Wakili akwamisha upelelezi wa kesi ya bilioni 188

Hearten

Member
May 17, 2016
46
54
Dara es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh188.9bilioni kupitia mashine ya risiti za kielekroniki (EFD) inayomkabili mfanyabiashara Mustapha Kambangwa (34), bado haujakamilika.

Kambangwa, mkazi wa Mbagala Kongowe anakabiliwa na mashtaka manne Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, likiwemo la kutakatisha fedha katika.

Kwa mara ya kwanza, Kambangwa alifikishwa mahakamani hapo Desemba 7, 2018 kujibu mashtaka manne katika kesi ya uhujumu uchumi namba 19/ 2018.

Wakili wa Serikali, Ester Martin amedai leo Alhamisi Desemba 20, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa utetezi kuwasilisha hoja za kupinga shitaka dhidi ya mshtakiwa.

Hata hivyo, hoja hizo hazikuwasilishwa mahakamani hapo baada ya Ester kudai kwamba wakili mwenzake Christopher Msigwa, ambaye ndio mwenye jalada halisi la kesi hiyo ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu ni mgonjwa.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, wakili wa utetezi Shamo Shadrack, amedai ofisi ya waendesha mashitaka ina mawakili wengi na kuhoji sababu za kuumwa kwa mtu mmoja kuzuie kesi kuendelea.

" Kuumwa kwa mtu mmoja kusizuie kuendelea kwa kesi, kwani mawakili wote wanafanya kazi ofisi moja hivyo tunaomba tarehe ijayo ambayo ni Desemba 24, 2018 tuweze kuwasilisha hoja zetu, " amedai Shadrack.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Janeth aliwataka upande wa mashitaka kuhakikisha shauri hilo linaendelea hata kama yule wa awali bado anaumwa aendeshe mwingine.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 24, 2018 na mshtakiwa kurejeshwa rumande.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa hiyo kati ya Juni Mosi ,2016 na Novemba 2, 2018.

Katika shtaka la kwanza, Kambangwa alijifanya amesajiliwa kuwa mlipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Amedai katika tarehe tofauti kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, 2018 maeneo ya jiji la Dar es Salaam mshitakiwa alijifanya kuwa amesajiliwa kukusanya kodi ya VAT Sh 188,928,752,166 kwa kujifanya anakusanya fedha hizo kwa niaba ya TRA.

Pia, Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, 2018, Kambangwa kwa udanganyifu alitumia mashine ya EFD namba 03TZ842011315 iliyosajiliwa kwa jina la Kampuni ya Abraham's Group LTD kukwepa kodi ya VAT yenye thamani ya fedha hiyo

Katika shtaka la tatu, ambalo ni utakatishaji wa fedha, mshtakiwa anadaiwa, tarehe na kipindi hicho, katika Jiji la Dar es Salaam alijipatia au kujimilikisha fedha hizo alizozipata kutokana na makato ya kodi ya VAT ambazo zilipaswa kutolewa kwa Kamishna wa TRA na mshitakiwa huyo alipaswa kujua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la ukwepaji kodi

Kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, 2018 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa kwa vitendo vya makusudi vya kukwepa kodi alitumia mashine ya EDF huku akijua kwamba hajasajiliwa kama mlipakodi ya VAT na hivyo kuisababishia hasara TRA ya 188,928,752,166
 
Back
Top Bottom