Wagonjwa kutundikiwa dripu kwenye miti inatusikitisha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wagonjwa kutundikiwa dripu kwenye miti inatusikitisha

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, May 24, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  May 24, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,495
  Likes Received: 5,725
  Trophy Points: 280
  Wagonjwa kutundikiwa dripu kwenye miti inatusikitisha

  Na PDIDY

  24th May 2009


  Wananchi wanapopigia kelele ufisadi, siyo kwa dhihaka bali ni kutokana na uchungu walio nao wa rasilmali kuibwa na wachache huku wao ambao ni wengi wakiendelea kughubikwa na umasikini unaopelekea hata kufa ovyo kwa maradhi.

  Bado tungali tunatambua kuwa maadui wakubwa wa taifa letu hili ni ujinga, umasikini na maradhi.

  Na ndiyo maana kilio kikubwa cha wananchi kinaegemea zaidi katika maeneo hayo hasa maradhi ambayo hupoteza nguvu kazi.

  Serikali ilitangaza kwamba kuanzia Julai mwaka 2007, itaelekeza nguvu zake katika kuhakikisha kwamba kila kijiji kinakuwa na ama zahanati au kituo cha afya kwa ajili ya kuhudumia wakazi wake kwa karibu.

  Hatua hiyo ni kutokana na ukweli kwamba bado wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini wanatembea mwendo mrefu au kusafiri ili kuweza kufikia huduma za afya.

  Lakini pamoja na mkakati huo uliowekwa na serikali, inasikitisha kuona kwamba hata zile zahanati au vituo vya afya vilivyopo, huduma zake haziridhishi au hazitoshelezi mahitaji kwa walengwa.

  Mfano mzuri ni taarifa kutoka zahanati ya Nyarugusu wilayani Geita ambako wagonjwa wanalazimika kulazwa nje na kutundikiwa dripu ambazo hufungwa juu ya miti kutokana na kukosa nafasi wodini.

  Hili linatusikitisha sana.Tena wagonjwa hao wanahudumiwa wakiwa wamelala juu ya mikeka na wala siyo magodoro.

  Je, huku ndiko kuboresha afya tunakozungumzia majukwaani kila kukicha?

  Mganga mkuu wa zahanati hiyo, Dk.Zablon Magwana anakiri hilo ni tatizo, lakini anasema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uhaba wa vyumba vya kulaza wagonjwa.

  Isitoshe hawezi kuacha wagonjwa waondoke wakati wanahitaji kuongezewa maji mwilini ili kuokoa maisha yao.

  Wizara ya Afya izinduke na kuelekeza watendaji wake wafuatilie zahanati na vituo vya afya vilivyopo sehemu mbalimbali nchini ili kuweza kutatua matatizo yaliyopo ambayo wakati mwingine ndiyo yanayochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vifo hasa vya kinamama wajawazito na watoto.

  Tunaelewa kwamba bejeti ya serikali katika sekta ya afya ni kubwa, ikitanguliwa na ile ya elimu na miundombinu.

  Kama hivyo ndivyo, kwanini hazielekezwi zaidi kwenye kuboresha vituo vya afya na zahanati vijijini?

  Hata ile ya Nyarugusu tuliyogusia hapo juu, kwa sasa inafanyiwa ukarabati na mashirika yasiyo ya kiserikali ili iweze kutoa huduma kwa wananchi 50,000 wanaoitegemea hivi sasa.

  Wakati mashirika kama hayo yanasaidia, wizara ya afya nayo isibweteke, ijipange kuhakikisha kuwa kero zinazohusiana na huduma mbovu kwenye vituo vya afya zinatokomezwa.

  Ni matumaini yetu kwamba tukio kama lile la Nyarugusu kwa wagonjwa kulazwa nje na kutundikiwa dripu litazindua watendaji sekta ya afya na kuhakikisha kuwa halijirudii tena sehemu zingine nchini


  Bravo Lukuvi, shupalia pia ulinzi shirikishi

  Tunapenda kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi kwa kukemea tabia ya baadhi ya watendaji wa wilaya na Kata wanaoamuru askari mgambo kukamata ovyo wafanyabiashara ndogo ndogo na pia ufungaji holela wa magari yanayoegeshwa Jijini.

  Wengi wa watendaji hawa na hasa madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa wamekuwa katika nafasi zao kwa lengo la kujinufaisha zaidi badala ya kutumikia wananchi kwa kutatua kero zao.

  Katika ziara zako Mheshimiwa Lukuvi, himiza pia suala la ulinzi shirikishi ambalo wenyeviti wa serikali za mitaa wanapaswa kulivalia njuga kwa lengo la kutokomeza uhalifu sehemu za makazi ya watu.

  Mfano maeneo ya Mbezi Beach hasa eneo la Makonde karibu na Shule ya sekondari ya Essacs, vibaka ni tishio kubwa. Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa ameitwa mara nyingi lakini hataki kuja hivyo kupelekea wakazi wa eneo hilo kupoteza kabisa imani naye.
   
Loading...