Wako wapi mafisadi waliyoyumbisha serikali ?

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
INAWEZEKANA Watanzania wengi watakuwa wamesahau kabisa tuhuma nzito zilizokuwa zikiwalenga baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nne wa Rais, Jakaya Kikwete.

Hoja kadhaa ziliibuliwa katika bunge lililomaliza muda wake ambalo kwa kiasi kikubwa liliweza kufanikisha kuibuliwa kwa tuhuma nzito za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ama uzembe katika utoaji wa maamuzi mazito ya umma.

Hapo ndipo wananchi wengi walipoweza kubaini kuwa kumbe wapo viongozi mafisadi ambao ni zaidi ya wala rushwa ambao kimsingi ilionekana kuwa uchumi wa nchi unashindwa kwenda mbele kutokana na hujuma nzito zinazotokana na matumizi mabaya ya mali za umma na raslimali za nchi.

Kwa kiasi kikubwa bunge lililopita liliwaamsha zaidi wananchi kiasi cha kurudisha imani na kuwafanya watu wengi wawe wafuatiliaji zaidi wa masuala muhimu yaliyokuwa yakiendelea bungeni kuliko ilivyokuwa katika mabunge ya nyuma yaliyopita.

Neno ufisadi lilibeba uzito wa juu kupita kiasi na kusababisha midahalo mbalimbali iweze kuibuka katika jamii yenyewe na vyombo vya habari juu ya tafsiri halisi ya neno ‘FISADI’ ,maana zililotolewa kwa kadri ya uelewa wa watu kuanzia ngazi za chini hadi juu,watu walijua kuwa ufisadi ni adui mkubwa katika maendeleo ya nchi kuliko kitu kingine.

Kwa maana hiyo mijadala kadhaa iliyokuwa ikitolewa bungeni na kuibuliwa kwa tuhuma mbalimbali kuliifanya serikali kuwa makini na kuanza kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wa serikali waliotajwa kujihusika na tuhuma hizo, tume ziliundwa na majibu yaliweza kutolewa bungeni na zile zilizoundwa na rais mwenyewe anajua hatua alizochukua.

Inanibidi nianze na suala la Fedha za Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) lililosababisha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Balali sasa ni marehemu akumbwe na misukosuko mikubwa pengine ndiyo iliyosababisha mauti yake ya haraka yaliyotokana na msongo wa mawazo licha ya kuwa na matatizo mengine ya kiafya.

Niliwahi kusema kuwa Dk. Balali atakuwa mmoja wa watendaji waandamizi wa serikali aliyehusishwa na sakata la BoT, ambaye atakuwa ametolewa kafara kwa kuwa wale waliohusika na wizi wa mabilioni hayo ya fedha na kutakiwa wawe yamerudisha serikalini, sijui imefikia wapi na Watanzania wanapaswa kujua nini juu yao.

Mambo yanaonekana kuzidi kupoa kama vile hayakuwepo kiasi kwamba jinsi suala la EPA lilivyovuma hakujawa na uwazi wa kutosha wa maelezo sahihi kuwa ni kweli wahusika wote waliotajwa na tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo watakuwa wamerejesha fedha za serikali ambazo mwenye nafasi pekee ya kulizungumzia ni Rais Kikwete.

Kama huo tunaweza kuuita ufisadi ni vyema ikajulikana wazi kuwa hao mafisadi walioweza kujichotea fedha za akiba za malipo ya madeni ya nje ziko wapi,zimerudishwa na zimefanya nini katika kukuza miradi kadhaa ya maendeleo na wahusika wa sakata hilo wote wamesamehewa?

Likaja suala la Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, watu wanakumbuka jinsi moto mkali ulivyowaka bungeni hadi kusababisha baadhi ya viongozi wa juu serikalini waamue kuachia ngazi na leo hii suala hilo limewekwa wazi kuwa Shirika la Umeme hapa nchini,TANESCO wanapaswa kulipwa fidia.

Na wakati huo huo kampuni nyingine ya Dowans nao wameibana koo TANESCO wakitaka walipwe mabilioni ya fedha za walalahoi kwa ajili ya uzembe usiomithirika uliofanywa na watendaji wa umma bila kujali maslahi ya nchi, Tanzania ni maskini na kesi kama hizi za kibiashara ni wazi kuwa zinazidi kuchimba donda ndugu lisilokuwa na tiba.

Huku wananchi wakiendelea kuumia kwa kukumbwa na mgao wa umeme usiokuwa na uhakika na haya masuala ya kudaiana fedha kunazidi kulitafuna shirika hilo ambalo baadhi ya wadau wa masuala ya biashara wamekuwa wakishauri kama ilivyo kwenye kampuni za simu za mkononi na kwenye suala la umeme kuwe na soko huria.

Hayo yote ni masuala mazito yanayozidi kutafuna uchumi wa nchi kwa kuwa kama hakuna miundombinu mizuri ya uzalishaji umeme wa uhakika nchi itaendelea kubanwa na mikataba mibovu ya Richmond, Dowans, IPTL na mingineyo ambayo sasa inakuwa kitanzi kwa serikali maskini kama ya Tanzania.

Tumeshuhudia sakata la kuwepo kwa mikataba mibovu ya madini ambayo ilisababisha Rais Jakaya Kikwete aunde tume ya wataalamu wachache waweze kuchunguza na kutoa maoni yao kuhusu sekta hiyo, majibu yalipatikana na suala lililopo ni utekelezaji wa maoni yote yaliyotolewa licha ya kuridhiwa kwa sheria mpya ya madini kwa kiasi fulani.

Ni wazi kuwa mikataba mibovu ya madini, suala la Buzwagi kuchochewa moto na baadaye kupoozwa bado jambo hilo linaashiria namna mambo mengi ya msingi yanavyokwenda mrama, mianya ya madini yetu kwenda nje kiholela ni mkubwa zaidi kuliko tunavyodhani kuwa tumeweza kudhibiti huku wananchi wengi wakipiga kelele kuwa hawaoni manufaa ya uwepo wa wawekezaji katika migodi mikubwa.

Kwa kutambua mazingira hayo na mengine kadhaa jibu la kuwepo kwa mafisadi wasioweza kukamatika nako kunatia shaka kwani tumeweza kujionea mkataba wa ununuzi wa RADA ulivyoweza kuchukuliwa kijuu juu huku kukiwa na mikinzano kati ya serikali ya Uingereza na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa hapa nchini(TAKUKURU) jinsi walivyoweza kutoa taarifa zinazopingana na mashitaka yaliyofunguliwa Uingereza.

Hizo zote ni dalili tosha kuwa, Tanzania imekuwa moja ya nchi inayofanikiwa zaidi kuwakingia vifua wahalifu wa kifisadi kuliko kudhihirisha wazi kuwa wote waliojihusisha na tuhuma hizo nilizozitaja hawapaswi kutetewa hata kwa hatua moja ya kwenda mbele au nyuma, vinginevyo umasikini huu hautakwisha.

Kwa tabia hiyo ya kulindana na kufikiri kuwa wananchi wamesahau tuhuma zote zilizoelekezwa kwa viongozi kadhaa waandamizi wa umma na Bunge lililopita, waliotajwa wanaendelea kupeta na waliofikishwa mahakamani ni wazi kuwa wakati sheria ikiendelea kuchukua mkondo wake lazima tujue kuwa hawa mafisadi wengine waliyoiyumbisha serikali wako wapi?

Kama waliweza kutajwa, wengine wakaamua kujiuzulu na wengine wanaendelea kutamba kuwa wamesafishwa ni sura ipi iliyofanya au kusababisha kukuzwa kwa jina la ufisadi katika nchi isiyoweza kushughulikia mafisadi, Je hawa waliohusishwa kweli ni mafisadi na kama si hao sasa wako wapi mafisadi walioiyumbisha serikali, ulikuwa wimbo au ngonjera?
 
Back
Top Bottom