Daniel Mbega
JF-Expert Member
- Mar 20, 2013
- 338
- 180
Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya Zimbabwe, inatarajiwa kuwasili leo Alhamisi mchana wakiwa na msafara wa watu 29, wakiwemo wachezaji 20 pamoja na viongozi 9 tayari kwa ajili ya mchezo wa siku ya Ijumaa dhidi ya wenyeji Twiga Stars uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Zimbabwe watafikia hoteli ya DeMag iliyopo Kinondoni, ambapo jioni watapata fursa ya kufanya mazoezi katika uwanaja wa Azam Complex utakaotumika kwa mchezo siku ya Ijumaa.
Upande wa waamuzi wa mchezo huo wanatrajiwa kuwasili kesho mchana kwa shirikia la ndege la Kenya (KQ) wakitokea nchini Ethiopia, huku kamisaa wa mchezo kutoka Congo DR akiwasili jioni kwa KQ.
Maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika ambapo ulinzi na usalama utakuwepo wa kutosha, tiketi za mchezo huo zitauzwa eneo la uwanja Chamazi siku ya Ijumaa. Viingilio vya mchezo ni shilingi elfu mbili (2,000) kwa mzunguko na shilingi elfu tatu (3,000) kwa jukwaa kuu.
TFF inawaomba wadau, wapenzi wa mpira wa miguu kujitokeza kwa wingi siku ya Ijumaa kuwapa sapoti Twiga Stars katika mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Cameroon.