Wafanyabiashara wa URUSI Kukutana DSM.

Mkaruka

JF-Expert Member
Feb 5, 2013
19,629
34,172
charles-mwijage_210_120.jpg

TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa kongamano la wafanyabiashara wa Urusi la mwaka huu (RAF 2016), litakalofanyika jijini Dar es Salaam keshokutwa. Kwa mujibu wa Waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda, Charles Mwijage, mkutano huo wa siku mbili utahusisha kundi kubwa la wawakilishi wa Serikali ya Urusi, wenye viwanda na wafanyabiashara wakubwa wenye dhamira ya kuboresha mazingira ya kibiashara.

“Mipango inafanyika kwa ushirikiano na Serikali ya Urusi na taratibu za maandalizi zipo katika hatua za mwisho,” alisema Mwijage. Katika kongamano hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Urusi, Denis Manturov na Waziri Mwijage watasaini mkataba wa makubaliano kuhusu namna ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Mwijage alisema mkutano utajadili kuhusu ushirikiano wa kampuni za Tanzania na Urusi na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa Urusi, mamlaka za kifedha na serikali ili kupata uelewa mzuri wa uchumi wa Tanzania na kujenga ushirikiano wa pamoja.

Alisema lengo la kongamano hilo kuangalia fursa za soko la Tanzania hasa katika maeneo ya kilimo, madini, mafuta na gesi, utalii, miundombinu ya kiuchumi, viwanda, uvuvi, benki na bima kama vile elimu na afya.

“Warsha hii pia itatoa fursa za Biashara-kwa-Biashara, Serikali-kwa- Biashara na Serikali-kwa-Serikali. Kutakuwa na ziara katika viwanda vya ndani,” alisisitiza. Alisema mauzo kati ya Urusi na Tanzania mwaka 2014 yalifikia dola za Marekani milioni 154 na takwimu ya robo ya kwanza ya 2015 ilikuwa asilimia 71.

RAF 2016 inaandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara ( Urusi), Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ( Tanzania), Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi, Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Wafanyabiashara wa Tanzania watapata fursa kutembelea Ekaterinburg Julai 12 mwaka huu, wakati wa Maonesho ya kila mwaka ya INNOPROM ambayo hukutanisha wageni zaidi ya 46,000 kutoka nchi 70 duniani kote.
Chanzo:HabariLeo
 
Back
Top Bottom