Wakulima wa miwa waanza kufurahi

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,409
20,759


Morogoro. Kitendo cha Rais John Magufuli kuzuia sukari kutoka nje ya nchi isiingizwe nchini kimewezesha kiwanda cha sukari cha Kilombero kulipa wakulima wa miwa bei ya juu.

Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa timu ya wakulima wa nje wa miwa (Out Growers), Job Zahoro katika siku ya wakulima iliyoandaliwa na watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Miwa Kibaha baada ya kutembelea shamba darasa linaloendeshwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na kiwanda na wakulima.

Zahoro alisema kumekuwa na ongezeko la malipo kwa jumla kwa wakulima wa nje tangu kiwanda hicho kianzishwe mwaka 1999.

Kiongozi huyo alisema kiwanda kililipa Sh1 bilioni kwa wakulima wadogo ukiondoa mishahara lakini kwa msimu ulioisha kimelipa Sh47 bilioni ambazo zinasaidia kuboresha maisha ya wakulima kwenye eneo dogo la wilaya za Kilosa na Kilombero.

Alisema Waziri wa Viwanda na Biashara amekipa kiwanda jukumu la kuzalisha tani 185,000 za sukari lakini kiwanda hakijafikia hata tani 150,000.

Kwa msimu uliopita kiwanda na wakulima walilima tani za miwa 1.2 milioni na bado kuna pengo la tani 700,000 na uwezo wa kiwanda kujipanua kwa mashamba umefika mwisho hivyo sehemu iliyobakia pekee ni kutoka kwa wakulima wadogo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo amepongeza kazi inayofanywa na watafiti kwa kuwawezesha kupata mbegu bora na kuwafundisha wakulima mbinu za kilimo.

Aliahidi kushirikiana na watafiti, kiwanda na wakulima kuhakikisha sukari inapatikana nchini na kuboresha maisha ya wakulima wa miwa.

Mtafiti wa miwa, Dk Hildelitha Msita alisema Taasisi ya Utafiti wa Miwa Kibaha imekuwa ikifanya kazi karibu na wakulima na viwanda vyote vya sukari nchini kwa kuwapatia mbegu bora, kuwafundisha kilimo bora, mbinu za kukabiliana na magonjwa ya miwa na kuanzisha mashamba darasa ambayo yamesaidia kubadilisha kilimo cha wakulima wadogo tangu waanze.


Chanzo: Mwananchi
 
Ni hatua nzuri sana, wazalishe miwa kwa kiwango kizuri ili isaidie maendeleo ya kiwanda na hata bei ya sukari iwe nafuu
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom