Wahusika wa madudu katika ripoti ya CAG wawajibike

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Kwa vyovyote itakavyochukuliwa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha wa 2010/11 si nzuri hata kidogo. Hali ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa inatarajiwa. Hali hii kwa bahati mbaya sana inatokea wakati wananchi wakilalamika kutokana na kuzidi kuongezeka kwa ugumu wa maisha.

Katika ripoti hiyo inayoishia Juni 2011, iliyotolewa wiki iliyopita, misamaha ya kodi inatajwa kuwa moja ya maeneo ambayo serikali inapoteza mapato yake kwa kiwango kikubwa mno. Misamaha hiyo inaelezwa kuwa imepunguza makusanyo ya taifa yenye thamani ya Sh. trilioni 1.02 sawa na asilimia 18.


Ripoti ilifafanua kuwa taarifa za mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zilionyesha kuwa misamaha iliyotolewa kwa taasisi mbalimbali ina thamani ya Sh. 1,016,320,300,00 ikiwa ni sawa na asilimia 18 ya makusanyo yote ambayo yalikuwa ni Sh. 5,550,205,244,378 kwa mwaka wa fedha wa 2010/11.


Ingawa kiwango hiki ni kikubwa kwa hali halisi ya uchumi wetu, pia ni kikubwa kikilinganishwa na viwango vya misamaha vinavyotolewa kwenye nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda ambazo ndizo tunashindana nazo katika soko la ajira, uwekezaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Habari si mbaya kwa mishamaha ya kodi tu, hata kwenye deni la jumla la taifa hali ni mbaya. Deni hilo limeongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh. trilioni 10.5 mwaka 2009/10 hadi Sh. trilioni 14.44) mwaka 2010/11. Hali hii haonyeshi kuimarika kwa uchumi wetu na kujivua kitanzi cha madeni makubwa ya nje.

Hali ni hiyo hiyo kwenye mikataba kwani ukaguzi umeonyesha kuwa usimamizi wa mikataba bado ni changamoto kubwa ya taifa hili.

Eneo hili linakabiliwa na changamoto zifuatazo, usimamizi mbovu wa mikataba kulingana na Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA); baadhi ya mikataba kukosa nyaraka muhimu kama vile masharti ya mikataba, michoro na maelezo ya kina ya jinsi ya kuitekeleza; kutotumika kwa kifungu cha fidia kwa kuchelewa kutekelezwa; na kutokuwepo mipango ya kudhibiti na kutoa hakikisho la ubora katika utekelezaji wa mikataba.

Mbali na udhaifu katika maeneo haya, bado ugonjwa sugu wa watumishi hewa umeendelea na safari hii kiasi cha Sh. bilioni moja kimelipwa kama mishahara kwa watumishi wa halmashauri ambao hawapo; kutokuwasilishwa kwa
vitabu vya stakabadhi za mapato kutoka halmashauri vyenye thamani ya Sh. 4,227,984,618.

Tumegusia maeneo haya machache hapo juu kueleza hali ilivyo ndani ya serikali, ingawa kimsingi maeneo mengi yametajwa kujaa changamoto nyingi ambazo katika sura ya kawaida yanaakisi ulaghai wa baadhi ya watumishi wa umma katika kutengeneza mazingira ya kuiibia serikali.


Ni dhahiri mwaka baada ya mwaka CAG amekuwa akitoa ripoti mzuri, na mara nyingi kumekuwa na maswali ya umma kwa ujumla wake, kwamba nini faida ya kuwa na ripoti hizi mwaka baada ya mwaka kama wahusika hawafanywi lolote kutokana na mapungufu yanayojitokeza kwenye ripoti hiyo?


Mwaka jana Rais alipata kutamka hadharani kuwa katika maeneo ambayo ripoti ya CAG inaonyesha dhahiri kuwa kulikuwa na wizi wa fedha za umma kwa watumishi wake, taarifa ipelekwe polisi na wahusika washitakiwe.


Ni mapema mno kusema kuwa amri hii imetekelezwa kwa kiwango gani, lakini itoshe tu kutaja hapa kasoro za kiutendaji kwa watumishi wa umma zinazojitokeza katika ripoti ya CAG zimekuwa ni kilio cha umma kwa muda mrefu.


Ndiyo maana nasi leo tunasema pamoja na ripoti nzuri ya CAG na kwa kweli ikiongezewa nguvu na ripoti za kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali za Mitaa (PLAC); Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC); Hesabu za Serikali (PAC), ambazo zimekuwa

wakati wote zikitaka kuwepo kwa uwajibikaji kwa mapungufu hayo, tunasisitiza kuwa itakuwa na nguvu na maana kwa umma kama kweli watu watawajibishwa.

Ni kwa maana hiyo CAG anapaswa kuongezewa nguvu kisheria ili ripoti yake ikishatolewa, basi hiari ya uwajibikaji kwa waliokutwa na makosa isiwepo tena, kwa kufanya hivyo tutajenga uwajibikaji serikalini na hivyo fedha za umma kutumika kwa kazi zilizokusudiwa.

CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom