Wakosoaji wa Rais Magufuli wana hoja zinazofanana, lakini wanakosa nguvu ya pamoja

Mzee Chayayi

Member
Feb 16, 2018
25
19
Wakosoaji wa rais Magufuli wapo na bila shaka wanatimiza haki yao ya msingi kwa mtawala yaani haki ya kukosoa, Wakosoaji hao ni watanzania na wasio watanzania, bila shaka ni maelfu kwa mamilioni. Wapo wanamkosoa hadharani, na wapo wanaomkosoa wakiwa wamejifungia vyumbani mwao,

Lengo la kukosoa ni kuonyesha njia, wakosoaji hawana mda wa kulalamika, bali hutoa ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii, hata hivyo, mamlaka inayojitambua ikikosolewa husikiliza, hupokea na kutolea ufafanuzi au kuyafanyia kazi yale yaliyosemwa na wakosoaji

Watawala hawawakubali wakosoaji, wanawaona si wazalendo, na hawataki kuitikia wito wa kumuombea yule anayeomba kuombewa. Hata hivyo ili watimize malengo yao, wakosoaji hawahitaji kukubalika na watawala, Wanahitaji sana kukubalika na wananchi walio wengi, wananchi hao huwasikiliza wakosoaji wanahoja gani, kama hoja hizo zinagusa maisha yao basi wananchi hao hujiunga na wakosoaji na kutengeneza vuguvugu la kung’oa mamlaka zilizokosolewa lakini hazikusikia sauti za wakosoaji wa awali.

Hoja inayohitaji kujibiwa ni, wakosoaji wanakosoa kuhusu nini? Na hao wanaokosoa ni akina nani? Je ni wapinzani wake wenye wajibu wa kumkosoa au ni wale wanaompenda hivyo wanamkosoa ili afanye vizuri au ni wale ambao wamechoka kuisoma namba basi wanatafuta pa kupumulia?

Unaweza ukadhani JPM anafanya yale ambayo wengi walitaka rais ayatekeleze, lakini ukifuatilia kwenye social media, au ukaenda kanisani kusikiliza mahubiri yanayoambatana na waraka, au ukaamua kusikiliza siasa za Tanzania unaweza kabisa kuamini wanaomshabikia au kumuunga mkono JPM ni wale tu wanaonufaika na utawala wake wakiwemo, mawaziri, wabunge, madiwani, makatibu wa wizara, mabalozi, wakuu wa mikoa, wilaya, Das, wakurugenzi, na viongozi waandamizi wa chama chake.

Ukiachilia mbali tabaka hilo la wanufaika na utawala wa awam ya 5, lipo kundi jingine liloumia lakini bado wanashindwa kupaza sauti zao. Hawa ni wale ambao hawana uwezo wa ku logic, wazee, watu wa vijijini, hawaoni mbali, hawana elimu na hivyo hawaoni cha kukosoa, wao kila kitu kipo sawa.

Hata wale wanaokosoa wanasema JPM na serikali yake ni sawa na mgonjwa aliyeko ICU, inatumia ubabe pale ambapo akiri ilipaswa itumike, kwenye kesi za uchochezi, watuhumiwa wanapimwa mikojo, Serikali inatumia mamlaka ya mapato (TRA) pamoja na uhamiaji kusurubu wakosoaji wake.

Bahati mbaya sana JPM na serikali yake haijajua, wakosoaji wanazidi kuongezeka na wote wana hoja zinazofanana. Wakosoaji hao wanazidi kuungwa mkono na wananchi walio wengi, Hata hivyo, Mtawala kuongea kwa uchungu sana hakumaanishi anayajua matatizo ya wananchi wake.


Lakini unaweza ukasema, wanaikosoa serikali ya JPM na siyo CCM, Inawezekana mkosoaji akamkosoa JPM na chama kikabaki salama??? Unaweza ukasema wanaomkosoa JPM ni mafisadi na au wanatumiwa na mafisadi, ni nani ambaye hajui kukosolewa kwa kiongozi ndiyo kuimalika kwake?? Je siku wakiungana na kuanza kukosoa wakiwa wamoja, je JPM na CCM yake watabaki salama?

1. TAASISI ZA DINI

Taasisi za dini hasa kanisa limejitahidi sana kutoa maoni yake juu ya utawala huu unaoongozwa na ‘’jiwe” maoni yao kupitia nyaraka mbalimbali, mfano, waraka wa Kwaresma kutoka Baraza la Maaskofu wa kanisa Katoliki 2018, na Ujumbe Wa Pasaka Kutoka Baraza La Maaskofu Wa Kanisa La Kiinjili La Kilutheri Tanzania (KKKT), jumbe hizo kwa pamoja zimezungumzia hali mbaya ya uchumi, kupungua uhuru wa kutoa maoni na kujieleza, mauaji na kutekwa kwa raia, kupigwa risasi kwa raia, maendeleo yenye mlengo wa kiitikadi, ubaguzi, vurugu na ubabe katika chaguzi za marudio, Hata hivyo, Tatizo lililopo hawajazungumza wakiwa wamoja., kila kanisa limezungumza kivyake.

Maaskofu hawajaanza leo kukosoa, wameanza miaka mingi sana, walikosoa kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), lakini kwa sasa ukosoaji huo haufanyiki kwa umoja, kila kanisa linakosoa kivyake, ingawa hoja zao zinafanana, Ndiyo maana inakuwa rahisi sana kwa DAB au kada yeyote wa ccm kusema ovyo vyo kuhusu nyaraka hizo za kanisa,

Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), linaundwa na Taasisi zifuatavyo:- Jumuiya ya Kikristo Tanzania – CCT, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania – TEC, Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania – PCT pamoja na Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (ambao hualikwa kama Watazamaji.

Mfano rejeeni Tamko hili, lililotolewa na TCF wakati wa utawala wa JK ,Tamko la Maaskofu kuhusu uchinjaji na hali ya mwelekeo wa kisiasa nchini. Tamko hili lilitolewa kwa umoja, ilikuwa ni vigumu sana kwa JK kuupuuza waraka huo.

‘’JIWE’’ pamoja na wateule wake wanapuuzia maoni ya kanisa kwa kuwa maoni hayo hayatolewi kwa ‘’umoja’’, watawala wanaona maoni hayo yanatolewa kwa mlengo wa kisiasa, ndiyo maana mara kadhaa rais Magufuli amesikika akitamka, ‘’zaka zimepungua makanisani’’ kwa kuwa zilikuwa zikitolewa na mafisadi, na baadhi ya makanisa yanatumiwa na watu wasiyoitakia mema nchi yetu’’

Ni vyema sasa kanisa litoe maoni yake kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania(TCF), hii itatoa mwamko mpya kwa watawala, wataliheshime kanisa na watasikiliza na kuzifanyia kazi hoja zitakazotolewa..

Kanisa liwaambiwe watawala, kwamba ZAKA NA SADAKA siyo lengo la kuanzishwa kwake, kanisa lilianzishwa na Yesu Kristo katika karne ya 1 hadi leo, liwaambie watawala kwamba, kanisa ni kitu kizuri na mhimu sana, ni bibiarusi wa Yesu Kristo, ni mwili wa Kristo, ni chombo cha Mungu cha kuunganisha waumini wake kwa Roho mtakatifu, liwaambie watawala kuwa kanisa linaatangaza habari njema, linaombea watu, linasaidia wenye dhiki na linatetea haki za binadamu.

2. VYAMA VYA SIASA

Hili kundi ni mhimu sana, na vyama vya siasa vya upinzani ninavyovizungumzia hapa ni vyama vyote vyenye usajiri wa kudumu (permanent registration) au usajiri wa mda (Temporary registration), vilivyonyimwa haki yake ya msingi ya kufanya siasa, isipokuwa CCM wao ndiyo wamejiruhusu kufanya chochote na kwa wakati wowote.

Vyama hivyo vya upinzani vyote vina hoja zinazofanana, vyote zinakosoa kukosa haki ya kufanya maadamano, mikutano ya hadhara, uhuru wa kusema, kutoa maoni nk.

Kila chama kinakosoa kivyake, kinapambana kivyake, viongozi wao wanafungwa, wanateswa, wanasweka mahabusu, wanabambikiziwa kesi, yote hayo bado vyama hivyo havitaki kuungana.


Hata hivyo ili chama cha siasa kifanikiwe kufikia malengo yake hakihitaji watawala wakiunge mkono, bali wananchi ndiyo wakiunge mkono, Yawezekana malalamiko hayo ya vyama vya upinzani hayajawagusa wananchi, Siyo kwamba hawajasikia wito wa vyama vya upinzani kuhusu utawala wa awamu hii, na kama wameusikia basi hawajaukubali na haujawashawishi.


Maelfu ya wananchi hawa wameona matokeo ya Maandamano miaka iliyopita, hawataki na hawapendi kurudi huko, wameona walivyowasaliti, wameona majigambo na hotuba moto moto bungeni na nje ya bunge, lakini mwisho wa siku wanasema hawajazikubali hoja za wapinzani, kutokana na ‘’KUTOAMINIKA KWAO’’

Ni vyema sasa vyama vya upinzani viungane vije na vision mpya, iliyojaa mikakati mbadala, vision hiyo ihubiriwe na wapinzani wenye ushawishi kwa jamii, wasio na makando kando, wanaoamini katika upinzani, wasionunulika na watawala, wasio waoga na walio wazuri kujieleza mbele ya wananchi na wakawaelewa. Mfano mzuri wa watu hao ni Tundu Lissu,

Mhimu sana, Wapinzani waachane na lile duduwasha linaloitwa UKAWA kwa sasa halina tena mikakati, halina ushwawishi lilitumiwa likafeli kuwapa majibu wale waliolikimbilia dakika za mwisho kuelekea Oct 25, 2015.


