Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu Geita waandamana

Mongoiwe

JF-Expert Member
Feb 26, 2008
524
263
WAFANYAKAZI wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) leo wanameandamana na kumtaka mwajiri wao kukitambua chama cha wafanyakazi wa Migodi, nishati na ujenzi (Tamico) ikiwa ni pamoja na kuunda tume huru ya kuchunguza madai ya wenzao wanaoumia kazini.

Maandamano hayo ambayo yalianzia mtaa wa Shilabela hadi jirani na lango kuu la Mgodi huo, yalipambwa na mabango mbalimbali ya wafanyakazi hao na kupokelewa na Afisa Utumishi wa Mgodi huo Samson Furugensi kwa niaba ya mwajiri.

Akizungumza jana mara baada ya maandamano hayo kupokelewa Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa Migodi, nishati na ujenzi (Tamico) Aloyce Shigela, tawi la mgodi huo alisema kuwa wameandamana kwa lengo na nia ya kumtaka mwajiri wao kukitambua chama chao na kuacha mara moja kutumia chama cha wafanyakazi alichojiundia yeye jambo ambalo ni kinyume na sheria ya ajira na mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004.

"Jambo lingine ambalo tunataka mwajiri wetu alitekeleze ni pamoja na kuacha mara moja kuwafukuza kazi wafanyakazi ambao ni wanachama wao bila ya kutuhusisha Tamico kujadili maslai yao na kusitisha mara moja zoezi la makusudi ambalo mwajiri analifanya la kupunguza wafanyakazi kwa lengo la kukidhohofisha nguvu chama chetu." alieleza.

Alisema leo wamefanya maandamano ya amani kwa lengo la kutaka mwajiri wao kusikiliza kilio chao na kusisitiza kuwa iwapo hata tekeleza madai yao basi watafanya maandamano mengine ambayo yataitikiwa na wafanyakazi wote Afrika wa kampuni ya Anglo Gold.

“Haya ni maandamano ya amani kabisa na tunaandamana kwa lengo la kuutaka uongozi wa Mgodi kuacha kikihujumu chama chetu kwa kuwaondoa wafanyakazi ambao ni wanachama wetu kwenye payroll kinyemela pasipo kufuata na kuzingatia taratibu,” alieleza.

Alisema pia wanamtaka mwajiri wao kuunda tume huru itakayohusisha watalaam wa wakala wa afya na usalama kazini (OSHA), wizara ya kazi na chama chao ili kubaini madai ya wafanyakazi kupata madhara ya matatizo ya migongo wawapo kazini na tukio la kuachishwa kazi kwa wanaoathirika na madhara hayo.

Kwa upande wake mwakilishi wa mwajiri huyo, Samson Fulugensi alisema kuwa amepokea maandamano hayo kwama alivyoagizwa na mwajiri mkuu na kuwashukuru kwa kuandamana kwa amani.

"Nina washukuru mmeandamana kwa amani na mimi nimetumwa na mwajiri kuja kupokea maandamano yenu asanteni sana," alieleza bila ya kufafanua zaidi na hivyo kuhitimisha maandamano hayo.
Source:KATUNEWS.
 
Back
Top Bottom