Wajibu Wa Wananchi Kwenye Uchaguzi Mkuu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wajibu Wa Wananchi Kwenye Uchaguzi Mkuu

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by X-PASTER, Aug 24, 2010.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Aug 24, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 106
  Trophy Points: 160
  Wajibu Wa Wananchi Kwenye Uchaguzi Mkuu

  ZIKIWA zimesalia miezi michache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba ni muhimu kwa kila mwananchi kujua jukumu lake katika kipindi hiki muhimu. Kipindi ambacho kama kutakuwa na maandalizi na mikakati ya kweli nchi itakombolewa kutoka kwa watu wachache wanaofaidi matunda ya uhuru.

  NCHI inapokuwa chini ya utawala mzuri kila mtu atafurahia bila kujali kuwa yeye ni tajiri au masikini, mkulima au mfanyakazi, mkereketwa wa chama tawala au la; Matunda ya utawala bora hautajali misingi ya dini wala kabila, watu wote watakuwa sawa na wenye furaha ya uhuru!

  Lakini kinyume chake nchi itakapo kuwa na utawala mbovu; unaoendekeza ubinafsi, ubaguzi, utawala usiofuata na kuheshimu sheria zake zenyewe, utawala usiokuwa na mipango ya kiutekelezaji. Serikali inayoshindwa kupambana na rushwa, ubadhirifu na uonevu kwa wananchi basi watakao athirika zaidi ni wananchi wa hali za chini, wanyonge wa sio na kitu.

  Katika utawala mbovu wale wenye nacho au waliopewa nafasi maalumu ya upendeleo katika utendaji wa serikali hawata athirika. Wao watasikilizwa kwa kila watakacho kitaka. Wanyonge na masikini watabaki kuwa hivyo kwao afya bora ni vitu vya kusikia tu, elimu bora ni ndoto za mchana. Watoto wao ndiyo watakao acha shule kwa kukosa ada. Siku zote watasimangwa kuwa si watu wanaopenda elimu na ilihali utawala ndio unaowafanya wawe hivyo.

  Na litakapo tokea tatizo lolote kama ukame na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu wao na watoto wao ndiyo watakao kufa kama nzige.

  Hii ndiyo hali halisi ya maisha ya Watanzania zaidi ya asilimia 80 mijini na vijijini. Wanachi wanyonge wanawajibika bila kujali itikadizao za kisiasa, dini, wala kabila kuhakikisha kuwa wanabadilisha hali zao za kimaisha kwa kusaidia kuuweka utawala ulio bora utakao waondolea matatizo waliyonayo.

  Njia kuu ya kuhakikisha kuwa nchi inapata utawala bora ni kwa kushiriki katika kutoa elimu ya demokrasia, kuhamasisha jamii kuwa na mwamko wa kisiasa. Ni muhimu wananchi wakaelimishwa nani mbaya wao. Wananchi wanapaswa kuambiwa kuwa inawezekana kabisa utawala uliopo unaweza kuondolewa madarakani kwa njia ya kura.

  Katika kutoa elimu ya Demokrasia si lazima kuandaa mikutano ya hadhara elimu ya demokrasia inaweza kutolewa kwa njia mbali mbali kutegemea na nafasi ya mtu na mazingira yaliyopo. Kwa mfano (1) kuanzisha mijadalakwenye mikusanyiko ya watu, kwenye mabasi, mabaraza ya jioni na kadhalika.

  Pili kuhamasisha watu walio karibu nawe, marafiki, ndugu na jamaa. Hapa unaweza hata kuwaandikia barua kwa wale walio mbali bila kujali chama chao. Wahamasishe na uwaandae kwa uchaguzi wawe tayari kuleta mabadiliko kwa kura. Toa mifano iliyo hai inayogusa halihalisi ya maisha yao.

  Katika familia zetu za Kiafrika, ukoo ni taasisi pana sana, kuna upande wa mama na upande wa baba. Hao wote wanahitaji elimu ya uchaguzi. Ujumbe ukiwafikia wote basi utakuwa umefanya kazi ya ziada.

  Tatu tunaweza kuanzisha vikundi mbali mbali vya kutoa elimu ya demokrasia. Vikundi hivi vinaweza kutembea sehemu mbali mbali kutoa elimu. Huu si wakati wa kuwaachia wanasiasa pekee yao kutembea sehemu zote. Kutokana na vikwazo mbalimbali si rahisi kwao kutembea sehemu zote za nchi. Hata vyombo vya habari navyo havifiki sehemu zote na vile vinavyofika sehemu zote kwa namna moja au nyingine vinapigia debe serikali ilioko madarakani.

  Pia huu si wakati wa kusifia tu Ah Lipumba ni kiboko bwana! Anachambua uchumi ile mbaya! Oh Dr Slaa anawakanyaga CCM kisawa sawa! Hii haitoshi ni lazima nasisi tuchukue nafasi zetu. Wakati kama huu kila mtu ni lazima awe mchezaji, mfungaji magoli.

  Kwa sasa haifai mtu kuwa mshangiliaji. Tuwe washangiliaji baada ya uchaguzi kwisha sio leo. Sote ni jukumu letu kuondoa dhulma kwa vinywa na mikono yetu.

  Tusiwaachie walewanaofaidi matunda ya uhuru kutoa elimu ya uraia peke yao kila inapowezekana tuandae semina, warsha, na makongamano ya utawala na demokrasia. Wasomi mnao elewa nini maana ya utawala mbovu msijitenge na jamii. Si kila msomi anaelewa nini maana ya utawala mbovu mfano wa hao ni wale wanaoandaa na kushiriki mikutano ya kuipongeza serikali kwa kile kinacho daiwa kusamehewa madeni. Hawa ni wasomi wasioelewa kitu wako tayari kuwasaliti wananchi kwa thamani ndogo tu.

  Wanyonge katika kipindi hiki wasichoke kuleta mazungumzo ya kisiasa misikitini, makanisani, mashuleni na hata kupiga simu redioni kuchangia mada mbali mbali zenye mwelekeo wa kisiasa. Wanyonge hawapaswi kuziacha nafasi adimu kama hizi.

  Kwenye siasa hakuna dogo na mshindi hupatikana hata kwa kura moja. Mfano mmoja wa mgombea anaweza kuongoza kwa kura 2000 tu! Kwa hiyo kura kama hizo pia zinaweza kuiondoa CCM madarakani. Ni jukumu lako ndugu msomaji kuanza leo kushiriki kuhamasisha na kutoa elimu ya uchaguzi. Siku nilizozitaja hapo juu si nyingi. Anza leo.
   
Loading...