Ngaliba Dume
JF-Expert Member
- Oct 6, 2010
- 1,710
- 3,675
Mgogoro wa uchaguzi visiwani Zanzibar umeingia katika sura nyengine baada Wawakilishi na Madiwani wateule wa Chama Cha Wananchi CUF kufikiria kwenda mahakamani kutetea uongozi wao.
Wamesema tayari Wawakilishi na Madiwani hao wateule walishachaguliwa na kukabidhiwa hati zao za ushindi kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, na kwamba hadi sasa hakuna mgombea wa nafasi hizo kutoka chama chochote aliyekwenda mahakamani kupinga uteuzi wao.
Msimamo huo wa CUF umetolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, katika mkutano maalum wa Chama hicho uliofanyika viwanja vya “nngoma hazingwa” Chake Chake Pemba.
Mkutano huo umewajumuisha viongozi wa Wilaya, Majimbo na Jumuiya za Chama hicho Kisiwani humo ambapo mkutano kama huo ulifanyika jana kwa upande wa Unguja.
Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea Urais wa Chama hicho amesema viongozi hao waliochaguliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 na kupewa shahada zao, watakwenda mahakamani kutetea nafasi zao, na kutoruhusu viongozi wengine wa ngazi hizo kuchaguliwa tena kwa vile wao wanavyo vielelezo vyote vya kuchaguliwa kwao.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi yaliyobandikwa katika vituo vya kupigia kura na kuthibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo, majimbo yote 18 ya uchaguzi Kisiwani Pemba yalichukuliwa na CUF, sambamba na wadi zote 32 za uchaguzi.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amewapa matumaini wafuasi wa Chama hicho kwamba atatangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 na hatimaye kuiongoza Zanzibar.
Amerejea kauli yake kuwa wanachokifanya watawala hivi sasa ni kuchelewesha kumtangaza, lakini hakuna namna yoyote ya CCM kuendelea kuongoza Zanzibar baada ya uchaguzi wa 2015 na kwamba uongozi uliopo hivi sasa ni batili kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Amesema Jumuiya na waangalizi wote wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa wameshuhudia uchaguzi huo na kujiridhisha kuwa ulikuwa huru, haki na wa uwazi na wanaendelea kushikilia msimamo wao kutaka mshindi wa uchaguzi huo atangazwe.
Amesisitiza kuwa Chama chake hakitoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20/03/2015, kauli ambayo pia imeungwa mkono na wafuasi wa Chama hicho kisiwani Pemba, kama ilivyokuwa kwa upande wa Unguja.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, amemtaja Maalim Seif kuwa kiongozi aliyebobea kisiasa na anayejali maslahi ya Wazanzibari.