Wakili ajitoa kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi Jiji la Arusha

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
981
2,658
Wakili wa utetezi Valentine Nyalu, aliyekuwa anawawakilisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima (44) na wenzake wawili wanaokabiliwa na makosa manane katika kesi mbili za uhujumu uchumi, amejitoa kuwawakilisha watuhumiwa.

Wakili huyo amechukua uamuzi huo leo Julai Mosi, 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ambapo kesi hizo zilipangwa kusomewa maelezo ya awali.

Katika kesi ya kwanza ya uhujumu uchumi namba 3/2022 mbali na Dk Pima, watuhumiwa wengine aliyekuwa Mkuu wa Idara ya fedha katika halmashauri hiyo, Mariam Mshana, Mkuu wa Idara ya Mipango ya uchumi, Innocent Maduhu na Nuru Ginana aliyekuwa mchumi.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa huku upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali mwandamizi, Akisa Mhando.

Bila kutaja sababu za kujitoa, Wakili Nyalu kutoka kampuni ya Maro Advocates ya jijini Arusha, alieleza mahakama kuwa wamelazimika kujitoa katika uwakilishi kwenye kesi hiyo na kuomba majina yake na ya kampuni hiyo yaondolewe kwenye kumbukumbu kuanzia sasa.

Baada ya Wakili huyo aliyekuwa anawawakilisha Dk Pima, Mariam na Maduhu kujitoa, mawakili Sabato Ngogo na Joshua Minja walieleza mahakama kuwa wanawawakilisha watuhumiwa wote wanne.

Hakimu Mbelwa alisema mahakama inaridhia na kuwa wakili huyo amesema kwa wakati sahihi kabla hati hiyo inayofanyiwa marekebisho haijasomewa na kuwa kuanzia sasa majina yake au kampuni ambayo naye ni mwanachama (Nyalu) hayatakuwepo.

Aidha baada ya kujitoa wakili huyo,Wakili Akisa alisoma hati mpya iliyorekebishwa baada ya hati ya awali kuwa na dosari katik shitaka la kwanza.

Aidha alishindwa kuwasomea washitakiwa hao maelezo ya awali ya kesi hiyo kwa madai kuwa wamebaini kuna mambo ya kiupelelezi yanatakiwa yakamilike kabla ya kuwasomea maelezo hayo ya awali (PH).

Katika kesi ya pili ya uhujumu uchumi namba 4/2022 inayomkabili Dk Pima, Mariam, Maduhu na Alex Daniel (aliyekuwa mchumi), Wakili Nyalu alieleza mahakama nia ya kujitoa kuwawakilisha watuhumiwa hao katika kesi hiyo pia ambayo ilipangwa leo kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Aidha Wakili Minja aliieleza mahakama kuwa dhamana iko wazi kwa washitakiwa wawili ambao ni Ginana na Alex, ambapo pia walishindwa kukidhi masharti ya dhamana na mahakama kuagiza Julai 4, 2022 wapelekwe mahakamani ili kama wamekamilisha taratibu za dhamana waachiwe kwa dhamana.

Hakimu Mbelwa ameahirisha kesi hizo hadi Julai 14, 2022 watuhumiwa hao watakaposomewa maelezo ya awali ambapo wanakabiliwa na makosa nane ambayo ni ufujaji na ubadhirifu pamoja na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.

Mbali na kesi hizo Dk Pima, Mariam na Maduhu, wanakabiliwa na makosa sita ikiwemo utakatishaji fedha,katika kesi nyingine ya uhujumu uchumi namba 5/2022, kosa la kwanza linalowakabili wote ni ufujaji na ubadhirifu wa Sh103 milioni.


Source: Mwananchi
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom