Wafuasi Chadema walipuliwa mabomu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wafuasi Chadema walipuliwa mabomu

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MziziMkavu, Oct 21, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Oct 21, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  Frederick Katulanda na Mussa Mkama, Mwanza
  KAMPENI za Uchaguzi Mkuu ambazo zinaelekea ukingoni zimezidi kuongeza joto la kisiasa nchini, baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kulazimika kutumia mabomu yamachozi kutawanya wafuasi wa Chadema kutokana na kuibuka mvutano kuhusu eneo ambalo mgombea urais wa chama hicho, Dk Willbroad Slaa, angepeswa kuhutubia.

  Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi kulazimika kutumia nguvu hizo, lilitokea saa 6: 39 mchana jana baada ya kushindwa kuelewana kati ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Nyamagana na Ilemela, Willison Kabwe na uongozi wa Chadema Mkoa wa Mwanza, kuhusu wapi mkutano wa Dk Slaa ungefanyika.

  Wakati Chadema wakitaka kufanyia mkutano katika Uwanja wa Furahisha Kirumba kutokana na uwezo wake wa kuchukua watu wengi, lakini msimamizi huyo wa uchaguzi, alitaka wafanyie mkutano wao eneo jingine.

  Mvutano huo, ulisababisha polisi kutumia mabomu hayo kutawanya wafuasi hao, hatua ambayo ilisababisha kujeruhiwa kwa mtu mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja baada ya bomu lililopigwa kumfikia mguuni.

  Kutokana na bomu hilo kupigwa na kutua miguuni, raia huyo alilazimika kubebwa na pikipiki kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza kwa matibabu, huku wananchi wengine wakikimbia na kupoteza viatu vyao.

  Awali askari wa kikosi cha FFU ambao walikuwa katika magari walipiga mabomu matano saa 6:39 na kutawanya wafuasi hao ambao walikuwepo tangu saa nne asubuhi.

  Lakini, mabomu hayo yalionekana kutowatisha wafuasi hao kwani waliendelea kumiminika zaidi hapo ndipo polisi walipolazimika kuwatawanya kwa kupiga mabomu manne saa 9:04 alasiri.

  Mbali ya hali hiyo tete, mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Ilemela, Haines Samson, alikamatwa na polisi mara baada ya mabomu hayo kupigwa kutokana na kile kilichoelezwa ni kukaidi amri halali ya Jeshi ya kuondoka katika eneo hilo akiwa na mfuasi mmoja wa Chadema ambaye jina lake halijafahamika mara moja.

  Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Willison Mshumbusi, alisema chama chake kwa kuzingatia ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), walipaswa kufanyia mikutano ya kampeni
  katika Kata ya Igoma kwa Jimbo la Nyamagana na Furahisha kwa Jimbo la Ilemela, lakini msimamizi aligomea kufanyika Furahisha.

  "Mpaka jana tulikuwa tukijua kuwa mkutano wetu utafanyika Igoma na Furahisha, lakini tulistuka jana (juzi) saa 9:45 baada ya kuwa tumefanya maandalizi Msimamizi wa Uchaguzi kutufahamisha kuwa hajaruhusu mkutano wetu kufanyika Furahisha kwa madai kulikuwa na mkutano wa Injili. Tuliwasiliana na polisi wao walidai hawana tatizo wanafuata maelekezo ya msimamizi," alifafanua Mshumbusi.

  Kabwe alipoulizwa kuhusu utata huo, alisema katika utaratibu wa kampeni hakuna chama ambachokilipangiwa kufanya mkutano wa kampeni kwenye uwanja huo, kwani uliachwa kwa ajili ya shughuli nyingine tofauti na siasa.

  Alifafanua kwamba, tangu kuanza kwa kampeni hakuna mgombea hata mmoja wa chama
  chochote cha siasa ambaye aliruhusiwa kufanya mkutano wake katika uwanja huo na kusisitiza, CUF pia waliombwa na kuzuiwa kufanya mkutano huo na badala yake wakafanyia mkutano wake Uwanja wa Mirongo.

  "Hawa Chadema wanataka kulazimisha mambo, hakuna chama cha siasa ambacho tulikiruhusu kufanyia mkutano hapo, tokea kampeni zinaanza,tuliuacha uwanja huo kuwa huru kwa ajili ya shughuli nyingine, sasa
  naona kama walitaka kufanya mkutano wao hapo kwa nguvu....basi hilo ndilo ninaweza kulieleza," alisema

  Lakini, Mshumbushi akifafanua zaidi, alisema baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kugomea kwa sababu za mkutano wa kidini, walitambua uwanja wa pili ambao walipewa wa Mgomeni, waliamua kuwasiliana na waandaaji wa mkutano huo wa Injili ambao waliwakubalia kufanya mkutano huo kwa vile walikua katika hatua za maandalizi tu na haikuwa siku ya kuanza mkutano wa
  huo wa kiroho.

  "Wanaoandaa mkutano tulipozungumza nao walikubali tufanyie mkutano hapo na kuomba tulinde majukwaa yao, ambayo walikuwa wameanza kujenga. Msimamizi pia alikataa kata na kuwaagiza polisi kutuzuia. Nadhani huu
  ni utumiaji mbaya wa mamlaka na unayatumia kwa maslai ya kuwafurahisha
  chama tawala," alilalamika Mshumbusi.

  Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Simon Sirro, alisema kabla ya jeshi lake kuchukua hatua ya kutawanya wafuasi hao
  ambao walianza kukusanyika mnamo saa 4:00 asubuhi, aliwaita viongozi wa Chadema mkoa na kuwaeleza amepokea barua kutoka kwa mamlaka za uchaguzi zikiwataka watafute uwanja mwingine kwani huo ulikuwa na shughuli nyingine.

  "Baada ya kuzungumza nao, niliambiwa kuna wafuasi wao wamekusanyika uwanjani hapo basi niliamua kwenda huko mnamo saa 4: 20 huko pia niliwakuta baadhi ya viongozi wa chama hicho na kuwasomea barua ya msimamizi wa uchaguzi, nikawaeleza kazi yangu siyo kutoa viwanja bali msimamizi na niliwataka watafute uwanja mwingine. Tukakubaliana na wakatafuta Uwanja wa Magombeni Kirumba, nikaondoka na kuwataka wawaeleze wafuasi wao kuondoka," alifafanua kamanda Sirro.

  Hata hivyo, kamanda huyo alishindwa kueleza ni watu wangapi walijeruhiwa na kusema atatoa taarifa yake rasmi leo.

  Hii ni mara ya pili kwa wafuasi wa Chadema kupima misuli na polisi mkoani Mwanza, awali katika ziara yake ya kwanza ya kampeni mkoani humo polisi pia walilazimika kutumia mabomu kutawanya wafuasi hao waliokuwa wamefunga barabara wakimsindikiza mgombea huyo wa urais hadi uwanjani.

  Chanzo: Gazeti la Mwananchi
   
Loading...