Wakati ukifika, umefika

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
74,640
155,001
Wakati ukifika umefika tu
Hebu tufikirie kidogo tu…kidogo
itatosha kweli? Haijalishi endapo
tutafikiri kidogo ama sana. Kufikiri
ni kufikiri tu.
Tufikiri nini? Enhee, hebu fikiria.
Fikiria huu ni mwaka 1490, nawe ni
bwana Alesandro Polo, ukiishi
Ureno. Halafu mtu akaja kukwambia
ipo siku, utaweza kusafiri kwenda
bara la Asia kwa kulizunguka bara la
Afrika. Nadhani utamwona mwehu
kwani jambo hilo haliwezekani.
Fikiria huu ni mwaka 1502, nawe ni
Kardinali Antonio Rovelle, msaidizi
wa Papa. Anakuja mwanasayansi na
kukwambia dunia si bapa. Dunia ni
duara na ndiyo inayolizunguka jua na
si jua kuizunguka dunia. Lazima
utamshitaki kwa Papa, na mtu huyo
kuuawa huku akipigwa chapa ya
msalaba kifuani na kutupwa
hadharani. Kwa kuwa utamwona
mwehu aletaye mawazo
yasiyowezekanika.
Fikiria huu ni mwaka 1515, nawe ni
Mfalme Louis wa Navarre,
Ufaransa. Anakuja mtu na
kukwambia utawala wa kanisa la
Kirumi utafikia mwisho. Utamwona
mtu huyo ni mwehu kabisa awazaye
jambo lisilowezekanika kamwe.
Fikiria huu ni mwaka 1831, nawe ni
bwana Sinatabu bin Salum, mkazi
wa Kaole, Bagamoyo. Anakuja mtu
na kukwambia, ipo siku moja
duniani, biashara ya utumwa itafikia
kikomo. Ama kwa hakika
utwamwona laanakum aongeaye
mambo yasiyowezekanika.
Fikiria tena. Sasa fikiria huu ni
mwaka 1897, nawe ni bi Tuwangile
Sekalinga, mkazi wa Itamba Iringa.
Anakuja mtu na kukwambia ipo siku
Mkwawa atachemka kwa
Wajerumani. Lazima utamjibu,
asee! Maana utaona anaongea
mambo yasiyowezekana kabisa.
Fikiria zaidi. Fikiria huu ni mwaka
1936, nawe ni Luteni Albredcht
Geiss, kamanda wa vikosi vya Nazi
unayesimamia usalama katika
michuano ya Olimpiki mjini Berlin,
Ujerumani. Anatokea mtu mmoja na
kukwambia Unazi utakufa tu. Ama
kwa hakika utampiga bastola
kichwani kwa kuona anaongea
mambo yasiyowezekana.
Fikiria huu ni mwaka 1950, nawe ni
bwana Adofo Abeeka mkazi wa
Kumasi, Ghana. Anatokea mtu
akikwambia ukoloni utakwisha tu
Afrika. Utamwona mwehu
azungumzaye bila kufikiria kwani
ukoloni hautokwisha.
Wakati unaendelea kufikiri unaufikia
mwaka 1986, nawe ni bwana
Konsantin Allochka, mkazi wa
Moscow, USSR. Anakuja mtu na
kukwambia Sovieti itameguka,
ukomunisti utakwisha na hatimaye
kuzika vita baridi. Lazima
utamwandika kwenye The Moscow
Times kama msaliti, mhaini na
mchochezi mkubwa azungumzaye
mambo yasiyowezekana asilani
abadani.
Halafu fikiria huu ni mwaka 1988,
nawe ni bwana Boudewijn Geertj,
Afisa Mkuu wa Polisi wa Transvaal,
Afrika Kusini. Mtu mmoja bwana
Sitiyeni Mmobhuzo anakwambia,
Nelson Mandela ataachiwa, ubaguzi
wa rangi utakwisha na mtu mweusi
atatawala Afrika Kusini.
Utamtazama mara mbili kabla ya
kumweka kwenye kiti cha umeme
kwa kuwa anazungumza ugaidi.
