Wafugaji na mbinu mpya za kuwaoza wanafunzi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
40,722
2,000
000001mwanafunzi.jpg
Naomi Meshilieki mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Simanjiro ambaye amebahatika kufika kidato cha nne, huku wenzake watatu waliofaulu kusoma katika shule hiyo wakiwa wameolewa kwa kutumia mbinu mpya zilizobuniwa na wazazi. Picha na Fredy Azzah.​
Fredy Azzah
“KWETU ukiwa na mtoto wa kike tayari unahesabu utajiri, sasa ni mtu gani mjinga utakubali kufa na njaa umwache mtoto akamalize miaka saba shuleni,” anasema Elibariki Kisongo mkazi wa Kirun’gurun’gu.Mzee huyo ana umri wa miaka 70 na anaweka wazi kwamba licha ya kuzaa wasichana 13 na wake zake watano, hakuna hata mmoja aliyesoma.
“We acha ujinga bwana, nikiwasomesha watakuja kunisaidia nini,” anasema mzee huyo.
Anasema anawaozesha watoto baada ya kuwa wakubwa, lakini anakiri kwamba wakati akifanya kazi hiyo anakuwa hajui umri wa watoto wake.
Kwa upande wake Martha Okida (50), mkazi wa Orkesument, anasema ili mtoto wa kike asome katika jamii ya kimasai, mzazi anapaswa kuwa na akili ya ziada.
“Siku hizi baada ya kujua kuwa kumuozesha mtoto wa shule ni vibaya, wanawapeleka kwa mume wakiwa na miaka sita mpaka nane,” anasema mama huyo.

Anasema kuna matukio mawili ya watoto wenye miaka nane walikuwa wameozwa kwa wazee wenye zaidi ya miaka 65, ambao hata hivyo waliwahi kuokolewa na watu wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Nafgem na kwenda kuwasomesha mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.


Anasema wanafunzi ambao wanataka kuolewa wanabeba mimba wakiwa shuleni ili wafukuzwe shule na wakati mwingine wazazi wao wanawaambia wafanye vibaya shuleni.

“Ili mtoto wangu asiole, ilibidi niende shuleni nizungumze na walimu waje wamchukue, lakini nikamwambia mwalimu akifika nyumbani

nitamkana kwamba simfahamu ili baba asinipige, Mungu akasaidia watoto wangu wakasoma,” anasema mama huyo.

Kauli ya mama huyo inaungwa mkono na Elibariki Morani anayesema tabia ya kuwaozesha watoto wenye umri chini ya miaka 10, imeshika kasi katika eneo hilo.

“Hawa watoto hawaendi moja kwa moja kwa mume bali utakuta tayari mzee amechukua mahari na mtoto atapelekwa kulelewa na mama wa kijana aliyetoa mahari ili akiwa mkubwa aanze kuishi na mume wake kama mke,” anasema kijana huyo.

Hoja za wazazi hao zinazua mjadala kwa kuwa kauli za watoa taarifa hazikufafanua ni vipi wanaweza kutambua kwamba mtoto amekua na sasa anaweza kuishi na mume.

Wakati morani akisema ni mtoto kutoka mazima, Jacobo Lemburis anasema mtoto anaruhusiwa kulala na mwanaume baada ya kinamama ambao wanawalea kujiridhisha kwamba anaweza kulala na mwanaume bila kujali ana miaka mingapi.

“Huku kwetu wanafunzi wanaoachishwa masomo ili waolewe ni wachache kwa sababu wengi hawapati hata hiyo nafasi ya kuingia darasa la kwanza,” anasema Lemburisi.

Lemburis pamoja na Martha, wanasema moja ya sababu inayochangia hali hiyo ni wazazi kuwa na tamaa ya kupata mahari.

“Wanajua kabisa kuwa ni kosa kuozesha watoto, lakini wana tamaa ya mali,” anasema Lemburisi.
Kwa upande wake Martha, anasema wanasiasa wamekuwa hawakemei ipasavyo vitendo hivyo kwa kuhofia kupoteza nafasi zao.

Mrakibu wa Polisi Simanjiro (ASP) Felix Kikwale anasema matukio machache yanaripotiwa polisi na kwamba tangu mwaka huu uanze ni tukio moja tu limeripotiwa.

“Siyo kwamba haya matukio hayapo, tunajua ni mengi sana, lakini watu hawaripoti polisi kwa kutojua sheria ama kwa tabia zao tu za usiri na kuogopa laana,” anasema Kikwale.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lalumorijoi Jeremia Lemandi, anasema katika kata yake, vitendo hivyo hakuna kabisa.

Pia Diwani wa Kata ya Langai, Jackson Lesikari anasema suala hilo lipo kwa kiasi kidogo na kwamba hana takwimu, huku akisema linasababishwa na watu kutokuwa na elimu.

“Wazazi wengi hawajui kwamba kumuozesha mtoto chini ya miaka 18 ni kosa, lakini kuna mashirika mbalimbali kwa kushirikiana na serikali yamekuwa yakitoa elimu kupinga vitendo hivyo,” anasema Diwani huyo.

Naye Diwani wa Orkesument, Naftal Samuel anasema: “Wananchi wangu wengi wameelimika, siyo rahisi ukute wakiozesha watoto.”
Mkuu wa Shule ya Sekondari Orkesument Jacobo Khahima inayohudumia wanafunzi kutoka Kata za Orukasument, Endonyongijape na

Langai, anasema hana ushahidi wa kutosha kuhusu suala hilo, ingawa kuna baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiacha shule na wengine kupata ujauzito.


“Hatuwezi kusema kuwa wanaolewa moja kwa moja, lakini wapo ambao wanaacha shule na wengine baada ya kupata mimba, yote haya yanaweza kuambatana na suala la kuolewa,” anasema mwalimu huyo.

Anasema tangu Januari mpaka sasa tayari wamepata wanafunzi wawili wajawazito, mmoja alipaswa awe kidato cha tatu sasa na mwingine kidato cha kwanza.

“Huyu wa kidato cha kwanza alikuja na mimba kutoka shule ya msingi,” anasema Khahima.

Pia anasema mpaka sasa wanafunzi sita wa kidato cha kwanza hawajaripoti shuleni, huku akifafanua kuwa watoto wengi wamekuwa wakienda likizo na kutorudi shuleni.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, Joyce Michael anasema wanafunzi wengi wamekuwa wakipewa mimba na matokeo yake kuacha shule.


“Wapo wengi tunaosoma nao, lakini wameolewa, wakirudi likizo wanaenda kuishi kwa waume zao na wakipata mimba wanaacha shule, lakini mara nyingi hawa hawajui umuhimu wa kusoma kwa sababu wanajua tayari wana wanaume,” anasema Michael.

Naye Naomi Meshilieki mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo anasema katika Kata ya Nangai anapotoka, suala la wanafunzi kuachishwa shule na kuolewa siyo jambo la ajabu.

“Tulipomaliza shule tulikuwa wanafunzi sita tuliofaulu, wenzangu wawili waliolewa na wengine waliacha shule wenyewe na sasa watatu tu tunaendelea na masomo,” anasema Meshilieki.

Mtendaji wa Kata ya Endonyongijabe, Mary Chisoji anasema suala la watoto kuachishwa shule katika kata yake ni kubwa.

Anasema tatizo hilo ni kubwa katika kata yake ambayo ina shule moja tu ya Msingi ya Orkirungrung. Anasema kutokana na tatizo hilo matokeo ya shule hiyo yamekuwa mabaya.


Kauli hiyo inaungwa mkono pia na Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Wilaya hiyo Jackson Mbise, anasema wanafunzi wamekuwa wakiachishwa kwa sura mbalimbali.

Anasema moja ya njia hizo ni pamoja na wanafunzi kubeba mimba kwa makusudi ili wafukuzwe shule na nyingine ni utoro.
“Unaweza kukuta kati ya wanafunzi 194 wanaoanza shule, wanaomaliza ni wanafunzi kati ya 40, 70 au 100, wengine wanatoweka kwa njia kama hizi, wengi wanaocha shule ni wasichana, pia wanaume wanaacha shule na kwenda kuchunga, lakini ni wachache,” Ng’ombe.

Mbise anasema njia nyingine ni mzazi kuhama kabisa katika Kijiji kwa kisingizo kwamba wanakwenda kutafuta malisho ya mifugo, lakini ukweli ni kwamba wanaenda kuwaozesha watoto.

Katika Shule za sekondari hali ni mbaya zaidi na kusababisha Ofisa Elimu Sekondari katika wilaya hiyo Julius Mduma kusema kwamba kila kukicha wanaumiza vichwa ili kuzuia tatizo hilo.

Anasema katika wilaya hiyo kuna shule 14 za sekondari na wanafunzi 1,976, kati yao wasichana ni 934 na wavulana ni 1,042 ambao wamepangwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu. Walioripoti shuleni mpaka Aprili 16, mwaka huu ni 1,283, wasichana wakiwa 606 na wavulana 677.


