Wakala wa Vipimo (WMA) wataka wananchi kutoa taarifa

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,009
9,874
Wakala wa Vipimo (WMA), imewataka wananchi kutokuwa waoga wa kutoa taarifa zitakazowafichua watu wanaochezea na kuharibu vipimo kwa lengo la kuwapunja wauzaji wa bidhaa mbalimbali.

Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa WMA, Deogratius Maneno, alisema hayo jana katika Viwanja vya Nyakabindi, mjini hapa wakati wa maonyesho ya Nanenane yanayoendelea.

Alisema taarifa hizo zitolewe kupitia ofisi za wakala zilizoko katika mikoa yote ya Tanzania Bara au kupitia namba yao ya simu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97 ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.

Maneno aliwataka wafanyabiashara kufanya kazi zao kwa uadilifu na kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa kwani adhabu zitolewazo kwa wakiukaji wa Sheria ya Vipimo ni kali.

Kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura na. 340 na mapitio yake, endapo mtu yeyote atabainika kutenda kosa kinyume cha sheria hiyo na akakiri kutenda kosa husika, atapaswa kulipa faini isiyopungua Sh. 100,000 na isiyozidi Sh. milioni 20 kwa kosa la kwanza.

Alisema endapo mtuhumiwa atakataa kukiri kosa na kufikishwa mahakamani na akabainika kutenda kosa hilo, atatozwa faini isiyopungua Tsh. 300,000 na isiyozidi Sh. 50,000,000 au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Pia alisema endapo mtuhumiwa atakamatwa na kosa kwa mara ya pili na kuendelea na akipelekwa mahakamani akakutwa na hatia, adhabu ni faini isiyopungua Sh. 500,000 na isiyozidi Sh. 100,000,000 au kifungo kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.

Alisema kwa sasa WMA inafanya pia uhakiki wa dira za maji, hivyo wananchi watembeleapo banda lao watapata fursa ya kujifunza namna ya kutambua dira ambazo zimehakikiwa na kufungwa lakiri ya wakala.

Nipashe
 
Back
Top Bottom