Ndugu watanzania wenzangu,katika kupitia magazeti mbalimbali yanyoaminika na kuheshimika mbele ya umma wa tanzania nimekutana na makala katika gazeti la mwananchi,nimeona niwaonjeshe utamu wa hii mada,sasa nimeanza kugundua kwanini serikali inalikandamiza hili gazeti.nawasilisha
Tumesikitishwa na jinsi baadhi ya watu na vyombo vyenye mamlaka na ushawishi katika jamii yetu vilivyopindisha hoja zilizotolewa na Chadema kuhusu kitendo cha wabunge wake kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akilihutubia mwishoni mwa wiki. Wapo watu waliokiona kitendo hicho kama uhaini na wapo waliokiita usaliti wa hali ya juu.
Wote hao walitaka wabunge wa chama hicho wafukuzwe bungeni, kwa madai kwamba wamekataa kumtambua rais aliye madarakani na ambaye pia ni sehemu ya Bunge. Walisema kitendo hicho walichokiita cha udhalilishaji wa Rais lazima kijibiwe kwa nguvu zote. Chama tawala kilitoa tamko kwamba kilikuwa katika mchakato wa kuhakikisha kuwa wabunge wa Chadema wanatiwa adabu.
Lakini wapo pia waliokiona kitendo hicho kama cha kawaida na cha kidemokrasia kabisa kilichokuwa na lengo la kufikisha ujumbe kwa chama tawala na serikali yake kuhusu umuhimu wa kuandika katiba mpya na kusimika tume huru ya uchaguzi baada ya matokeo ya chaguzi nyingi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kuacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Chadema kilisema kuwa hoja yake hiyo ilikuwa imepindishwa na kupotoshwa makusudi, lakini kilifafanua tena na tena kwamba sio kweli kwamba kilikuwa hakimtambui Rais, bali mfumo uliomuweka madarakani.
Moja ya sauti muhimu katika jamii iliyozungumzia kitendo hicho cha wabunge wa Chadema ni aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta aliyesema kuwa kitendo cha wabunge hao kilikuwa cha kawaida ambacho hakizuiwi na kanuni yoyote ya Bunge pia hakina adhabu yoyote. Alisema wabunge wanaruhusiwa kuonyesha hisia zao kwa kutoka nje ya ukumbi pale wanapotofautiana na jambo fulani. Alikumbushia mwaka 2000 wabunge wa upinzani walipotoka nje kwa kupinga kupitishwa kwa bajeti ya serikali.
Tumeorodhesha mlolongo mzima wa matukio hayo ili kuyaweka katika muktadha wa mgogoro huo na kuwakumbusha wadau wa demokrasia katika nchi yetu kuwa mgogoro uliopo hivi sasa sio kati ya Rais Kikwete na Chadema, bali mfumo uliobuniwa na kulelewa na chama tawala ambao ni katiba ambayo pia ilizaa tume ya uchaguzi. Katika hali hiyo, chama hicho kimetangaza madai matatu ya msingi ambayo ni katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na tume huru ya kuchunguza yaliyotokea katika uchaguzi uliopita.
Tunapenda kuamini kuwa madai ya Chadema ni ya msingi katika kutafuta mustakabali wa nchi yetu. Tunaamini pia kuwa madai hayo sio ya Chadema pekee bali Watanzania wote bila kujali dini, kabila au chama cha siasa. Umoja wa kitaifa na amani ambayo imekuwa ikihubiriwa haitakuwapo bila katiba inayokidhi matakwa ya watu wote. Ni katiba mpya tu itakayofuta sheria mbovu kama ile ya uchaguzi ya 1985, inayoipa tume ya uchaguzi madaraka ya kumtangaza rais na kuwanyima wananchi fursa ya kupinga matokeo hayo mahakamani.
Ni katika kupima hali hiyo tunadhani kuwa tume huru ya kuchunguza yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu pia ni muhimu. Watanzania watahitaji kujua, kwa mfano, kwa nini watu zaidi ya milioni 20 walijiandikisha kupiga kura lakini waliojitokeza ni milioni 8 tu? Nini kilichosababisha watu milioni 12 kutopiga kura au kuchelewa kutangazwa matokeo au katika sehemu fulani matokeo hayo kutangazwa na wakuu wa wilaya badala ya Nec?
Ni bahati mbaya kwamba Rais katika vipaumbele 13 vya serikali yake katika kipindi kijacho hakugusia masuala hayo ambayo Chadema inayadai. Baadhi ya vyombo vya habari vimefanya juhudi za makusudi kuwapotosha wananchi badala ya kuwaelimisha kuhusu suala hili linalohusu muktakabali wa nchi yetu. Sisi tunasema kuwa juhudi za Chadema na wanaharakati wengine zitashinda ili mwishowe upande huu wa Jamhuri ya Muungano nao upate maridhiano kama yaliyopiganiwa vilivyo na CUF huko Zanzibar.