Naona wameamua la maana.
Wagombea mwakani kubanwa kitaaluma
Baraza la Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) limepitisha uamuzi wa kuishirikisha Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kuhakiki vyeti vya wote wanaoomba kuwania nafasi za kisiasa ili sifa zao kielimu zitambulike.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Mayunga Nkunya, aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam, TCU imewasiliana na NEC kwa barua, ili utaratibu huo uanze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.
Nkunya alitoa taarifa hiyo wakati akizungumzia maonyesho ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na TCU yatakayoanza kesho hadi Aprili 24, mwaka huu. Baraza letu limepitisha uamuzi ili watu wanaotaka kugombea nafasi za kisiasa, vyeti vyao vihakikiwe, ili akipita sifa ijulikane rasmi kama ni daktari basi awe daktari na si daktari feki, alisema Profesa Nkunya.
Hatua hiyo ya tume inatokana na kilichoelezwa na Nkunya kuwa ni kukithiri kwa vyuo na vyeti bandia nchini, jambo ambalo alisema wamejipanga kulivalia njuga kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha Tanzania haiangamii kitaalamu na kitaaluma.
Alisema orodha ya vyuo visivyotambulika vya nje ambavyo Watanzania wengi wakiwamo mawaziri na wabunge wamesoma, ni ya kweli na kwamba kama kuna mtu anahisi kuonewa ruhusa kwenda mahakamani.
Sisi TCU tumepewa jukumu na taifa hili, kuhakikisha elimu inayotolewa kwa Mtanzania inatambulika duniani kote na inatolewa na vyuo vinavyotambulika, tulitoa orodha ya vyuo feki sasa kama kuna mtu anapinga aende mahakamani, alisema Profesa Nkunya wakati akijibu swali juu ya ukweli wa orodha ya vyuo feki iliyotolewa na tume hiyo hivi karibuni.
Akizungumzia tatizo la kughushi vyeti, alisema linazidi kukua, hali ambayo inatishia sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na uwezekano wa Tanzania kuzalisha wataalamu feki. Tatizo la kughushi vyeti linazidi kuwa kubwa nchini hali ambayo ni hatari na haipaswi kufumbiwa macho, si siri tatizo hili lisipodhibitiwa nchi itaenda pabaya, tushirikiane tulidhibiti, alisema.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji huyo wa TCU, katika udahili wa mwaka 2008/09 pekee, tume hiyo ilipelekewa majina ya wanafunzi zaidi ya 200 ambao vyeti vyao vinasadikiwa kughushiwa. Hii ni hatari, tusaidiane kukabiliana na tatizo hili, tukiacha liendelee nchi yetu itakwenda pabaya na hatari yake ni kuzalisha wataalamu feki, alisema Nkunya.
Alisema kwa sasa watu wanaoongoza kwa kupeleka vyeti vya kughushi vyuoni ni waliosoma miaka ya nyuma, hali inayoonyesha ni upungufu wa nidhamu ambao inabidi uchukuliwe hatua. Alitoa mfano wa Liberia ambayo iliacha tatizo hilo la kughushi na kuwa na vyuo feki likakua na kusema nchi hiyo imefanya elimu yake kutokuwa ya kuaminika.
Kwa sasa hali ya Liberia kielimu ni mbaya, waziri anaweza kuanzisha chuo chake na kujipa shahada, hiyo elimu gani? Alihoji. Profesa Nkunya aliitaka jamii isiliache tatizo hilo mikononi mwa TCU na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) pekee, bali liwe mikononi mwa kila mtu vikiwamo vyombo vya Dola, katika kupambana nalo.
Sheria ziangaliwe, kwani kukithiri kwake kunatokana na wanaokamatwa kutochukuliwa hatua thabiti za kukomesha tabia hiyo, alisema. Alisema katika kuhakikisha kuwa hadi kwenye ofisi watu wenye vyeti bandia wanadhibitiwa, TCU pia imejipanga kurekebisha sheria yake, ili iwe na uwezo wa kutembelea ofisi moja baada ya nyingine, kuhakiki vyeti vya watu.
Alisema imeshaanza mchakato wa kurekebisha sheria hiyo. Hivi karibuni, NECTA ilitoa taarifa na orodha ya maelfu ya wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya ualimu wanaotarajia kufanya mtihani wao wa mwisho mwezi huo, ambao walibainika kutumia vyeti bandia na kuwataka wawasilishe vithibitisho, vinginevyo hawataruhusiwa kufanya mtihani.
Hata hivyo, kutokana na kukithiri kwa vyeti bandia, serikali imedhamiria kupambana na watumishi waliowasilisha vyeti bandia baada ya idara zote za serikali kutakiwa kuhakikisha zinawasilisha vyeti vya watumishi wake kwa ajili ya uhakiki, mchakato ambao unaendelea hadi sasa, huku baadhi wakiachishwa kazi kutokana na kukutwa na vyeti bandia.