Wabunge wawili wa CHADEMA wasimamishwa, ni Susan Lyimo na Anatropia

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,397
Leo June 17 2016 idadi ya wabunge kusimamishwa imeongezeka baada ya Naibu Sika, Tulia Ackson kutangaza kusimamishwa kwa wabunge wawili ambao ni Mbunge wa viti Maalum CHADEMA Suzan Lyimo na Anatropia Theonest.

Mbune Suzan Lyimo amesimamishwa na Bunge kuhudhuria vikao vitano vya Bunge baada ya kubainika kusema uongo kwamba Jeshi la polisi nchini limenunua magari 777 ya washawasha wakati ukweli ni kwamba hiyo ni Idadi ya magari inayopangwa kuingizwa na jeshi hilo kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Licha ya Mbunge kuonesha ushirikiano kwa kamati ya maadili, haki na madaraka ya bunge, kamati imemwona Mbunge ni mzoefu wa shughuli za bunge hivyo anapaswa kusimamishwa vikao hivyo kuanzia June 17 hadi 24 mwaka huu.

Aidha Mbunge Anatropia Theonest amesimamishwa kuhudhuria vikao vitatu vya bunge kwa kosa la kulidanganya Bunge kuwa waziri wa ardhi na nyumba William Lukuvi alichukua ardhi ya wananchi akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam.

kas_23067-1290-2-30_220.jpg


Habari zaidi ndani ya Video hii:



==================


UTANGULIZI
1.1 Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 4 fasili (2) na (3) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 naomba kuwasilisha Mbele ya Bunge lako Tukufu Taarifa ya Kamati kuhusu shauri la Mhe. Susan A. Lyimo (Mb) na Mhe. Anatropia Theonest (Mb) kudaiwa kusema uongo Bungeni.

1.2 Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kukushukuru wewe binafsi kwa ujasiri mkubwa ulionao katika kuliongoza Bunge letu kwa ufanisi mkubwa.

1.3 Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 17 Mei, 2016, kwa mujibu wa Kanuni ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 ulipeleka malalamiko ya baadhi Wabunge mbele ya Kamati ili iyachunguze na kutoa mapendekezo yake kuhusiana na malalamiko hayo. Wabunge waliolalamika walieleza kuwa walalamikiwa walisema uongo Bungeni na kutoa taarifa ambazo hazina ukweli kinyume na Kanuni ya 63(1) na 64(1)(a) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

1.4 Mheshimiwa Spika, Wabunge waliowasilisha malalamiko ni Mheshimiwa Yusuph Hamad Masauni (Mb) Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyemlalamikia Mhe. Suzan Lyimo (Mb) na Mheshimiwa William Lukuvi (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi aliyemlalamikia Mheshimiwa Anatropia Theonest (Mb).

1.5 Mheshimiwa Spika, baada ya maelekezo hayo taratibu za kuanza kusikiliza shauri hili zilifanyika ikiwa ni pamoja na kuwaita mashahidi kwa Hati za Wito. Hati hizo zilielekeza kuwa waheshimiwa hao walitakiwa kufika mbele ya Kamati ili kutoa ufafanuzi kuhusu malalamiko yao na Wabunge waliolalamikiwa walitakiwa kufika mbele ya Kamati ili waweze kueleza ni kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kukiuka Kanuni ya 63 (1) na 64 (1) (a) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.

1.6 Mheshimiwa Spika, taarifa ambazo zinazodaiwa kuwa ni za uongo zilitolewa kwa nyakati tofauti katika Bunge la Kumi na Moja ambapo, katika tukio la kwanza Mheshimiwa Anatropia Theonest (Mb) alituhumiwa kutoa kauli katika Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi na Moja na matukio mengine ni katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja unaoendelea hivi sasa.

