Wakazi wa Chanika wagoma kuhesabiwa kutokana na Mgogoro wa Mipaka

Lady Whistledown

JF-Expert Member
Aug 2, 2021
1,023
1,609
Wakazi Mtaa wa Ngobedi Kata ya Zingiziwa wilayani Ilala mkoani hapa wamewagomea makarani wa sensa kuwahesabu kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa mipaka katika eneo hilo.

Eneo hilo linaopakana na Wilaya ya Kisarawe upande wa Magharibi na Wilaya Mkuranga upande wa Kusini zote za mkoani Pwani, limezua utata wa mipaka.

Wakizungumza leo Agosti 23 na Mwananchi, viongozi wa maeneo hayo waliofika ofisi ya Serikali ya Mtaa kufikisha malalamiko yao, wamesema mgogoro huo umekuwepo tangu mwaka 2018 na haujawahi kupatiwa ufumbuzi hadi leo.

Mjumbe wa Shina namba 23, Daniel Masanja amesema hata kipindi cha uandikishaji anuani za makazi watu walipigwa, kujeruhiwa na kufunguliwa kesi mbalimbali kutokana na kugoma kuandikishwa upande wa Kisarawe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Miundombinu, Issa Kambona amesema ni aibu kutokea kwa tukio kama hilo la kususia kuhesabiwa katika Kata ambayo anaishi Makamu wa Rais, Philip Mpango, ambayo ingetakiwa iwe ya mfano katika shughuli hiyo.

Naye Salma Sultan amesema huduma zote za kijamii wanazipata Kata ya Zingiziwa iweje leo wahesabiwe Kata ya Mazimbu ambayo ipo Kisarawe.

"Tunavyojua sensa moja ya sababu ni kujulikana kuna watu wangapi ili hata baadaye huduma zitakapotolewa ijulikane wanahudumiwa wangapi, sasa kwa utaratibu huu inamaana tutaachwa pembeni na bajeti yetu haitakuwepo huko serikalini," amesema Salma.

Mwananchi ilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Nickson Simon ambaye alimtaka mwandishi kuvuta subra kufuatilia suala hilo halafu atamrudia.

Kwa upande wake Mwenyekiti Serikali ya Mtaa ya Zingiziwa, amesema mgogoro huo waliomba viongozi wa juu kuushughulikia kwa muda mrefu, lakini hawajafanya hivyo na hata wakifika kweye eneo husika wanajikuta wakigombana wenyewe kwa wenyewe.

Mmoja wa maofisa aliyejitambulisha kuwa ni msimamizi wa makarani wa sensa eneo hilo,alisema katika uchukuaji wa taarifa hawakuangalia suala la mipaka.

Majibu hayo yalionekana ambayo kutowaridhisha wananchi hao na kumtaka kwenda kueleza wakubwa wake vizuri kuhusu tatizo hilo na kuja na majibu ya kueleweka.

Kutokana na hilo, ofisa huyo alirudi ndani ya ofisi ya Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa kuzungumza na wenzake watatu ambao alikuwa kaongozana nao kuja kusikiliza malalamiko hayo.



CHANZO: Mwananchi
 
Back
Top Bottom