Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,498
- 9,279
OFISI ya Makamu wa Rais imetoa mwongozo wenye vipengele tisa kwa wakaguzi na watekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki katika halmashauri zote nchini, utakaoanza kutumia Juni mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 23, mwaka huu, wakaguzi wameagizwa kutumia busara kutekeleza agizo hilo huku matumizi ya nguvu ikiwamo kuwapiga au kuwabeba watu na kuwaweka ndani yakikatazwa.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, vipengele hivyo ni kuwataka wakaguzi kufanya ukaguzi huo madukani, magengeni, viwandani, masokoni, mipakani, kwenye maduka makubwa na maeneo mengine yanayouza bidhaa.
Kipengele cha pili cha mwongozo huo ni kuwataka wakaguzi wote wajitambulishe na kuonesha vitambulisho vyao kwa wahusika kwenye maeneo wanayokagua, huku ukiwakataza wakaguzi kuwasimamisha watu au mtu na kumpekua au kupekua migizo yake ili kutafuta mifuko ya plastiki.
Vilevile, mwongozo huo unamkataza mkaguzi kutoingia kwenye makazi ya watu au kusimamisha magari au vyombo vingine vya usafiri ili kutafuta mifuko hiyo.
Taarifa hiyo ya Ofisi ya Makamu wa Rais ilisema, lakini iwapo magari au vyombo vingine vya usafiri vitasimamishwa kwa sababu nyingine na kukutwa na shehena ya mifuko ya plastiki, adhabu stahiki itatolewa na wahusika wataelekezwa mahali mahususi kwa kupeleka shehena hiyo.
Aidha, ilisisitiza kuwa atakayekutwa na kosa la kuendelea kuuza, kuhifadhi au kutumia mifuko hiyo ya plastiki kuanzia Juni Mosi, mwaka huu, ataelekezwa mahali pa kuipeleka kisha atapigwa faini na kupewa muda wa kulipa na iwapo atakataa kusaini au kushindwa kulipa katika muda aliopewa, atafunguliwa mashitaka.
Kadhalika, watakaotozwa au kulipa faini watapewa risiti za serikali kwa malipo hayo na pia mwongozo huo ukiwaonya pia wale wote watakaokaidi kwa kutotoa ushirikiano katika ukaguzi huo, kuzuia au kuhujumu utekelezaji wake, kuwa watachukuliwa hatua kali zaidi kwa mujibu wa sheria nyingine za nchi.
Aprili mwaka huu serikali ilitoa taarifa rasmi ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza kutumika Juni Mosi, mwaka huu na kuwataka wazalishaji, wauzaji na wanunuzi kutumia mifuko mbadala. Sambamba na hilo, pia elimu imeendelea kutolewa kuhusu matumizi mbadala wa mifuko hiyo na kuwataka wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia fursa hiyo kuzalisha mifuko rafiki wa mazingira.