2.0 CHIMBUKO LA SHAURI LA MALALAMIKO YA MHE. YUSUPH HAMAD MASAUNI (MB), NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI DHIDI YA MHE. SUZAN LYIMO (MB)

2.1 Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 12 Mei, 2016, Mhe. Yusuph Hamad Masauni (Mb), aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya 68(7) na 64(1) (a) kuwa siku ya tarehe 11 Mei, 2016 wakati wa mjadala wa Hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee Mhe. Suzan Lyimo (Mb) alisema uongo Bungeni.

2.2 Mheshimiwa Spika, akijenga hoja yake Mhe. Masauni (Mb) alisema kuwa Mhe. Suzan Lyimo (Mb) alipokuwa akichangia alitoa kauli kwamba, kuna magari 777 ya washawasha ya polisi yameingizwa nchini, taarifa za uhakika alizonazo kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ni kwamba, magari ya washawasha yaliyonunuliwa ni 32 tu na sio 777 yaliyotajwa na Mhe. Susan Lyimo.

2.3 Mheshimiwa Spika, Mhe. Masauni (Mb) aliomba mwongozo wa Kiti kwamba ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa na Bunge kutokana na maelezo hayo ya uongo Bungeni.

2.4 Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kumbukumbu Rasmi za Bunge za tarehe 11 Mei, 2016 Mhe. Suzan Lyimo(Mb) alinukuliwa akisema kama ifuatavyo;

“Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kama wakinamama kukubali hali hii iendelee na nasema hivi kwa sababu nchi hii ina uwezo kama tuliweza kununua magari ya washawasha narudia, kama tuliweza kununua magari ya washawasha 777 ambayo ni 50 tu yalitumika kwenye uchaguzi na gari moja nime-google kwa Alibaba ambao ndio wanaleta magari, gari moja lina gharama ya shilingi milioni 150 mpaka 400 lakini tuchukue wastani wa dola laki tatu kwa moja.

Inamaana kwa magari 700 ni dola laki mbili na kumi milioni ukizipeleka kwenye hela za kitanzania ni bilioni 420, bilioni 420 kwa kata 3990 tulizonazo Tanzania nzima na ambulance, ambayo ambulance moja nime-google vilevile ambayo tena ni advance inaenda kwa shilingi milioni 105 ukigawanya ina maana kila kata hapa Tanzania ingepata ambulance (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, tunajiuliza priorities za nchi hii ni zipi, ni afya ya mtanzania au kitu gani? Kwa sababu kama ni suala nimesema magari 77 ya washawasha yangeweza kubaki, tunazungumzia yale 700 yaliyobaki yaani yangetosha ambulance. (Makofi).

2.5 Mheshimiwa Spika, kufuatia ombi hilo la mwongozo lililoombwa na Mhe. Masauni, Mhe. Spika alielekeza kuwa, kwa kuwa Mhe. Suzan Lyimo (Mb) hakuwepo ukumbini wakati mwongozo ulipoombwa, hivyo atakaporudi katika kikao cha jioni atatakiwa kufuta kauli yake au kutoa uthibitisho ndani ya Bunge.

2.5 Mheshimiwa Spika, katika kikao cha jioni cha siku tajwa, Mheshimiwa Spika alimtaka Mhe. Suzan Lyimo kufuta maneno aliyoyatoa au kuthibitisha kauli yake na Mhe. Lyimo alionekana kuwa tayari kuthibitisha. Kwa kuwa uthibithisho wake ulielekea kuwa ungeweza kuchukua muda mrefu, Mheshimiwa Spika alimtaka Mhe. Lyimo awasilishe uthibitisho wake kwa maandishi na kwamba Spika angewasilisha uthibitisho huo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Mhe. Lyimo aliwasilisha uthibitisho wake wa maandishi kama alivyotakiwa na Spika.

