Wahariri kutoka Jukwaa la Kimataifa Waipongeza Serikali ya Tanzania

blix22

JF-Expert Member
Jun 23, 2013
213
645
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wahariri kutoka Jukwaa la Kimataifa la Wahariri na Wanahabari Duniani (International Press Institute, IPI) wameeleza kufurahishwa na mwitikio wa Serikali ya Tanzania katika kuboresha taaluma ya habari nchini.

Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari, Jijini Dar es Salaam leo Alhamisi, Makamu Mwenyekiti wa IPI, Khadija Patel kutoka Afrika Kusini aliyeongoza jopo la watu sita kutoka nchi mbalimbali ameelezea hatua walizofikia baada ya kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali na Bunge, jambo ambalo limewaridhisha waandishi hao.

“IPI tumefurahishwa na Serikali ya Tanzania kukubali kufanya majadiliano, kuboresha ubora wa vyombo vya habari. Tumekutana na viongozi kadhaa na tunashukuru walitusikiliza na tumefurahishwa kwa kukubali kwao kuboresha uelewa baina ya Serikali na Wadau wa sekta ya Habari nchini," alisema.

Naye Mkuu wa Akademi ya Chumba cha Habari cha DW kutoka Ujerumani ambaye pia ni mwandhishi mkongwe wa chombo hicho, Carsten von Nahman, alieleza furaha yake kwa Serikali ya Tanzania kufungua mlango wa mjadala kuhusu uboreshaji wa vyombo vya habari na amesema kuwa hatua hiyo ni bora zaidi kwani itawasidia Waandishi pia kuboresha utendaji na kuacha kulalamikiwa na Serikali.

“Tumefurahishwa na mwitikio wa Serikali kuungana na wadau wa sekta ya Habari katika kubadilishana mawazo kwa kuangalia mbele zaidi katika kuijenga sekta hii, lakini katika mikutano tuliofanya na viongozi wa Serikali, kuna madai ya ubora na maadili kwa Waandishi kutozingatiwa hapa nchini kwa hiyo hatua hii ya mjadala itaboresha utendaji kwa Waandishi wa Habari,” alisema.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Wa IPI, Scott Griffen, yeye aliweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania imeonyesha nia ya kufanya mazungumzo kwa nia ya kuboresha sekta hiyo na amesema kuwa ni muda mzuri wa vyombo vya Habari kujiweka katika nafasi nzuri ya utendaji kazi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, TEF, Deodatus Balile amewaasa wanahabari kutekeleza kazi zao kwa ubora na maadili ili kuonyesha weledi katika tasnia hiyo.

“Ukiwa Tanzania ujumbe huu wa IPI umekutana na Mhe Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, Waziri wa Habari, Msemaji Mkuu wa Serikali na baadhi ya wabunge na hawa wala hawakuambiana kuwa tunakwenda kuwaona lakini wote wamelalamikia kiwango cha uandishi wa habari nchini kuwa chini.Sisi wanahabari tunapaswa kufanyakazi zaidi kuboresha kiwango chetu," alisema Balile.

Aidha Mwenyekiti huyo wa TEF amewataka waandishi kuwa na weledi ili siku moja Tanzania iwe na vyombo vya habari ambavyo vikifanya kazi havilalamikiwi wala vyenyewe havilalamiki, na alisema kuwa IPI iko tayari kuwasaidia wanahabari katika kuongeza kiwango cha elimu katika mafunzo mbalimbali na kubadilishana uzoefu ndani na nje ya nchi.


Sent from my iPhone using JamiiForums
 
Back
Top Bottom