Wahanga wa 'Plea Bargain' waomba Jaji Biswalo asimamishwe kupisha uchunguzi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,117
Ni baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuthibitisha kuwa ofisi yake imeanza uchunguzi wa jambo hilo na ripoti yake itatoka March 2023.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ofisi ya CAG imeanza kuwahoji waathirika wa utaratibu huo kuanzia ngazi ya Kata, huku kukiwa na madai baadhi ya Fedha na Mali zilizochukuliwa kutofikishwa Serikalini.

Mwandishi Eric Kabendera na Wakili Peter Madeleka wametaja kuwepo ufisadi katika mpango huo na kuhamasisha waliolazimishwa kutoa fedha ili kuachiwa huru wajitokeze kutoa ushahidi dhidi ya wahusika.

=======================

Wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akiendelea na uchunguzi wa fedha zilizopo katika akaunti ya ‘Plea Bargaining’, baadhi ya watu walioguswa na utaratibu huo wa mashitaka, wametoa malalamiko ikiwamo kuvunjiwa haki zao za kibinadamu.

CAG Kichere amenukuliwa na kituo cha televisheni cha Azam hivi karibuni akisema kufikia Machi mwakani, ofisi yake itamkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan ripoti ya uchunguzi wa bakaa ya fedha zaidi ya Sh51 bilioni zilizolipwa na kutaifishwa kupitia utaratibu wa ‘Plea Bargaining.’

Kulingana na taarifa hiyo, CAG alisema kwa sasa kinachoendelea ni maofisa wake kuwahoji watu wa kada mbalimbali waliotajwa kuhusishwa na sakata hilo kuanzia ngazi ya kata, huku kukiwa na madai baadhi ya fedha hizo hazikuingia serikalini.

Hata hivyo, baadhi ya mawakili na ndugu wa washitakiwa walioachiwa huru kupitia utaratibu huo, wanataka uchunguzi ufanyike kwa maofisa wa Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP) na wale wa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) mikoani, walioshiriki katika utaratibu huo.

“Kuna maofisa kwenye hizo ofisi tunawafahamu wameneemeka na Plea Bargaining. Yaani kile kiwango walichokuwa wanakubaliana kilipwe kwenye akaunti ya DPP hakifikiwi bure bure. Kunakuwa na pesa ya pembeni,” ilidaiwa.

“Baadhi ya hao maofisa wamekuwa na mali ghafla tu. Wako wamenunua viwanja, wako wamejenga majumba na wako walionunua mali nyingine, lakini ukifuatilia unakuta ni hizo rushwa za plea bargaining,” kilidai chanzo chetu kimoja.

Alipoulizwa kuzungumzia tuhuma dhidi ya ofisi yake, Mkurugenzi wa Mashtaka, Sylivester Mwakitalu hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa kile alichosema suala hilo lipo chini ya uchunguzi wa CAG.

“Si vema kuzungumzia jambo lolote kuhusiana na suala hilo, wakati CAG hajakamilisha uchunguzi wake na kutoa ripoti yake,” alisema.

Alipotafutwa kwa simu azungumzie tuhuma hizo, aliyekuwa na wadhifa huo kipindi hicho ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Biswalo Mganga simu yake haikupatikana.

Waathirika waibua tuhuma

Juzi saa 6:38 mchana, kupitia ukurasa wake wa twitter, mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera ambaye ni mmoja wa waathirika, aliibua tuhuma za ufisadi katika mpango wa watuhumiwa kukubaliana na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kukiri makosa.

Alienda mbali zaidi na kuwahamasisha waathirika waliolazimishwa kutoa fedha ili plea bargaining zao zikubalike, wajitokeze kutoa ushahidi dhidi ya wahusika.

Mwandishi huyo hakuishia kuhamasisha kundi hilo kujitokeza, lakini amewataka wafanyabiashara aliodai walitekwa na kupelekwa ofisi za Serikali na kushurutishwa kwa mtutu wa bunduki kutoa fedha, nao wajitokeze kutoa ushahidi dhidi ya wahusika.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter Oktoba 13, 2022 saa 6:38 mchana, Kabendera aliandika: “Wale mliouza mali zenu kupata pesa za kuhonga kusaidia plea bargaining zenu zikubaliwe mjitokeze kutoa ushahidi.

“Wafanyabiashara mliopelekwa ofisi maarufu ya Serikali (hakuitaja ni ya idara gani na iko wapi), mkatishwa kwa mitutu ya bunduki... mkalazimishwa kutoa pesa mjitokeze.”

Aliongeza kuandika: “Si mara ya kwanza zoezi kama hili kufanyika (la kuchunguza). Rais Mwinyi (Ali) aliunda tume ya kupitia upya kesi zote za uhujumu uchumi alizoziendesha Sokoine baada ya kuingia madarakani na kuna watu walirudishiwa mali zao,”

Kabendera aliachiwa huru Februari 22, 2020 baada ya kuingia makubaliano na DPP kukiri makosa ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilimwamuru kulipa Sh273 milioni kwa makosa ya kukwepa kodi na utakatishaji fedha.

