Wafadhili waingilia kati hali ya Pemba | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wafadhili waingilia kati hali ya Pemba

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Aug 17, 2009.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Aug 17, 2009
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  Mataifa 15 na jumuiya moja ya kimataifa, wamezitaka Serikali mbili za Tanzania kuhakikisha kila mwananchi mwenye haki ya kushiriki uchaguzi mkuu mwakani anaipata na kuvitaka vyama vya siasa kuepuka vurugu katika kutoa mawazo na misimamo yao.

  Taarifa ya pamoja ya mataifa hayo fadhili na jumuiya hiyo iliyotolewa jana na mabalozi wa Japan, Norway, Canada na Marekani kwa niaba ya wengine, ilieleza kusikitishwa kwake na hali inavyoendelea Visiwani hususan Pemba ambako inaonekana utoaji vitambulisho umegubikwa na upendeleo.

  Mataifa mengine yaliyoandaa tamko hilo kuhusu mchakato wa uandikishaji wapiga kura Visiwani ni pamoja na Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Hispania, Sweden (Rais wa Jumuiya ya Ulaya- EU), Marekani na EU yenyewe.

  "Tungependa kusema kuwa haki ya kupiga kura ni kanuni ya msingi ya demokrasia... ni wajibu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata fursa ya kutimiza haki yao katika uchaguzi wa mwaka 2010," ilisema taarifa hiyo.

  Walisema wameshtushwa na taarifa kuwa Watanzania wengi walioko Pemba wanakabiliwa na matatizo ya kupata vitambulisho vya mkazi wa Zanzibar, ambavyo vinatumika kama vigezo vya mpiga kura kujiandikisha.

  Mabalozi hao walisema wanatarajia kuwa Serikali za Jamhuri ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar, zitahakikisha kuwa hatua zote zinachukuliwa kurekebisha kasoro zilizomo katika mchakato wa uandikishaji wapiga kura.

  "Hatua zitakazochukuliwa zilenge kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania wakiwamo Wazanzibari, atakayenyimwa haki ya kupiga kura mwakani," ilisema taarifa hiyo. Wakati huo huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema itaanza uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya pili nchi nzima, kuanzia Agosti 31 mwaka huu na kukamilika Februari mwakani.

  "Itafanyika kwa siku sita katika vituo vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari awamu ya kwanza na vituo vitafunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa 12 jioni," ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajab Kiravu.

  Kitakachofanyika wakati huo kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania kisheria, watakaokuwa na umri wa miaka 18 au zaidi, ikiwa ni pamoja na watakaofikisha umri wa miaka 18 siku ya upigaji kura mwakani.

  Pia kuandikisha wenye sifa ambao hawajawahi kujiandikisha na sasa wanataka kufanya hivyo lakini pia kuondoa wapiga kura waliofariki dunia au waliokosa sifa kwa mujibu wa sheria.

  Muda huo pia utatumika kurekebisha taarifa za wapiga kura zilizokosewa na waliohama kutoka kata moja kwenda nyingine au jimbo lingine. Kulingana na taarifa hiyo, wale waliopoteza kadi zao za kupigia kura, watapewa nyingine huku walioandikishwa wakipewa fursa ya kukagua taarifa zilizo kwenye Daftari.

  Taarifa iliongeza kuwa kwa wenye kadi lakini majina yao hayakuonekana kwenye Daftari wakati wa uchaguzi mkuu na uchaguzi mdogo uliopita, watatakiwa kwenda katika vituo vya kujiandikisha ili taarifa zao zichukuliwe.

  "Waliojiandikisha awali na hawajahama kata au majimbo ya awali na wana kadi kamilifu hawatahusika na utaratibu huu," ilisema taarifa.

  Kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji ya NEC, mikoa imegawanywa katika kanda sita za Lindi, Mtwara, Iringa na Ruvuma ambako wataanza Agosti 31 hadi Septemba 5; Dodoma, Mbeya, Rukwa na Singida (Septemba 21-26) na Tabora, Kigoma, Shinyanga (Novemba 23-28).

  Mingine ni Mwanza, Kagera, Mara (Desemba 21-26); Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga (Januari 18-23, 2010) na Dar es Salaam, Pwani, Morogoro (Februari 22-27). Ratiba kwa Zanzibar itatangazwa baadaye.
  http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=3191
   
Loading...