasi yake ngazi ya chama. Kura zilizoenda kwa wapinzani wake zinaonyesha kulikuwa na upinzani mkali sana. Kama makundi hayatavunjwa na Upinzani ukasimamisha mgombea anayekubalika bado Balozi Mongela ana kazi pevu usoni.
   
 2. kinepi_nepi

  kinepi_nepi JF-Expert Member

  #2
  Aug 6, 2010
  Joined: Aug 16, 2007
  Messages: 870
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Katika baadhi ya majimbo imeelezwa kuwa baadhi ya maofisa wa Taasisi ya Kupamba na Kuzua Rushwa (TAKUKURU) walifumbia macho usafirishaji wa fedha taslimu pamoja na mchakato wa kuzigawa katika vituo vya uchaguzi, baadhi ya majimbo ya mkoani Tabora yakitajwa
   
 3. M

  Mkandara Verified User

  #3
  Aug 6, 2010
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Hawa viongozi tuliwambia dhjamira ya mtandao hawakuamini. Walikuwa na muda wa kujitoa nma kujiunga na Upinzani waliona ni usaliti. Leo yamewakuta wao ndio kwanza wanajua kwamba vitu hivi hufanyika?...

  Na huyo Mama Mongela kapita kwa mbinu za kuweka wagonmbea mia kidogo lakini kama CCm ingeweka mfumo wa maoni kama ulivyo ule wa kiti cha Urais (mchujo) au wangegombea watu watatu tu, Mama huyu asingemtoa Lyato.
  Pongezi nyingi namshushia wangu Deus Tungaraza kuingia ulingoni japokuwa hakufanya vizuri.. Deo, kama ni msomaji wa JF nakuomba sana tuwasiliane..
   
Loading...