Fikiria huu ni mwaka 1990, nawe ni
Imam Sree Kumar Shakeek wa
Kuwait. Anakuja mtu na kukwambia,
utawala wa Saddam Hussein una
mwisho. Utamlaani kwa kuwa
unazidi kuteseka na vita.
Fikiria tena ni mwaka huo huo 1990,
nawe ni bwana Bernard Bwalya
Mulenga, mkazi wa Kitwe, Zambia.
Anakuja mtu na kukwambia chama
cha UNIP kitaondoka madarakani na
KK hatotawala tena Zambia.
Utamwona ni taahira kwani Zambia
bila KK haiwezekani kamwe.
Fikiria huu ni mwaka 1995, nawe ni
bibi Abigale Hakizimana, ukiwa
katika kambi ya wakimbizi Ngara,
Tanzania. Mtu mmoja anakwambia
amani itarejea Rwanda na Rwanda
itang’ara kiuchumi. Utamtazama
kwa jicho la kisirani kwa kuona
ayasemayo hayawezekaniki kamwe.
Fikiria huu ni mwaka 2000, nawe ni
bwana Atwoli Otieno, mkazi wa
Kericho, Kenya. Anakuja mtu na
kukwambia KANU itaondoka
madarakani siku moja. Utambishia,
utamkodia Mungiki kwani waona
analeta za kuleta kwa mambo
yasiyowezekana kamwe.
Sasa hebu fikiria kwa mara
nyingine. Huu ni mwaka 2006, nawe
ni bi Adeline Wilbur, Seneta wa
Texas, Marekani. Mtu mmoja
anakujia asubuhi ukipata kahawa.
Anakwambia kuna siku moja
Marekani itatawaliwa na mtu
mweusi. Utakula viapo vyote na
kusema walaaniwe wote wenye
mawazo kama hayo. Utamwona ni
mwendawazimu kwa kuwa na ndoto
za Alinacha. Haiwezekani asilani
abadani.
Fikiria sasa kwa mara ya mwisho.
Huu ndiyo haswa mwaka 2010, nawe
ni bwana Ndilibaha Pakaye, mkazi
wa Kidegembye, Njombe. Wewe
huambiwi walichoambiwa Alesandro
Polo, Antonio Rovelle, Mfalme Louis,
Sinatabu bin Salum, Tuwangile
Sekalinga, Luteni Alberdcht Geiss,
Adofo Abeeka, Konstantin Allochka,
Boudewijn Geertj, Sree Kumar
Shakeek, Bernard Bwalya Mulenga,
Abigale Hakizimana, Atwoli Otieno
wala Adeline Wilbur.
Wewe unaambiwa ipo siku CCM
itang’oka madarakani. Lazima
utamtazama kwa mashaka mtu
huyo. Utamwona mwehu kwa kuwa
unaamini hilo jambo haliwezekani.
Lakini wao wahenga hutulazimisha
kuamini mambo ya ajabu sana. Eti
bila ya haya, wanasema historia ni
mwalimu mzuri sana. Upuuzi tu
huo. Nani kakudanganya eti CCM
itaondoka madarakani?
Hayo yanawezekana tu Kenya,
Zambia na Malawi. Hapa
haiwezekani katu. Tanzania ni
kisiwa cha amani sana. Kisiwa cha
watu tulioridhika kabisa na maisha
yetu. Hakya kweli vile. Taabu yote
ya nini hiyo? Mi nakwambia Mungu
na Ntume mie. Haiwezekani. Hiyo
mifano 14 ni upuuzi mtupu. Ni
kweli. Ni upuuzi mtupu.
Muda? Ha ha hahaaaaa sitaki kuwa
Zuzu, kuamini vitu
visivyowezekana. Kwani pale
mwaka 1967, Ebrahim Hussein
alisema, “Wakati Ni Ukuta”
alinisema mimi? La hasha.
Wanaosema kila jambo lina wakati
wake wanaweza kuwa wehu.
Mie ni mwehu basi!
www.blogger.com/profile/10322331153810581894
 
Back
Top Bottom