Manispaa ya mji wa Luasanne, Uswizi, imechana fomu za maombi ya uraia ya Waislam wawili wanandoa kwa sababu ya kukataa kwao kupeana mikono ya salamu na watu wa jinsia tofauti.
Mstahiki Meya wa Luasanne, Gregoire Junod, amesema mamlaka hiyo imekataa kupokea maombi hayo kwa sababu watu hao hawaheshimu usawa wa jinsia. Alisema, waliwahoji waombaji hao mieze kadhaa iliyopita kutaka kujua kama wanafikia vigezo vya uraia na waling'amua kwamba walipungukiwa kwenye eneo la utangamano.
Pia walikuwa na wakati mgumu kujibu maswali yaliyoulizwa na maofisa wa jinsia tofauti, alisema Meya huyo.
Baadhi ya Waislamu wasalihina wanadai Uislam hauruhusu kugusana kimwili na yeyote wa jinsia tofauti, isipokuwa tu na baadhi ya wanafamilia wa karibu.
Mstahili Meya Junod alieleza kwamba uhuru wa kidini na kuamini umesimikwa kwenye sheria za Canton of Vaud, ambayo inajumuisha Lausanne. Lakini "mafanyizi ya kidini hayaangukii nje ya sheria," alisisitiza.
Kwa upande wake Naibu Mstahiki meya, Pierre-Antoine Hildbrand, ambae alikuwepo kwenye jopo lililowahoji wanandoa hao alisema ameridhishwa na uamuzi huo wa kukataa maombi hayo kwa vile "Katiba na usawa kati ya wake na waume uko juu ya ubaguzi."
Wanandoa hao wana siku 30 za kukata rufaa.
Hii si mara ya kwanza kuibuka sintofahamu nchini Switzeland juu ya Waislamu na kupeana mikono.
Mwaka 2016 ilitokea taharuki nchi nzima baada ya sekondari moja Kaskazini mwa nchi hiyo kuwakubalia wanandugu wawili wenye asili ya Syria kutowapa mikono waalimu wao wa kike baada ya kulalamikia utaratibu huo kuwa ni kinyume na misingi ya dini yao.
Ruksa hiyo ilipingana vikali na desturi zilizojichimbia za Kiswizi za wanafunzi kuwapa mikono walimu kama alama ya nidhamu na utii, na katikati ya mtafaruku huo na vilio ya kitaifa mamlaka ya kikanda ilitengua uamuzi wa shule hiyo.
Chanzo: The Guardian