Wajerumani wachefuliwa na ufisadi kwenye miradi; Wafadhili wakiondoka Miradi hiyo hufa...

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797

Na Nickson Mahundi

UBALOZI wa Ujerumani nchini Tanzania umesema ubabaishaji uliokithiri nchini, ndio unakwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya maji safi na salama nchini.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mratibu wa Miradi ya Maji kutoka nchini Ujerumani, Bi. Andrea Moser wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI), Bw. Aggrey Mwamri kufunga mkutano wa wadau wa maji.

"Serikali ya Ujerumani ina fedha za kutosha kuisaidia Tanzania kutatua tatizo la maji, lakini tatizo limekuwa katika kutoa ripoti na uhalisia wa utekelezaji wa miradi ikilinganishwa na fedha iliyotumika," alisema Bi. Moser na kuongeza;

"Kama suala hilo lingetekelezwa nina imani serikali yetu ingetoa kipaumbele kwa kutoa misaada zaidi ya kusaidia miradi ya maji safi na salama," alisema Bi. Moser.

Bi. Moser alisema wao kama wasimamizi ya miradi inayotekelezwa nchini wamekuwa wakipata wakati mgumu pale wanapoulizwa na Bunge la Ujerumani kuhusu miradi inayotekelezwa nchini kutoenda sambamba na uhalisia wa fedha zinazotolewa.

Alisema jambo la kushangaza ni miradi hiyo kutotolewa taarifa wala kutekelezwa ipasavyo.

"Ndugu zangu waandishi nyie mninukuu kwa haya ninayosema, kwani tumekuwa tukihojiwa juu ya fedha zinazoletwa Tanzania, lakini miradi inayotekelezwa inaonesha kuwepo ubadhirifu mkubwa kutokana na ripoti zinazotolewa na utekeleza wa miradi ya maeneo husika," alisema na kuweka wazi kuwa fedha za kusaidia miradi zipo nyingi lakini hazitolewi na nchi yake kutokana na kasoro za aina hiyo.

Awali, Bw. Mwamri akifunga mkutano huo alikiri kuwa uwezo wa watendaji kusimamia miradi kuanzia ngazi ya halmashauri za vijiji ni mdogo, hivyo jamii inapaswa kuelimishwa ili iweze kupata uelewa wa kutosha na kuitunza.

Alisema miradi mingi inayoletwa na wafadhili, jamii inakuwa haijashirikishwa kikamilifu, hivyo wafadhili wanapoondoka miradi hiyo hufa kutokana na uelewa mdogo wa jamii.

"Tumekuwa na asasi ambazo zinaanzisha miradi vijijini, lakini hazishirikishi jamii ili kujua tatizo kama ni maji au kitu kingine, ndio maana wafadhili wakiondoka miradi hiyo hutoweka kutokana ukweli kwamba haikuwa na hitaji la wananchi," alisema.

Bw. Mwamri alisema serikali imeanzisha mpango wa kamati za vijiji ambazo zitaibua matatizo ya jamii na kuiendeleza miradi mbalimbali inayoanzishwa na wafadhili ikiwa pamoja na utoaji wa ripoti sahihi za utekelezaji.
 
Back
Top Bottom