3. VYOMBO VYA HABARI

Mpaka sasa hakuna chombo chochote cha habari ambacho hakijasoma namba isipokuwa TBC hicho ni kitengo cha propaganda kinachotumiwa na watawala kuonekana mubashara.


ITV iliyokuwa mahiri katika kuonyesha ‘’mubashara’’ midahalo na makongamano mbalimbali, yaliyoamsha ari kwa jamii kufuatilia kile kinachofanywa na watawala, sasa ITV imekuwa ni Televisheni ya kusifia mtawala, hata maswali yao ya kipima joto siku ya alhamis na ijumaa vyote vimekuwa ni kumpamba mtawala, Vyombo vya habari vimelalamikia sana kuhusu, sheria ya makosa ya mitandao pamoja na sheria ya huduma za habari,

Kupitia sheria hizo gandamizi, Mamlaka imetumia sheria hizo kufungia au kupiga faini vyombo vya habari vinavyoikosoa serikali, Watawala wanapenda kile kinachoandikwa na TANZANITE, JAMVI LA HABARI, UHURU, HABARI LEO, ZANZIBAR LEO, Magazeti hayo hayapati adhabu kali kama inayotolewa kwa magazeti mengine kama MAWIO, TANZANIA DAIMA, MWANAHALISI, RAIA MWEMA, NIPASHE nk

Hata hivyo hivi karibuni uongozi wa Jukwaa la Wahariri (TEF) umetoa maoni yake, wameongea kuhusu kupungua na kuelekea kupotea kabisa kwa uhuru wa kujieleza, kutekwa, kuuawa kwa waandishi wa habari, na pia matukio ya kupotea kwa wananchi.

Hoja ni kwamba, tamko hilo la TEF lilipaswa kupewa mkazo na Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika- Tawi la Tanzania ( Misa Tan), Mfuko wa vyombo vya habari Tanzania (TMF), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Kukosekana kwa taasisi hizo katika tamko la TEF, kumepelekea tamko hilo kupita pasipo ‘’jiwe’’ kutikiswa.

4. VYAMA VYA KITAALUMA PAMOJA ASASI ZA KIRAIA.

Hili kundi lina umuhimu wake katika dhana nzima ya kukosoa watawala, Hawa ni wasomi, wanajua tulipo, tulipotoka na tunapaswa kuwa wapi, na ninani katufikisha hapa, na ni nani anaweza kututoa hapa, inasemekana wasomi hawa ndio walitaka na bado wanataka mabadiliko zaidi, wanakosoa kwa hoja, hata hivyo ukiangalia utaona kuwa wasomi ndiyo wananufaika zaidi na utawala huu wa awamu ya 5, wasomi wengi wamekimbilia teuzi, wakishateuliwa huanza kusifia yale waliyokuwa wanayakosoa kabla hawajapata teuzi. Rejeeni kauli mbalimbali za Prof. Kabudi, Prof Mkumbo kabla na baada ya kupata teuzi.


Mfano, Vyama vya kitaaluma au asasi za kiraia TLS pamoja na Tume ya haki za binadamu na utawala bora nk. Taasisi hizi zimetoa matamko mbalimbali kuhusu yale yanayoendelea nchini, lakini matamko hayo hayajalitikisa jiwe, jiwe lipo imara, linahubiri ukanda, linahubiri kuombewa, na hivi karibuni limepoteza 1.5Trillion.


Haya yote yanafanyika kwa sababu hakuna umoja katika kukemea mambo ya ovyo yanayofanywa na mtawala, Vyama hivi pamoja na asasi za kiraia viungane, viandae makongamano, watu waelimishwe, waambiwe tulipo, tulipotoka, na wapi tunapaswa kuwa. Na tufanye nini ili tufike huko.

Itolewe elimu ya uraia hususani haki za raia na wajibu wao kwa nchi, wananchi waelimishwe wajibu wa kiongozi kwa nchi na raia wake, elimu hiyo itolewe kwa wote. Kwa kufanya hivyo jamii itapona, itachukua hatua dhidi ya mtawala mfanya maigizo. Mwenye kipaji cha kuongea kwa hisia, lakini hajui matatizo yanayowakumba wananchi ni yapi na afanye nini ili awatoe kwenye matatizo hayo.


TANZANIA NI YETU SOTE, TUUNGANE TUKOSOE TUKIWA WAMOJA. TUTETEE KILICHO CHETU.
 
Back
Top Bottom