3.0 HADIDU ZA REJEA NA HOJA ZA MSINGI (ISSUES)
3.1 Mheshimiwa Spika, Katika Waraka wa Spika wa kuleta shauri kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ulirejea Kanuni ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongea ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hiyo:

4(1) Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itatekeleza majukumu yafatayo:-
(a) Kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala yote ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge yatakayopelekwa na Spika;

(b) Kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya wabunge yatakayopelekwa na Spika

4.0 UCHAMBUZI WA KAMATI KUHUSU MALALAMIKO YA MHESHIMIWA YUSSUF HAMAD MASAUNI (MB) DHIDI YA MHESHIMIWA SUZAN LYIMO (MB)

4.1 Mheshimiwa Spika, kwa mujibu waraka uliouwasilisha mbele ya Kamati na kwa kuzingatia maudhui yaliyo katika malalamiko ya Wabunge waliowasilisha malalalamiko yao Kamati inajukumu la kuchunguza kwa kujiuliza hoja mbili ambazo ni:-

(a) Iwapo Mheshimiwa Suzan Lyimo (Mb) alisema uongo au kutoa taarifa ambazo hazina ukweli kinyume na Kanuni ya 63 (1) na 64(1) (a) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.

(b) Ikiwa hoja (a) itathibitika, ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.

4.2 Mheshimiwa Spika, katika kufanya uchambuzi wake kuhusu suala hili, Kamati imefanya rejea zifuatazo;
(i) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
(ii) Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
(iii) Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 3 Februari, 2016, tarehe 10 na 11 Mei, 2016.
(iv) Uthibitisho uliowasilishwa na Mbunge aliyetakiwa kuwasilisha uthibitisho huo.
(v) Mahojiano na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati.

4.3 Mheshimiwa Spika Kanuni za Bunge zilizotungwa chini ya Ibara ya 89(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeweka utaratibu maalum unaopaswa kutumika kwa mambo yote yanayohusu uendeshaji wa Bunge. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuweka Kanuni za majadiliano Bungeni.

4.4 Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Bunge zimeweka masharti kuhusu maneno au taarifa zinazoruhusiwa kutolewa Bungeni. Kanuni ya 63 (1) na 64(1)(a) za Kanuni za Kudumu za Bunge zimekataza Mbunge yeyote kutoa taarifa au kusema uongo Bungeni na zinamtaka Mbunge kusema au kutoa taarifa ambazo ana uhakika nazo. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hizo kama ifuatayo;-

“63(1) Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, ni marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge yeyote anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli na siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu”

“64(1) (a) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge:-
(a) Hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli”

5.0 MAHOJIANO KATIKA SHAURI LA MHE. HAMAD MASAUNI (MB) DHIDI YA MHE. SUZAN LYIMO (MB)
5.1 Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 31 Mei, 2016, Kamati ilipata fursa ya kumhoji Mhe. Hamadi Masauni (Mb) kuhusiana na malalamiko yake dhidi ya Mhe. Suzan Lyimo (Mb). Mhe. Masauni alieleza kuwa alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee Mhe. Suzan Lyimo (Mb) alieleza kuwa Serikali imenunua Magari ya Washawasha 777 badala ya kununua MRI na CT Scaners. Mhe. Masauni alieleza kuwa mchango huo ulilenga kupotosha jamii kwani Serikali haijanunua idadi hiyo ya magari ya washawasha bali Magari 777 ni mpango wa Serikali wa kuboresha Jeshi la Polisi kwa kulipatia vitendea kazi ikiwemo magari. Magari 777 yanayotarajiwa kununuliwa ambapo baadhi yamekwishapokelewa ni kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya Jeshi la Polisi na kwamba kati ya Magari hayo, 32 tu ndiyo magari ya washawasha na mengine ni kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kipolisi ikiwemo ya oparesheni za polisi, doria, zimamoto na kadhalika.

