Uchaguzi 2020 Wagombea watakiwa kutumia majukwaa yao kukemea na kupinga udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,498
9,279
WANAHARAKATI wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wamewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuwa na ajenda ya kupambana na vitendo hivyo ili kuhakikisha wanawake na watoto wanakuwa salama.

Mwanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia mkoa wa Kaskazini Unguja, Fatma Saleh Ukindu, alisema hiki ni kipindi kizuri kwa wanasiasa kubeba ajenda ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kueleza jinsi watakavyopambana navyo kama wakifanikiwa kushika nafasi za uongozi.

“Kwa mfano wagombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar wanatakiwa kubeba ajenda hiyo katika kipindi hiki wakati wakiomba kura kwa wananchi na jinsi watakavyopambana navyo kama wakichaguliwa kuongoza Zanzibar,” alisema.

Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Uwezeshaji Wanawake, Watoto na Wazee, Zuwena Hamad Omar, alisema njia nzuri ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji kwa jamii ni wananchi kutoa taarifa mbele ya vyombo vya sheria na kuacha kuficha wahusika wa matukio hayo.

‘’Vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vitaondoka kama jamii yetu itaachana na usiri na kutoa taarifa mbele ya vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa,’ ‘alisema.

Khamis Othman kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), aliitaka jamii kuongeza ushirikiano katika kupambana na vitendo hivyo, ikiwamo kutoa ushahidi kwa Jeshi la Polisi ili kesi ziweze kupelekwa mahakamani.

‘’Kesi nyingi zinaletwa ofisini kwetu kwa ajili ya kuzipeleka mahakamani lakini ukiziangalia yapo mapungufu mengi ambayo yamekuwa kikwazo kwa kesi hizo kufikishwa mahakamani,’’ alisema.

Awali, Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mohamed Amour Haji, alisema tabia ya jamii kukataa kutoa ushahidi mbele ya Mahakama ni kati ya sababu ya kesi hizo kufutwa na kuibua malalamiko kutoka kwa jamii.

“Ili kesi iwe tayari kusikilizwa, ushahidi wa pande zote unahitajika ambao ndiyo utakaofanya mwenendo wa kesi kutajwa mahakamani.”
 
Back
Top Bottom