Kabendera alifikishwa katika Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Agosti 5, 2019 kwa mashtaka matatu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustino Rwezile.

Mashtaka hayo ni kupanga na kushiriki mtandao wa uhalifu, kukwepa kodi zaidi ya Sh173 milioni na utakatishaji fedha zaidi ya Sh173 milioni.

Kauli ya Kabendera ambaye ameitoa kupitia ukurasa wake wa Twitter juzi, inaungwa mkono na Tito Magoti, mwathirika mwingine wa utaratibu huo.

Kulingana na Magoti, kuna kila sababu ya waathirika kutoa ushirikiano katika maofisa hao wanaofanya uchunguzi iwapo wataitwa au kufikiwa.

Alisema kilichofanyika haikuwa Plea Bargaining, badala yake ni mbinu ya ukusanyaji wa fedha.

“Kuna mazingira yalitiliwa shaka, haikuwa Plea Bargaining kwa kuwa ilikosa misingi yake,” alieleza Magoti, ambaye kwa sasa yupo nje ya nchi.

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu, alitaja misingi ya Plea Bargaining ni mtuhumiwa kuruhusiwa kujitafakari kisha akiri mwenyewe kosa lake, aandike barua kwenda kwa DPP kisha wajadiliane.

Lakini, kilichofanyika wakati wao alidai ilikuwa kinyume chake, kwani ni kama walilazimishwa wafanye hivyo na zaidi hakukuwa na majadiliano kama inavyohitajika kwa mujibu wa misingi ya Plea Bargaining.

“Sidhani kama kuna wakili au ndugu wa mtuhumiwa aliyewahi kukaa meza moja na DPP kujadiliana, badala yake tulikuwa tunalazimishwa kuandika hizo barua,” alidai.

Magoti ofisa aliyehudumu katika ofisi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mwenzake Theodory Giyan ni waathirika wengine wa makubaliano na DPP.

Wawili hao walikamatwa Desemba 2019 na baada ya kukiri makosa yao walitakiwa kulipa Sh17 milioni, kisha waliachiwa huru Januari 2021.

Barua kwa Rais Samia

Wakati CAG akiendelea na uchunguzi wake, Peter Madeleka ambaye ni mwathirika mwingine wa utaratibu wa Plea Bargaining amemuandikia barua Rais Samia kumtaka atengue uteuzi wa Jaji Biswalo Mganga.

Biswalo aliteuliwa kuwa Jaji Februari 15, mwaka jana baada ya kuhudumu nafasi ya DPP kwa miaka sita na miezi minne alipoteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete Oktoba 16, 2014.

Katika barua yake hiyo kwa Rais Samia, Madeleka alisema kwa kuwa anayelalamikiwa kwenye utaratibu huo ni Biswalo Mganga, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi anapaswa kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.

Katika barua hiyo ambayo gazeti hili limeona ya Oktoba 12, 2022 inasema: “Kwa heshima na taadhima kubwa, nakuomba (Rais Samia) utumie utaratibu wa Jumuiya ya Madola na sheria za Tanzania, umsimamishe kazi Mheshimiwa Jaji Biswalo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.”

Kulingana na barua hiyo, Madeleka aliandika kufanya hivyo kutalinda heshima ya mahakama ambayo Biswalo ni mmoja wa watoa haki.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 110A(2) na (3) (a) (b) na (c) Rais ana mamlaka ya kumsimamisha kazi jaji na kuunda tume ya kumchunguza kwa tuhuma za utovu wa maadili.

Kadhalika, Ibara ya 110A (4) ya Katiba ya Tanzania, utumishi wa jaji utakoma pale atakapokutwa na hatia baada ya kuchunguzwa. Hata hivyo, alipotafutwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus kuhusu barua ya Madeleka kama imefikia kwenye taasisi hiyo, alijibu ni vigumu kujua, kwa sababu barua nyingi zinafika hapo, huku akiomba atumiwe nakala ya barua hiyo.

Kuhusu Plea bargaining


Mbali na malalamiko ya waathirika kuhusu Plea Bargaining, Wakili Kiongozi katika kampuni ya Haki Kwanza, Aloyce Komba alisema utaratibu huo hautekelezwi ipasavyo hapa nchini.

Alibainisha kuwa utaratibu huo umerithiwa kutoka Marekani na unahusisha makubaliano baina ya mtuhumiwa na mahakama.

“Utaratibu huo sio kwa kesi iliyofika mahakamani tu, hata mtuhumiwa anapokamatwa mnaweza kuzungumza kwamba kulingana na kesi yako, tunaomba utusaidie kuwapata wengine wewe tutakupunguzia adhabu sio kutaka kukusanya hela tu,” alisema.

Kwa mtuhumiwa ambaye tayari ameshitakiwa, alisema inaangaliwa thamani ya kosa kisha anakiri kwa kuandika barua kwa DPP wanajadiliana na kuamua.

Hata hivyo, alisisitiza Plea Bargaining ni makubaliano ya pande mbili na mtuhumiwa hapaswi kutozwa fedha yote ambayo angepaswa kulipa baada ya kesi yake kukamilika.

Wakili huyo aliongeza utekelezwaji wa utaratibu huo, uliwahi kupingwa na mawakili nchini, baada ya kutakiwa kutoshiriki kikao cha Plea bargaining akitakiwa mshitakiwa pekee.

“Kwa nini wakili wa pande zote wasiruhusiwe maana yake wanataka kumkandamiza mtuhumiwa hili tulikataa,” alisema.

Waathirika wengine

Utekelezaji wa sheria hiyo, uliwahusisha watu mbalimbali kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Harbinder Seth. Naye ni miongoni mwa walioingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hivyo alihukumiwa kulipa faini ya Sh26.9 bilioni baada ya kukutwa na hatia ya kujipatia Sh309 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Hukumu hiyo ilitolewa Juni 16, mwaka jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi ambapo pamoja na faini hiyo pia alimhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa sharti la kutojihusisha na kosa lolote.

Katika kesi ya msingi, Seth anadaiwa kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 24, 2014 katika benki ya Stanbic na benki ya Mkombozi iliyopo Wilaya ya Ilala na mwenzake James Rugemalira walijipatia Sh309 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Waathirika wengine wa hilo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ushauri wa Uwekezaji na Upatikanaji wa Fedha, Harry Kitilya na wenzake wanne waliokiri na kuamriwa kulipa Sh1.5 bilioni.

Mbali na hao, pia yupo Deogratius Mwanyika aliyekuwa Makamu wa Rais wa mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Mwanyika na wenzake sita walifunguliwa mashitakiwa 39, yakiwemo ya utakatishaji fedha na kukwepa kodi katika kesi ya uhujumu uchumi namba 77/2018. Juni 17, 2020 Mwanyika aliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wenzake wawili, baada ya kukubali kulipa fidia ya Sh1.5 bilioni kila mmoja.

Mkurugenzi wa kampuni ya Mr Kuku Farmer Ltd, Tariq Machibya maarufu Mr Kuku ni mwathirika mwingine wa utaratibu wa Plea Bargaining. Mr Kuku alihukumiwa kulipa fidia ya zaidi ya Sh5.4 bilioni, Desemba 16, 2020 baada ya kukiri mashitaka ya kushiriki katika upatu na kupokea miamala ya fedha kutoka kwa umma.

Katika hukumu hiyo mahakama iliagiza Sh5.4 bilioni ambazo zipo katika akaunti za mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali, ikitaka kiwango hicho cha fedha kuhamishiwa katika akaunti namba 9921169817 iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa jina la mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP).

Machibya alifikishwa mahakamani hapo Agosti 2020 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 60/2020 yenye mashtaka saba likiwemo la kufanya biashara haramu ya upatu na kukusanya fedha za umma Sh17 bilioni. Wengine ni Ndama Hussein na Mkemia Yusuph waliohukumiwa kulipa faini ya Sh145.8 milioni baada ya kuandika barua ya kukiri kosa na kisha kuingia makubaliano na Mkurugenzi ya Mashtaka nchini( DPP).

Aliyekuwa Mbunge wa Kishapu mkoani Shinyanga, Suleiman Nchambi (CCM) naye alihukumiwa kulipa Sh22.5 milioni baada ya makubaliano na DPP kutokana na mashitaka tisa, likiwemo la uhujumu uchumi yaliyokuwa yanamkabili. Katika kesi hiyo Nchambi alishitakiwa na wenzake wawili, ambao ni Yahya Soud aliyeshitakiwa kwa makosa manne na Abdalla Soud aliyekutwa na makosa mawili.

Mohamed Yusufali naye alikumbwa na kikombe hicho, baada ya kukutwa na hatia ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh27 bilioni kwa kukwepa kodi. Yusufali aliwahi kutajwa na hayati John Magufuli kuwa alikuwa anaiibia Serikali Sh7 bilioni kwa dakika kupitia mashine za kodi za kielektroniki (EFD).

Mfanyabiashara huyo aliachiwa huru Oktoba 16, 2019.

MWANANCHI
 
Hili lilitegemewa fdha zile kuliwa na yale maharamia!
Sabaya hapa hakwepi kabisa, na wale waliokuwa ma RC wa Dsm na AR
 
Walipwe tu kama kuna ushahidi. Tusiwachukie wenye hela kwa vile sisi hatuna hela.

Magufuli alitenfa mambo mabaya sana kwa nchi yetu, ndiyo maana Mkono wa Mungu ukamnyakua na kumtupa jehanam
 
Back
Top Bottom