Wadau mbalimbali watoa maoni kuhusu Bunge la 11 lilivyokuwa. Wengine wasema lilikiuka sana Katiba na kuibeba Serikali badala ya wananchi. Wewe je?

Mchambuzi wa masuala ya Katiba, Sera, Siasa na Maendeleo ya Watu, Mcheleli Machumbana, alisema kwa miaka mitano ya Bunge la 11 lilikuwa na upitishaji wa sheria zinazokinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa mfano Bunge limeweka kinga ya kupindukia kwa viongozi wakuu wa nchi kushtakiwa, suala ambalo linatuhitaji kudai Katiba mpya kwa kuwa sheria ya namna hii inaondoa dhana ya usawa,” alisema.

Alisema Katiba inalitaka Bunge kutunga sheria isiyokinzana na Katiba na kama ikitungwa sheria ya namna hiyo itakuwa ni batili.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema jukumu kubwa la Bunge kwa mujibu wa Katiba sura ya 62-64, ni chombo cha uwakilishi, kuiwajibisha, kuisimamia, kuishauri serikali na kutunga sheria.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ya Bunge la 11 katika eneo la uwakilishi kama sehemu ya jukumu la Bunge, halikufanya kazi hiyo bali ilikuwa ni sehemu ya kutetea mhimili mwingine ambao ni serikali.

“Ukiniambia Bunge limefanya kazi kiasi gani ni lazima yaguswe maeneo hayo matatu, katika eneo la uwakilishi, kipindi chote cha miaka mitano ikilinganishwa la mabunge yaliyotangulia, hili halijatimizwa na badala yake lilikuwa sehemu ya uwakilishi wa serikali,” alisema Olengurumwa.

Alisema mwenendo wa Bunge ulivyokuwa wakati mwingine Spika alikuwa akizungumza kama Bunge limeungana na serikali, hivyo wananchi walikosa watu wa kuwatetea.
Kuhusu suala la kusimamia na kupitisha mabadiliko ya sheria, Olengurumwa alisema hilo halikusimamiwa kwa sababu Bunge lilipitisha mabadiliko ya sheria mbalimbali bila kuwashirikisha wawakilishi kikamilifu.

“Bunge la 11 ni wakati ambao limepitisha sheria kali mbalimbali bila kuwashiriki wawakilishi. Sheria hazitungwi kwa manufaa ya nchi,” alisema Olengurumwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC), Theodosia Nshala, alisema Bunge la 11 liliwanyima wananchi fursa kufuatilia utendaji wa wabunge wao baada ya kubadilisha utaratibu uliokuwa ukifanyika kipindi cha nyuma kwa kurusha matangazo yake mubashara kupitia vyombo vya habari.

Pia, alisema utaratibu wa kutokurusha matangazo hayo, ulichangia Bunge kuonekana halina mvuto kwa wananchi na walikata tamaa kufahamu kinachoendelea.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Paul Loisulie, alisema bunge hilo limejitahidi kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Hata hivyo, alisema imetokana na utendaji mzuri wa Rais Magufuli na mambo mengi yaliyozoeleka kuibuka bungeni hivi sasa yanaibuliwa na rais na wasaidizi wake.

Je, wewe mdau una mtazamo gani kuhusu Bunge la 11? Unakumbuka tukio gani lililotokea?
Lilikuwa bunge la hovyo kabisa kuwahi kuwepo Tanzania 🇹🇿
 
Bunge la 11 ndio bunge la hovyo kuwahi kutokea duniani,wabunge wa ccm hawachangii lolote wako kwa ajili ya kumsifia yesu na kuchukua posho tu
 
Bunge lilikuwa dhaifu sana. Viongozi wa Bunge walikuwa wanajikomba kwa Serikali bila sababu za maana. Mawazo kinzani yakigandamizwa na mapambio ya kuisifia Serikali yakiwa ndio mwongozo. Yaani bora hata Bunge la kabla ya Vyama vingi.
 
Wabunge wa CCM walitoka kwenye mstari kujadili bajeti na kukebehi na kuwachamba chademe. Ni Kama walitoka shule na debate ya Nani Bora CCM au upinzani. Sikufurahishwa nalo
 
Bunge la 11 limetimiza wajibu wake kikamilifu kwa kuwa ni Bunge rafiki wa serikali ila pia likiwa ndilo Bunge dhaifu kuliko mabunge yote katika kuisimamia serikali, ni Bunge kandamizi kuliko mabunge yote na ni Bunge lenye vituko kuliko mabunge yote!.
P
Nimekuelewa mkuu, hapo umesimama kweli
 
Back
Top Bottom