Wakati ni huu kwa Kikwete kupunguza Mawaziri | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wakati ni huu kwa Kikwete kupunguza Mawaziri

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by The FaMa, Jan 13, 2012.

 1. The FaMa

  The FaMa Senior Member

  #1
  Jan 13, 2012
  Joined: Oct 6, 2011
  Messages: 125
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Wakati ni huu kwa Kikwete kupunguza mawaziri
  Johnson Mbwambo
  Hata hili mpaka tuelekezwe na asasi za Bretton Woods?
  SIKU za karibuni nimekuwa nikifuatilia kwa karibu taarifa mbalimbali kuhusu mwelekeo wa hali ya uchumi wa dunia. Taarifa za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa na tovuti zinazoheshimika za masuala ya uchumi zinaonyesha kwamba hali si nzuri hata kidogo.

  Kwa hakika, tovuti kama ile ya Morgan Stanley Global Economy Forecast inazungumzia hali ya uchumi wa dunia kuwa mbaya kwa kipindi cha muongo mzima ujao.

  Kwa mujibu wa taarifa hizo, uchumi wa dunia kwa mwaka huu wa 2012 utakua kwa kasi ndogo ya asilimia 3.2, utakua kwa asilimia 3 hadi 5 kuanzia mwaka 2013 hadi 2016, na kisha utaporomoka hadi asilimia 2.7 kati ya 2017 na 2025.

  Hii ina maana kwamba kati ya sasa na mwaka 2025 ambao ndio mwisho wa Dira ya sasa ya Taifa ya Maendeleo (Vision 2025), hali ya kasi ya kukua kwa uchumi wa dunia haitakuwa ya kiwango cha kuridhisha - na hii ni habari mbaya kwa watawala wetu na Watanzania kwa ujumla.

  Barani Ulaya tayari wameshaanza kukiona cha moto baada ya euro kusambaratika. Baadhi ya wakazi wa nchi za Ulaya (kama Hispania) wameshaanza kuzikimbia nchi zao na kwenda kutafuta makazi mapya sehemu nyingine duniani (kama vile Australia) ambako uchumi bado haujaathirika sana.

  Kusambaratika huko kwa euro sasa kunatishia kusambaratisha pia uchumi wa Marekani. Kama vile hiyo haitoshi,* hata China ambayo ndiyo kwa sasa yenye uchumi imara, imebashiriwa kuwa uchumi wake kwa mwaka huu wa 2012 nao utakua kwa kasi ndogo kuliko mwaka juzi na jana.

  Ni hali hii ya kusikitisha ya mwelekeo wa uchumi wa dunia iliyomlazimisha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Christine Legarde, atangaze kwamba shirika hilo litashusha rasmi kiwango cha kukua kwa uchumi wa dunia ilichokibashiri.

  Shirika hilo ambalo ndilo lenye wajibu wa kubashiri (forecast) na kutangaza rasmi kiwango cha kukua kwa uchumi wa dunia kinachotarajiwa kila mwaka, lilishatangaza kwamba mwaka huu uchumi ungekua kwa asilimia nne. Sasa Lagarde anasema utakua kwa kiwango cha chini ya asilimia nne.

  Mama huyo alisema hivyo, wiki iliyopita, akiwa Afrika Kusini ambako, kwa mara nyingine tena, aliwasihi viongozi wa bara la Afrika kuanza kuchukua hatua za kujihami (austerity measures) kutokana na kuporomoka kwa uchumi wa Ulaya kulikosababishwa na kutetereka huko kwa euro.

  Katika siku za karibuni tumeshuhudia mataifa kadhaa – makubwa kwa madogo -yakichukua hatua mbalimbali za kujihami na kujifunga mikanda. Mfano mzuri ni Marekani ambako Rais Obama alitangaza kuwa nchi hiyo haitapigana tena vita mbalimbali duniani. “US can no longer fight world’s battles”; ndivyo alivyosema Rais Obama wiki iliyopita.

  Lakini si hivyo tu; kwani Serikali ya Marekani imetangaza pia kusitisha miradi yake mikubwa ya utafiti wa anga za mbali ili kuokoa fedha.

  Katika Afrika; mfano wa haraka haraka unaonijia kichwani mwangu ni wa Nigeria ambako mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Goodluck Jonathan alitangaza kupunguza mishahara ya wafanyakazi wote wa Serikali kwa asilimia 25 na kusitisha safari zote za nje kwa maofisa wake.

  Rais Jonathan alisema kwamba hali ya uchumi wa dunia ni mbaya, na kwamba hakuna njia yoyote ambayo Serikali yake ingeweza kufanya ili iweze kuendelea kutoa ruzuku kwenye bei ya mafuta. Hatua* ya Serikali kufuta ruzuku hiyo imesababisha bei ya mafuta ipande mno Nigeria, na hivyo kusababisha maandamano makubwa nchini humo.

  Habari za kuaminika zinasema kuwa hatua hizo ni maelekezo ambayo Nigeria imepata kutoka IMF na Benki ya Dunia (WB) kupitia kwa Waziri wake wa Fedha, mwanamama Dk. Ngozi Okonjo-Iweala ambaye alipata kuwa mmoja wa maofisa wa juu wa WB.

  Katika kuhakikisha kwamba hata wakubwa serikalini nao ‘wanaumia’ kama waumiavyo wananchi wa kawaida, Rais Jonathan akaamua kuifyeka mishahara ya watumishi serikalini kwa asilimia 25. Ni uamuzi mgumu kuuchukua, lakini usiokwepeka.

  Ndugu zangu,* nikirejea ya hapa nyumbani; ni kwa kuzingatia hayo yote yanayotokea hivi sasa duniani nilikuwa na matarajio makubwa mno na hotuba ya Rais wetu Jakaya Kikwete ya kuuaga mwaka 2011 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2012.

  Nilitarajia kwamba Rais wetu Kikwete si* tu angelieleza taifa kuhusu hatari iliyoko mbele yetu ya misukosuko inayokabili uchumi wa dunia iliyoanzia kwenye kusambaratika kwa euro na kuwahimiza Watanzania kujifunga mikanda, lakini pia nilitarajia angelitangazia taifa hatua kadhaa za kubana matumizi (austerity measures) ambazo serikali yake itachukua.

  Lakini sivyo alivyofanya. Hotuba yake haikugusia kabisa hali hiyo mbaya inayotarajiwa ya uchumi wa dunia, na badala yake alijisifu kwamba uchumi wetu utakua mwaka huu wa 2012 kwa kiwango cha asilimia 7.

  Rais Kikwete alisema hivi: “Pamoja na changamoto hizi, tunatarajia uchumi wetu utakua kwa asilimia* 7 ingawa wenzetu wa IMF wanakadiria kuwa utakua kwa asilimia 6.3”.
  Rais wetu anasema kwamba uchumi wetu utakua kwa asilimia saba, lakini, kama nilivyoeleza, bosi mkuu wa IMF (Mama Lagarde) alieleza wiki iliyopita tu huko Afrika Kusini kwamba uchumi wa dunia utakua kwa asilimia ambazo ni chini ya nne! Sasa; tumwamini hapa nani? Tumwamini Rais Kikwete au Mama Lagarde?

  Nauliza hivyo nikitambua kwamba uchumi wa dunia unaweza kukua kwa asilimia chini ya nne, lakini hapo hapo uchumi wa Tanzania ukakua kwa asilimia hizo saba anazozitaja Rais Kikwete kwa sababu kinachozungumzwa ni wastani tu.

  Kwa hiyo, tofauti hiyo inaelezeka kabisa. Hata hivyo, shaka yangu na takwimu hiyo ya Rais Kikwete ni ya kimazingira zaidi; yaani inazingatia hali iliyopo hivi sasa hapa nchini. Hali ya sasa hapa nchini haiaminishi kabisa kwamba uchumi wetu unakua.

  Mimi si mchumi, lakini haihitaji kuwa mchumi kutilia shaka tambo za kukua uchumi kwa nchi ambayo mfumuko wake wa bei umepanda kutoka wa tarakimu moja (single digit) hadi tarakimu mbili (asilimia 20).

  Mimi si mchumi lakini haihitaji kuwa mchumi kutilia shaka tambo za kukua uchumi kwa nchi ambayo deni lake la taifa la ndani na nje sasa limefikia dola bilioni 700, au kwa nchi ambayo maelfu kwa maelfu ya vijana wanaomaliza chuo kikuu hawana ajira.

  Mimi si mchumi lakini hakika kope sitapepesa nikisikia nchi inatamba kuwa uchumi wake unakua; ilhali kila mwaka Serikali inakopa benki za biashara kuziba nakisi kwenye bajeti yake, na tena inakopa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na si kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

  Kama kuna viashiria vya kusinyaa kwa uchumi wa nchi visivyogusa mambo hayo niliyoyataja, basi, niambieni; lakini mimi na uelewa wangu mdogo naamini kwamba viashiria hivyo pia vimo, na tena vinabeba uzito mkubwa.

  Lakini hata kama utaamua kuvipuuza viashiria hivyo, ni vipi unaweza kuielezea hali ya sasa ya Serikali yetu kushindwa kuwalipa kwa wakati watumishi wake na wazabuni wengi kama sio ukata unaoikabili?

  Ndugu zangu, mwenye macho haambiwi tazama. Kwa sababu ya ukata huo unaoikabili Serikali, mwaka huu mpya wa 2012 tutasikia habari nyingi za migomo ya wafanyakazi au ya wanafunzi wa vyuo vikuu au hata watoa huduma mbalimbali kwa sababu ya ucheleweshaji wa malipo yao ambao chanzo kikuu ni ukata wa Serikali ambao nao chanzo chake kikuu ni kutetereka kwa uchumi wa dunia.

  Ni kwa kuzingatia yote hayo namshauri Rais Kikwete afuate mapema njia aliyoifuata Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria kabla mambo hayajaharibika kabisa. Namaanisha akutane haraka na jopo lake la washauri wa kiuchumi kuangalia namna Serikali inavyoweza kubana matumizi yake, na umma utangaziwe hatua hizo.

  Haitoshi tu kuchukua hatua moja (tena kimya kimya) ya kusitisha ajira mpya zilizopitishwa kwenye bajeti. Kinachotakiwa na kinachoweza kutuokoa ni uchukuaji wa hatua kadhaa za kubana matumizi na si hatua moja tu.

  Kwa mfano; badala ya Rais Kikwete kusubiri alazimishwe na asasi za fedha za Bretton Woods (IMF na World Bank), angeanza kupunguza ukubwa wa baraza lake la mawaziri.

  Baraza la sasa ambalo ni sawa na timu nne za soka haliendani kabisa na mazingira ya sasa ya ukata wa Serikali na ni mzigo mkubwa kwa walipakodi. Isitoshe, tuna wizara ambazo hata ukizifuta hakuna cha mno tutakachoki-miss.

  Huwa (kwa mfano) wakati mwingine najiuliza; Hivi Waziri wa Habari, Utamaduni na Vijana anafanya nini kila siku anapokwenda kazini? Hivi Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia* na Watoto naye ana kazi gani anazozifanya kila siku?

  Kwa ufupi, kuna wizara ambazo hazina shughuli zozote kubwa (ama kwa sababu ya ufinyu wa bajeti zao au ukosefu wa ubunifu) ambazo zinaweza kufanywa vitengo tu katika wizara nyingine na mambo yakaenda. Sote tunajua wizara hizi ziliundwa kwa malengo ya kisiasa ya kuwatafutia wanamtandao nafasi za uwaziri.

  Ukizichunguza baadhi ya wizara hizo utagundua kwamba wanaoziongoza ni wale ambao shughuli zao kubwa huwa ni kuhudhuria semina, warsha na mialiko mbalimbali.

  Baada ya kulipunguza baraza lake la mawaziri, Rais Kikwete anaweza kuangalia maeneo mengine kama vile kupunguza siku za vikao vya Bunge, kufuta posho zote serikalini, kusimamisha safari zote za nje ya nchi kwa maofisa wa serikali na kuanzisha kodi maalumu (special levies) kwa matajiri wakubwa nchini na kwa kampuni zinazotengeneza faida kubwa kama ilivyofanya Ugiriki.

  Kwa hakika, anaweza kwenda mbali zaidi na kusitisha uanzishaji wa mikoa mipya na wilaya mpya hadi hapo uchumi wa nchi utakapotengemaa.

  Sote tunajua kwamba uanzishaji wa wilaya na mikoa mipya ni kitu kinachohitaji mabilioni ya shilingi; fedha ambazo kila dalili zinaonyesha kuwa serikali yetu imekaukiwa nazo kwa sasa.

  Asipochukua hatua hizi katika kipindi hiki ambacho msaada kutoka kwa “wajomba” wa Ulaya na Marekani hautaonekana kwa sababu na wao wanapigana kivyao, Rais Kikwete atalazimika kukopa tena na tena kutoka katika benki za kibiashara hadi deni la taifa lifikie trilioni za dola.

  Itabidi akope tena na tena kwenye benki hizo za kibiashara za hapa nchini (Standard Bank, Barclays Bank, Stanbik); vinginevyo nakisi katika bajeti ya Serikali yake itamkosesha usingizi kwa ukubwa wake.

  Vyovyote vile; asipopunguza matumizi ya Serikali yake na kuziba nakisi kwenye bajeti, hatutashangaa mwaka huu wa 2012 ukitawaliwa na migomo ya kudai malipo yaliyocheleweshwa na minyukano mingine inayoambatana na uchumi wa nchi kudorora.

  Tafakari!

  Source: Raia Mwema, Januari 11, 2012
   
 2. Chimunguru

  Chimunguru JF-Expert Member

  #2
  Jan 13, 2012
  Joined: May 3, 2009
  Messages: 9,843
  Likes Received: 270
  Trophy Points: 180
  Nadhani ni wakati muafaka hata yeye kutoka madarakani
   
Loading...