Wajumbe wa Bunge Kamati ya NUU watembelea Miradi ya Kikanda ya EAC

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,806
11,968
Wizaraa (4).jpeg

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakifuatilia kwa makini mada kuhusu utekelezaji wa miradi ya kikanda ya miundombinu ya EAC iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliabi Chodota.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) chini ya Mwenyekiti wake, Vita R. Kawawa, wameitaja Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama Jumuiya yenye maono na inayatafsiri kivitendo maono yake.

Wameeleza hayo wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya kikanda ya Barabara ya EAC iliyofanyika katika Mikoa ya Dodoma, Manyara na baadaye Arusha kuanzia tarehe 02 hadi 04 Septemba 2022.

Ziara hiyo iliyoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilitoa fursa kwa wajumbe wa Kamati ya NUU kujionea baadhi ya miradi ya Jumuiya na namna Tanzania inavyoshirikiana na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama kutekeleza miradi hiyo, kuanzia kufanya uchambuzi yakinifu na baadaye kutafuta fedha za utekelezaji.
Wizaraa (3).jpeg

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) wa Mkoa wa Arusha, Bw. Paul Kamukulu akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Namanga kwa wajumbe wa Kamati ya NUU walipotembelea kituo hicho tarehe 03 Septemba 2022.

Wajumbe walielezwa kuwa Tanzania imepakana na nchi tano za EAC ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na katika nchi zote hizo kuna miradi ya barabara ya kuiunganisha Tanzania na nchi hizo ambayo baadhi yao imekamilika, mingine ipo katika hatua za ujenzi na mingine inatafutiwa fedha ili iweze kutekelezwa.

Miradi michache ambayo ipo katika ujenzi ni pamoja na barabara ya kutoka Kabingo, Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilomita 260 inayounganisha Tanzania na Burundi. Barabara ya kutoka Tanga, Pangani, Saadan hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilomita 256 inayounganisha Tanzania na Kenya. Ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha pia daraja la Pangani la mita 500.

Kwa upande wa Tanzania na Uganda, kuna mradi wa barabara ya Mutukula, Kiyaka, Kasulu hadi Benako yenye urefu wa kilomita 124 na Bugene, Burigi, Chato hadi Kasulo yenye urefu wa kilomita 68.

Wakikagua barabara ya kikanda ya Arusha, Namanga, Ath River pamoja na barabara ya mzunguko ya Arusha, wajumbe wlielezea namna ujenzi wa barabara hizo unvyounganisha nchi wanachama wa EAC na kuchochea biashara, muingiliano wa watu na hatimaye kuimarisha mtangamano wa EAC.

Walisisitiza umuhimu wa nchi zote wanachama kuwa wamoja bila kujali mipaka ya nchi zao ili kwa pamoja waweze kutafutia ufumbuzi wa changamoto zinazotokana na utekelezaji wa miradi hiyo.

Wajumbe wa Kamati hiyo ambao pia walitembelea Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Namanga, walisikiliza mada kutoka kwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota. Mada hiyo pamoja na mambo mengine, ilieleza miradi mingine inayotekelezwa kwa uratibu wa EAC katika sekta za usafiri wa anga, reli, majini; hali ya hewa na nishati katika nchi wanachama wa Jumuiya.

Wizaraa (2).jpeg

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala, Mhandisi Steven Mlote akiongea jambo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) ilipotembelea Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mshariki jijini Arusha kabla ya kuanza kutembelea miradi ya miundombinu ya EAC inayotekelezwa mkoani humo. Mwingine katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati ya NUU, Vita R. Kawawa
 
Back
Top Bottom