5.2 Mheshimiwa Spika, Mhe. Hamad Masauni (Mb) alipohojiwa kuhusu majibu yake katika Swali la Nyongeza lililoulizwa na Mhe. Suzan Lyimo kuhusu idadi hiyo ya magari ya washawasha alieleza kuwa, katika kujibu swali la nyongeza hakusema kuwa Serikali imenunua magari ya Washawasha 777. Mhe. Masauni alirejea Hansard ya tarehe 4 Februari, 2016 ambayo inasomeka

Nanukuu
“Si kweli kwamba magari ya washawasha yamenunuliwa na hayana tija. Magari ya washawasha yamenunuliwa ikiwa ni miongoni mwa ile program ya kununua magari 777, kwa ajili ya matumizi ya askari kwa hiyo magari haya yanasaidia sana na bado mengine yatafika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za polisi”

5.3 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Masauni aliieleza Kamati kuwa majibu aliyoyatoa hayaelezi kuwa Serikali imenunua Magari 777 ya Washawasha bali inaeleza kuwa magari hayo siyo washawasha pekee bali ni kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya Jeshi la Polisi. Kutokana na maelezo hayo, Mheshimiwa Masauni aliieleza Kamati kuwa Mhe. Suzan Lyimo alisema uongo Bungeni.

5.4 Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata fursa ya kumhoji Mhe. Suzan Lyimo kuhusiana na malalamiko ya Mhe. Yusuph Masauni. Mhe. Suzan Lyimo aliieleza Kamati kuwa aliwasilisha utetezi wake kwa Spika. Kamati iliupata utetezi wake. Utetezi huo umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni:

(i) Ripoti kutoka vyombo vya habari kama Jamii Forum na Gazeti la Mwananchi Online
(ii) Hansard ya Bunge kuhusu majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Eng. Masauni ya tarehe 04/02/2016 alipokuwa akijibu swali ya nyongeza kuhusu ununuzi wa Magari ya washawasha 777 badala ya kununua CT-Scaners na MRI pesa ambayo ingetosha kununua mashine hizo kwa hospitali zote za rufaa nchi nzima.
(iii) Mtandao wa Alibaba ambao ni Wakala wa Kimataifa wa kuuza bidhaa mbalimbali yakiwemo magari ya aina zote.

5.5 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Suzan Lyimo (Mb) alipofika mbele ya Kamati alieleza kuwa katika vielelezo alivyowasilisha. Pia kuna taarifa kutoka Habarikablog.blogspot.com. Kamati ilipofanya uchambuzi wa vielelezo hivyo, ilibaini kwamba katika vielelezo hivyo hakukuwa na Kielelezo cha Mwananchi online bali Mwanahalisi Online. Aidha, katika vielelezo alivyowasilisha kwa Spika kielelezo cha Habarikablog.blogspot.com hakikuainishwa.

5.6 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Suzan Lyimo (Mb) aliieleza Kamati kuwa alirejea Kanuni ya 63(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2016 kwamba Mbunge hatachukuliwa kuwa anasema uongo iwapo anafanya rejea ya habari kuhusu jambo fulani lililotangazwa au lililoandikwa na vyombo vya habari. Hivyo alisisitiza kuwa kauli alizozisema Bungeni hazikuwa za uongo kwa kuwa alifanya rejea ya vyombo vya Habari alivyovitaja.

5.8 Mheshimiwa Spika, Kamati ilijiuliza swali moja la msingi kuhusiana na shauri hili, nalo ni Je? Mhe. Suzan Lyimo alisema uongo Bungeni kinyume na Kanuni ya 64(1) kama alivyolalamikiwa na Mhe. Yussuf H. Masauni (Mb).

5.9 Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kama ilivyonukuliwa katika taarifa hiyo, Mbunge yoyote haruhusiwi kusema uongo Bungeni.

5.10 Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Bunge hazijaeleza zipi ni habari zenye sifa ya kuwa na ukweli. Hata hivyo, Kanuni ya 63(1) inaeleza kuwa Mbunge anatakiwa kutoa Bungeni taarifa ambazo ana uhakika nazo na si za kubahatisha tu. Kwa maana nyingine Mbunge anapaswa kutoa taarifa ambazo amezifanyia utafiti na kuwa na uhakika na jambo ambalo analizungumza.

