Wafanyakazi Urafiki waandamana kupinga kufukuzwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,029
Posted Date::10/30/2007
Wafanyakazi Urafiki waandamana kupinga kufukuzwa
Na Furaha Kijingo
Mwananchi

WAFANYAKAZI wa kiwanda cha nguo cha Urafiki jijini Dar es Salaam jana (TFC) waliotimuliwa wameandamana na mabango na kuzuia geti la kutokea nje ya kiwanda hicho, kuushinikiza uongozi wa kiwanda hicho kuwapa haki zao kufuatia kuachishwa kwao kazi.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana wafanyakazi hao walidai kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuachishwa kwazi kufuatia ongezeko la mshahara mpya iliyotangazwa na serikali hivi karibuni ambao uongozi ulidai kuwa hauwezi kuwalipa .

Wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe kwa Rais Jakaya Kikwete na uongozi wa kiwanda hicho walisema wamefukuzwa kiwandani hapo bila mafao yoyote licha kufanya kazi kwenye kiwandani kwa zaidi ya miaka mitano kama vibarua na kulipwa Sh10,000 kwa wiki.

"Tupo hapa kwa muda usiopungua miaka mitano, lakini tumekuwa tukifanya kazi kama vibarua na leo wanatusimamisha kazi bila kutulipa mafao yetu, sasa sisi tutafanya nini," alisema Pita Jastini mmoja wawaandamanaji.

Waliongeza kuwa endapo uongozi wa kiwanda hicho hautafanyia kazi madai yao ya kuwalipa mafao ya watachukua hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungua kesi mahakamani.

Hata hivyo walibainisha kuwa uongozi kiwandani hapo umewaeleza kuwa wanahitajika watu kumi kwaajili ya kuwawakilisha katika kikao ambacho kitafanyika leo saa 4 asubuhi katika ukumbi wa maendeleo kuzungumza na uongozi wa Mkoa wa Chama cha Wafanyakazi (Tuico) .

Akizungumzia suala hilo Meneja Utumishi wa Kiwanda hicho, Mosses Swai alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa hawajawafukuza kazi ila wamewasimamisha kwa muda usiojulikana kutokana na viwango vipya vya mishahara vilivyotangazwa na serikali.

"Hatujawafukuza ila tumewasimamisha kwa muda usiojulikana kwa sababu kiwanda hakina uwezo wakuwalipa mishahara mipya ...," alisema Swai.

Alisema bodi itakaa na chama cha wafanyakazi wa kiwanda ilikuangalia jinsi ya kuwalipa hizo haki zao za msingi kama kutakuwa na uwezekano.

Akizungumzia kuhusu suala la kukaa na mfanyakazi kwa muda mrefu bila kumwajiri au kumpa mkataba wa muda, Meneja huyo alisema kwake kila mtu ni mfanyakazi hata kama analipwa kwa kutwa.

Wafanyakazi hao wapatao 500 walisimamishwa kazi mwishoni mwa wiki kwa njia ya mdomo na wengine kubandikwa majina yao kwenye ubao wa matangazo.

Idadi hiyo ya wafanyakazi 500 inaungana na ile ya wafanyakazi wengine 500 wa viwanda viwili vya nguo mkoani Arusha ambavyo pia vilitangaza kuwaachisha kazi kutokana na ongezeko la mishahara
 
Back
Top Bottom