“Kwa hiyo mpaka sasa wanafunzi 491, wasichana wakiwa 272 na wavulana 219 hawajafika shuleni mpaka sasa, Wilaya tumekuwa tukitoa gari kila mara ili tukawatafute katika maeneo ya vijijini bila mafanikio,” anasema Ofisa huyo.

Anasema mbali ya wanafunzi hao kukwepa kuanza kidato cha kwanza, pia ambao wanaanza kidato cha kwanza, zaidi ya nusu ya wanafunzi wamekuwa hawahitimu kidato cha nne.

Takwimu za Wilaya hiyo zinaonyesha kuwa, kati ya wanafunzi 157 walionza kidato cha kwanza mwaka 2004, wavulana wakiwa 70 na wasichana 87, waliohitimu kidato cha nne mwaka 2007 walikuwa 47 tu, wavulana wakiwa 30 na wasichana 17.

Pia mwaka 2005 wanafunzi walioanza kidato cha kwanza walikuwa 334, wavulana 185 na wasichana 149, na waliohitimu kidato cha nne mwaka 2008 walikuwa 154, wavulana 94 na wasichana 60.

Mwaka 2006, wanafunzi 400 walianza kidato cha kwanza, wavulana wakiwa 200 na wasichana 200, lakini waliohitimu mwaka 2009 walikuwa 350, wavulana wakiwa 195 na wasichana 155.

Mwaka 2007, wanafunzi 754 walianza kidato cha kwanza, wavulana walikuwa 361 na wasichana 393 na walioitimu mwaka 2010 walikuwa 622, wavulana 340 na wasichana 282.

Katika mwaka 2008 wanafunzi walioanza kidato cha kwanza walikuwa 1,431 na kati yao wavulana walikuwa 720 na wasichana 711,

waliohitimu kidato cha nne mwaka 2011 walikuwa 763, wavulana 400 na wasichana 363.

“Hilo ndiyo tatizo kubwa la huku, na kwa kweli ukiangalia wasichana wengi wanaoacha shule, tatizo kubwa ni mimba na kuolewa,” anasema Ofisa huyo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa kushirikiana na Tamwa, umebaini kuwa sababu kubwa inayochangia mimba kwa wanafunzini ngoma maarufu kama Esoto ambazo huchezwa usiku kucha na morani pamoja na wasichana.


Baada ya ngoma wanaume na wasichana hufanya ngono kwa kile kinachoitwa ni kuwafundisha wasichana hao ambao ni wachumba wao.

Mtendaji wa Kata ya Endonyongijape Mary Chisoji, anasema baada ya ngoma kuchezwa wasicha wanaoshiriki huwa wameshakeketwa na wapo tayari kwa kuolewa, hufanya ngono na Morani na tayari wanakuwa wamelipiwa mahari.
Morani Saitoti (38), Mkazi wa Orkujit anakiri kuwapo kwa ngoma hizo na kusema vitendo hivyo vinafanyika, lakini anasema haoni tatizo

kwa kuwa wasichana hao ni wachumba wa watu.

“Sasa kuna ubaya gani kama utatoka na msichana wako ambaye umeshamtolea mahari,” anahoji Saoitoti.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Simanjiro Steve Mibeyazo, anasema kesi za watoto kuachishwa shule zimekuwa zikifikishwa katika mahakama hiyo na maofisa watendaji wa kata na zimekuwa zikitolewa uamuzi.
Hata hivyo anasema sheria iliyopo sasa ina changamoto kwa sababu haisemi kama msichana anayepewa mimba, anatakiwa achukuliwe hatua gani.

Anasema kutokana na udhaifu huo amekuwa akitumia uzoefu wake katika kutoa adhabu kwa washtakiwa.
Mwisho
Wafugaji na mbinu mpya za kuwaoza wanafunzi
 

Kimbori

JF-Expert Member
Feb 21, 2012
4,604
2,000
Hiyo ndiyo hali halisi, jamii za wafugaji zinaangamia. Watoto husafirishwa hata mikoa ya mbali kama DSM, ambako wanaandaliwa ili waolewe.
SULUHU: KILA MZALENDO AJITAHIDI KUTOA TAARIFA SERIKALI ZA MITAA, POLISI N.K ANAPOONA HALI KAMA HIYO. La sivyo, mabadiliko yatachelewa sanaa....
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom