Wafanyabiashara watatu kizimbani wakidaiwa kuingiza vifaa vya mawasiliano Tanzania bila kibali

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Wafanyabiashara watatu wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka nane yakiwemo ya kuingiza na kusimika vifaa vya mawasiliano bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) pamoja na kuisababisha Serikali hasara ya Sh69 milioni.

Washtakiwa hao ni Hemed Hemed (22), Daud Kalombe (31) na Lucas Nkunguru (29) wote wakazi wa Chamazi.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali, Ester Martin akisaidiana na Adolf Ulaya mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Rashid Chaungu.

Wakili Martin amedai washtakiwa wanakabikiwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 33/2021.

Kati ya mashtaka nane yanayowakabili washtakiwa hao, moja ni kuongoza genge la uhalifu kwa kuratibu shughuli za kihalifu, kuingiza vifaa vya mawasiliano bila kuwa na kubali cha TCRA, kusimika vifaa vya mawasiliano Tanzania na kuendesha mitambo ya mawasiliano bila kuwa na kibali.

Mashtaka mengine ni kutumia vifaa vya mawasiliano bila kudhibitishwa na TCRA, matumizi ya kilaghai ya vifaa vya mawasiliano, kuisababisha hasara Serikali na TCRA pamoja na kutakatisha Sh69, 690,000.

Akiwasomea mashtaka yao, wakili Martin amedai washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Desemba Mosi, 2020 na Februari 22, 2021 katika maeneo Dodoma, Mbeya na Dar es salaam walipanga kujipatia faida kwa kuratibu shughuli za kihalifu.

Katika shtaka la kuisababisha hasara, washtakiwa hao wanadaiwa katika siku na Mikoa hiyo, kwa matendo yao ya kihalifu waliisababishia Serikali na TCRA hasara ya Sh69 milioni.

Kuhusu shtaka la kutakatisha fedha, washtakiwa katika kipindi hicho na maeneo hayo, huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la kihalifu na matumizi ya kilaghai ya kukwepa tozo ambazo zingelipwa kwa ajili ya kusambaza mawasiliano, walijipatia Sh69 milioni.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, isipokuwa kwa kibali maalumu na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Hakimu Chaungu ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 27, 2021 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom