Wahariri kuandamana leo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wahariri kuandamana leo

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Oct 28, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Oct 28, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,802
  Likes Received: 83,174
  Trophy Points: 280
  Wahariri kuandamana leo

  na Mwandishi Wetu
  Tanzania Daima~Sauti ya Watu

  WAHARIRI wa vyombo mbalimbali nchini, leo wanatarajia kufanya maandamano ya amani yenye lengo la kupinga uamuzi wa serikali wa kulifungia kwa muda wa miezi mitatu gazeti la kila wiki la MwanaHALISI.

  Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, inaeleza kwamba, tayari maandalizi kwa ajili ya maandamano hayo ya kimya kimya yamekamilika.

  Akizungumza na gazeti hili jana, Kibanda alisema maandamano hayo yataanzia katika Mtaa wa Lugoda zilipo ofisi za magazeti ya Majira, Dar Leo, Business Times na Spoti Starehe saa 4:00 asubuhi.

  Alisema maandamano hayo ambayo tayari yameshapata baraka za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, yatapita katika barabara za Sokoine, Azikiwe, Samora na kumalizikia nje ya jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ambako wahariri watakabidhi tamko lao la kupinga uamuzi huo wa serikali uliotangazwa hivi karibuni.

  “Tumeandaa maandamano ya amani na tunaamini wadau wote wa habari wakiwamo wahariri, waandishi wa habari, wasomaji wa magazeti, watetezi wa haki za binadamu na makundi mbalimbali ya kijamii yataungana nasi katika maandamano hayo,” alisema Kibanda.

  Alisema wakati wa maandamano hayo waandamaji wote watakuwa wamefungwa plasta au vitambaa midomoni kama kielelezo cha kupinga hatua ya serikali ya kujaribu kuzuia uhuru wa vyombo vya habari.

  “Kimsingi lengo la maandamano yetu si kuitetea habari iliyoandikwa na MwanaHALISI, la hasha. Tunachopinga sisi ni hatua ya kulifungia gazeti hilo kwa muda wa miezi mitatu, kwani tunaamini kulikuwa na njia nyingi mbadala zaidi ya adhabu hiyo, ambayo tunaamini inaingilia haki ya watu kuhabarishwa,” alisema Kibanda.

  Uamuzi wa kuandaa maandamano ya kupinga hatua hiyo ya serikali, ulifikiwa wiki mbili zilizopita wakati wa mkutano wa pamoja wa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliokutana kujadili uamuzi huo wa serikali.

  Tayari Jukwaa la Wahariri limewasiliana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania kupinga hatua hiyo ya serikali ya kutumia sheria ya magazeti ya mwaka 1976, inayolalamikiwa kwa muda mrefu na wadau wa habari, inayompa mamlaka waziri mwenye dhamana na masuala ya habari kulifungia gazeti.
   
Loading...