Juni 13 ikiwa ni wiki chache kabla ya UK haijapiga kura kujiondoa katika Muungano wa Ulaya, Umoja wa Africa (AU) ulitangaza kuzindua Passport moja kwa nchi zote za Afrika. Wataalamu wa mambo wamesema kuwa itasaidia kukuza uchumi na ushirikiano kwa sababu itapunguza vikwazo vya biashara, itaruhusu watu, mawazo, bidhaa, huduma na mitaji kote barani Afrika bila vikwazo vya mipaka.
Lakini AU inakabiliwa na changamoto moja kuwa ya kuhakikisha kwamba, Passport ya kielektroniki (e-Passport) inafikia malengo yake na si kupelekea ugaidi au wahamiaji haramu.
Passport hii itawaruhusu wananchi kutoka katika nchi washirika kuingia katika nchi yeyote bila ya kuwa na Visa. Lakini kwa kuanzia Passport hizo zitapatikana kwa Wakuu wa Nchi, Mawaziri wa Mambo ya Nje na viongozi wengine wawakilishi kutoka nchi wananchama. Inatarajiwa kuzinduliwa katika mkutano ujao wa AU nchini Rwanda.
Je! Kwanini passport hii ni muhimu?
Passport hii itaruhusu raia kutoka katika nchi wanachama kufanya biashara na kuingiliana kwa kiasi kikubwa. Kiufupi ni kuwa, passport hii ni alama ya umoja katika bara la Afrika, kitu kitakachosaidia kukuza uchumi na siasa ya Afrika.
AU imekuwa ikipigana vikali kuhakikisha kuwa inaondoa mipaka iliyowatenga wa Afrika iliyowekwa na wakoloni na kukuza umeoja na muingiliano kote barani Afrika.
Ni vipi vikwazo vya passport hii?
Vikwazo vingi vinavyojitokeza katika utekelezaji wa passport hii ni kuwa wengi wanahofia masuala ya kigaidi. Usalama wa mataifa hayo umekuwa katika amshaka ya kuweza kuruhusu utumikaji wa passport hii.
Mbali na hilo, suala la usafirishaji wa dawa za kulevya, uenezaji wa magonjwa, ushindani katika upatikanaji wa ajira, wahamiaji haramu na vitu vinavyofanana na hivyo vinachangia utekelezwaji wa passport hii.
Wataalamu wameeleza kuwa mpango huu ni mzuri ila kama utatumika vibaya basi ni wachache tu ndio watakaofaidika na kuwaacha maelfu ya waafrika wakiwa katika umasikini mkubwa.
Lengo kubwa la passport hii ni kukuza umoja wa Afrika ili kupelekea kuinua uchumi wake na kupunguza utegemezi kutoka katika mataifa tajiri barani Ulaya na Marekani.