Wahariri waazimia kuendelea kusaka nyaraka za mafisadi

mwanaizaya

Senior Member
Apr 26, 2008
133
1
Wahariri waazimia kuendelea kusaka nyaraka za mafisadi

Na Reuben Kagaruki

WAHARIRI wa vyombo vya habari nchini wameazimia kuendelea kutafuta nyaraka zinazohusiana na ufisadi na kuzichapisha kwa lengo la kufichua maovu yanayofanyika bila kuogopa vitisho.

Msimamo huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Bibi Sakina Datoo, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa wahariri uliofanyika Dar es Salaam ili kutoa tamko kuhusiana na tukio la makachero wa Polisi kuvamia ofisi za gazeti na MwanaHalisi na nyumba ya Mhariri Mtendaji wake, Bw. Saed Kubenea.

"Tungekuwa hatutafuti nyaraka za siri, leo hii Tanzania tungekuwa wapi? Tunazitafuta kwa sababu tuna uchungu na nchi yetu, kazi yetu si kuwafurahisha watu wachache.

"Tukiogopa kutafuta nyaraka za siri tutaonekana mafisadi ...tutafanya hivyo kwa sababu sisi ni Wazalendo tunaipenda nchi yetu," alisema, Bibi Datoo.

Alisema kama waandishi wa habari wangeogopa kutafuta nyaraka za siri na kufichua ukweli, uozo wa mikataba ya Richmond, madini na Kiwira isingejulikana.

Alisisitiza kuwa Jukwaa la Wahariri linapinga kitendo cha Polisi kuvamia ofisi za gazeti na MwanaHalisi na kufanya upekuzi hasa kwa kuzingatia kuwa waandishi wa habari wako mstari wa mbele kupiga vita rushwa.

Alisema na kusisitiza kuwa Bw. Kubenea si mhalifu bali ni jasiri na mzalendo anayetetea nchi yake.

Aliongeza kuwa kitendo kilichofanywa na Polisi kinaingilia uhuru wa vyombo vya habari kwa lengo la kuwatisha wanahabari ili waache kuandika habari muhimu.

"Sisi kama wahariri tuna heshima zetu, sio kama wahalifu wa mitaani," alisema na kutoa mwito kwa wahariri kutoogopa kwani kufanya hivyo kutakwamisha maendeleo ya nchi.

Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilisema linaamini kuwa kitendo cha Polisi kuvamia ofisi za MwanaHalisi linahusiana na habari za uchunguzi ambazo zimekuwa zikiandikwa nalo.

Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAJA), kilisema katika nchi yenye ufisadi mwandishi wa habari akilalamikiwa, nchi hiyo inakuwa imejaa vitendo vya kifisadi.

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN), ilisema kitendo kilichofanywa na Polisi ni mlolongo wa matukio ya kukwamisha juhudi za upatikanaji habari.

Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (HLRC), kilisema kitendo kilichofanya na Polisi kinawanyima wananchi haki ya kupata habari na alilitaka Jeshi la Polisi kuacha vitisho ili wananchi waendelee kupata habari muhimu.

Asasi za Kiraia Zinazopigania Haki ya Upatikanaji Habari, ilisema Ibara ya 18 ya Katiba inawapa wananchi haki ya kupata habari. "Kitendo cha Polisi kuvamia ofisi za MwanaHalisi kinapindua Katiba," alisisitiza.

Bw. Kubenea alisema gazeti lake halitaogopa kuandika habari za viongozi wasio waadilifu. "Sisi hatuogopi, tuna namba za akaunti za viongozi wote wanaojilimbikizia mali ndani na nje...hatutafuti akaunti ya mkulima wa korosho kule Mtwara au kahawa aliyepo Kagera," alisema

Alisema hata Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Bw. Robert Manumba, kama ana mashaka kuwa si mtu safi naye MwanaHalisi itamchunguza.
 
umoja ni nguvu, ..........waanishi wa habari kuweni pamoja kutuhabarisha wananchi. ufisadi uliotawala nchi hii hauwezi kuondoka bila ya kazi zenu.
 
matokea yake CCM wametolea kauli tukio la kuvamia mwanahalisi kama vile wao ndio wasemaji wa jeshi la polisi. inasikitisha
 
"Tungekuwa hatutafuti nyaraka za siri, leo hii Tanzania tungekuwa wapi? Tunazitafuta kwa sababu tuna uchungu na nchi yetu, kazi yetu si kuwafurahisha watu wachache.

"Tukiogopa kutafuta nyaraka za siri tutaonekana mafisadi ...tutafanya hivyo kwa sababu sisi ni Wazalendo tunaipenda nchi yetu," alisema, Bibi Datoo.



They fear you because you are Young

They fear you because you are the future generation

They fear you because you are powerful.

Amandla...........ngawethu
 
Uzuri wa kuenzi Rushwa ndo huo.

Jana ulitoa Rushwa kuziba midomo watu; leo wapokea Rushwa kuwashughulikia wale wasiotaka kunyamaza, kesho Rushwa hiyo hiyo inapokelewa na watu kadhaa miongoni mwa watu wako kwa nia kukufunua makalio na kuonyesha aibu yako hadharani.
Rushwa nyumbani kwao wapi??


Huo ndo uzuri na utamu wa Rushwa.
 
Back
Top Bottom