Wafanya 'diet' hatarini kuwa dhaifu kiakili

Inside10

JF-Expert Member
May 20, 2011
26,060
23,939
Watu wanaopunguza mwili kwa kuacha kula baadhi ya vyakula – ‘diet’, wametahadharishwa kuwa huenda wakapata madhara ya kuwa dhaifu kiakili na kuandamwa na maradhi.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na harakati zinazofanywa sehemu mbalimbali, hasa katika mitandao ya kijamii, kuhamasisha watu kupunguza mwili na uuzwaji wa dawa tofauti zinazodaiwa kusaidia tatizo hilo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Walbert Mgeni, alisema kila chakula kina umuhimu wake mwilini, hivyo kukiacha kabisa kunaweza kusababisha mwili kukosa baadhi ya virutubisho.

“Watu wanataka kupunguza uzito, lakini wanapata elimu isiyo sahihi na kuamua kuacha kabisa vyakula vya wanga, hatushauri hivyo. Ukiacha kabisa utakuwa dhaifu, akili itashindwa kufanya kazi inavyotakiwa, ubongo unaweza kupata athari.

“Wanaotaka kufanya ‘diet’ waende kwa wataalamu wakashauriwe ili wasiathiri sehemu nyingine za mwili na wasifuate elimu ya mtaani,” alisema Mgeni.

Mtaalamu huyo alifafanua kuwa vyakula vimegawanyika katika makundi matano kutokana na umuhimu wake mwilini, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakichanganya kati ya makundi ya vyakula na virutubisho vinavyopatikana.

Aliyataja makundi hayo na virutubisho vyake kwenye mabano kuwa ni vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi mbichi (wanga), mikunde na vile vyenye asili ya wanyama (protini), mbogamboga (vitamini na madini), matunda (vitamini na madini) na sukari, mafuta na asali (nishati).

“Kundi la tano (sukari, mafuta na asali) tumekuwa tukishauri litumike kwa umakini mkubwa kwa sababu vyakula vyake vina uhusiano mkubwa na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, moyo na saratani. Kama mafuta, huwa tunashauri yale yanayotokana na mimea ndiyo mazuri kama vile karanga na alizeti.

“Tukila vyakula kutokana na makundi haya ndiyo tutapata mlo kamili, vinginevyo mtu anaweza kupata utapiamlo wa kuzidi au upungufu wa kirutibishi fulani,” alisema Mgeni.

Mtaalamu huyo alisema pia ingawa maji si chakula, lakini ni muhimu kwa uyeyushaji na usafirishaji wa virutubishi na kuondoa sumu mbalimbali mwilini.

Alisema wamekuwa wakitoa elimu sahihi kuhusu lishe bora kupitia kwa maofisa lishe waliopo katika halmashauri mbalimbali na kwa watoa huduma za afya, kwa sababu wanakutana moja kwa moja na wananchi.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto kwenye jamii ya kutozingatia ushauri unaotolewa na wataalamu kuhusu suala zima la lishe na umuhimu wake mwilini.

“Elimu ya kinga ni suala linalohusiana na mabadiliko ya tabia, ni gumu kwa sababu binadamu tunasahau madhara unayapata baadaye.

“Watu wanaambiwa fanyeni mazoezi, nyonyesheni watoto… kama Ukimwi kila siku watu wanaambiwa, wanasikia, lakini hawafuati,” alisema Mgeni.

KUPIMA UZITO

Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza Tanzania (TANCDA), linasema lishe bora na mazoezi ya viungo vyote ni muhimu ili kuwa na uzito unaotakiwa.

Kulingana na shirikisho hilo, uzito unaotakiwa ni muhimu katika kudhibiti maradhi ya moyo, shinikizo la damu, kisukari na hata kinga yake.

Kanuni ya kujua iwapo mtu ana uzito mkubwa ni kupima mzunguko wa kiuno yaani futi kamba ipite kwenye kitovu na ikizidi sentimita 84 kwa wanaume na 102 kwa wanawake inaashiria uzito mkubwa.

Pia unaweza kupima kwa kipimo cha uwiano wa uzito na urefu (BMI) ambacho hulinganisha uzito wa mtu kwa kila mraba wa urefu wake kujua uzito unaostahili kiafya.

Source: Mtanzania
 
Wao kama wataalamu wa lishe wa serikali kwanini wanasubiri kuibuka na matamko tu?

Kwanini wao wasiandae hizo kanuni na kuwafundisha watu kupitia magazeti,Luninga nk, kwani hawaoni kuwa watu wenye uzito ullipitiliza wanazidi kuongezeka Tanzania?

Juzi utafiti umeonesha kwamba Kilimanjaro ndio inaongiza wa watu kuwa na viribatumbo sasa wao ndio ilikuwa waongoze katika kutoa elimu hata kuanzisha kitengo kinachotoa hio huduma kwa malipo kiasi.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Wao kama wataalamu wa lishe wa serikali kwanini wanasubiri kuibuka na matamko tu?

Kwanini wao wasiandae hizo kanuni na kuwafundisha watu kupitia magazeti,Luninga nk, kwani hawaoni kuwa watu wenye uzito ullipitiliza wanazidi kuongezeka Tanzania?

Juzi utafiti umeonesha kwamba Kilimanjaro ndio inaongiza wa watu kuwa na viribatumbo sasa wao ndio ilikuwa waongoze katika kutoa elimu hata kuanzisha kitengo kinachotoa hio huduma kwa malipo kiasi.

Sent using Jamii Forums mobile app
Well said
 
Back
Top Bottom