X-PASTER
JF-Expert Member
- Feb 12, 2007
- 11,610
- 1,809
Wafungwa Wa Kitanzania Walia Njaa Kenya
WATANZANIA zaidi ya 66 waliofungwa katika Gereza la Kamiti jijini Nairobi nchini Kenya, wamelalamika kuteswa na kunyimwa chakula, hivyo kuomba Serikali ifanye utaratibu wa kuwarudisha nchini ili kumalizia vifungo vyao.
Katika mazungumzo yao na gazeti hili kutoka Nairobi, wafungwa hao walidai kuwa wapo katika hali mbaya sana kiafya na mateso mengi, ikiwa ni pamoja ya kutokuwa na chakula.
Kenya imetangaza baa la njaa na sisi Watanzania tulioko jela tunanyimwa chakula na kuambiwa kuwa Serikali ya Tanzania imekataa kuuzia mahindi Serikali ya Kenya, walidai wafungwa hao.
Walidai kwamba Balozi wa Tanzania nchini humo (hawakumtaja jina), hafiki kuwasaidia licha ya wapo kupeleka malalamiko yao tangu mwaka 2009 wakati wafungwa wengine kutoka Nigeria, Uganda na Ghana husaidiwa na balozi zao zilizopo nchini humo.
Tumepeleka taarifa za malalamiko yetu kwa balozi wetu tangu mwaka 2009, lakini hakufika kutusaidia na hatujui iwapo kahamishwa au katudharau, walilalamika wafungwa hao ambao hawakutaja makosa yaliyosababisha watupwe jela.
Walidai kuwa katika gereza hilo la Kamiti, wako wafungwa 66, na wengine wako katika magereza ya Naivasha na Kisumu.
Walidai kwa sasa kuna wafungwa wengi Watanzania ambao ni wagonjwa na baadhi wanatakiwa wakafanyiwe upasuaji, lakini wanaambiwa magereza ya Kenya hayana fedha, hivyo wasubiri ndugu zao watoe fedha ndipo wafanyiwe upasuaji wakati hawana ndugu humo.
Aidha, walidai wako Watanzania wanaokufa kwa kukosa huduma za matibabu kutokana na kubaguliwa hivyo wanaomba Serikali kuwarudisha nchini wamalizie vifungo vyao.
Tunaomba Mheshimiwa Jakaya Kikwete atusaidie kupitia Muungano wa Afrika Mashariki turudishwe Tanzania kwani Watanzania tuliopo magereza ya Kenya tunanyanyasika sana haki hakuna na tunabaguliwa sana kwani hata sasa kuna Mtanzania mwenzetu amevunjwa mkono na askari na hajapatiwa matibabu yoyote, walidai wafungwa hao.
Chanzo: habarileo