5.11 Mheshimiwa Spika, majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Yussuf Hamad Masauni (Mb) hayaelezi kuwa Serikali imenunua Magari 777 ya Washawasha bali inasema magari hayo yamenunuliwa kwa ajili ya matumizi ya askari na kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kipolisi. Aidha Naibu Waziri ameeleza kuwa kati ya Magari hayo, ni 32 tu ndiyo ya washawasha.

Mheshimiwa Spika, Aidha, katika vielelezo vyote vilivyowasilishwa na Mhe. Suzan Lyimo, hakuna kielelezo hata kimoja kinachothibitisha kuwa Serikali imenunua magari ya washawasha 777 jambo ambalo lina dhihirisha kuwa alisema uongo Bungeni.

5.12 Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo hayo na kwa mujibu wa masharti ya Kanuni za Bunge Kamati inamtia hatiani Mheshimiwa Suzan Lyimo kwa Kusema uongo Bungeni.

5.13 Mheshimiwa Spika, baada ya Kumtia hatiani Mheshimiwa Suzan Lyimo (Mb) na kwa kuzingatia Kanuni ya 63(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Kamati inapendekeza mbunge huyu kupewa adhabu ifuatayo:-

Katika kupendekeza adhabu Kamati ilizingatia kuwa Mhe. Suzan Lyimo ni kosa lake la kwanza na alitoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati pamoja na kutekeleza kikamilifu maelekezo ya Kiti cha Spika.

Hata hivyo, Kamati ilizingatia pia kuwa Mhe. Suzan Lyimo ni mzoefu katika shughuli za Bunge na anaelewa vyema masharti ya Kanuni za Bunge, kwa msingi huo Kamati inaliomba Bunge lako tukufu likubali pendekezo la Kamati la kumsimamisha Mhe. Suzan Lyimo (Mb) asihudhurie vikao vitano (5) vya Bunge mfululizo kuanzia tarehe 17 Juni, 2016 hadi tarehe 24 Juni, 2016.

2.2.1 CHIMBUKO LA MALALAMIKO YA MHE. WILLIAM V. LUKUVI (MB) DHIDI YA MHE. ANATROPIA THEONEST (MB)
2.2.2 Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 4 Februari, 2016 Mhe. William Lukuvi (Mb) Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwasilisha katika Meza ya Spika katika Ukumbi wa Bunge barua ya malalamiko akilalamikia kuwa mnamo 3 Februari, 2016 katika Mkutano wa Pili, Kikao cha Saba, Bunge la Kumi na Moja wakati wa majadiliano kuhusu Kamati ya Mipango, Mhe. Anatropia Theonest wakati alipokuwa akichangia kuhusu Kamati ya Mipango alisema uongo Bungeni kwa kudai kuwa yeye Mhe. Lukuvi, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mwaka 2011 alihusika na uporaji wa viwanja walivyopewa waathirika wa mabondeni na kwamba jambo hilo kweli kwa kuwa Mwaka 2011, Mhe. Lukuvi hakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam bali alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.

2.2.3 Mheshimiwa Spika, Mhe. Lukuvi katika maombi ya mwongozo alikitaka kiti kimtake Mhe. Anatropia Theonest kufuta kauli yake au arekebishe kauli yake. Kwa namna moja au nyingine barua hiyo haikumfikia Spika hivyo, Mhe. Lukuvi aliandika tena barua nyingine mwezi Mei, 2016 kukumbushia kuhusu malalamiko yake ili yafanyiwe kazi.

2.2.4 Mheshimiwa Spika, Malalamiko ya Mhe. Lukuvi yanatokana na mchango wa Mhe. Anatropia Theonest alipokuwa akichangia Bungeni mnamo tarehe 3 Februari, 2016 wakati wa majadiliano kuhusu Kamati ya Mipango ambapo alieleza yafuatayo:

…”.Natokea katika jiji la Dr es salaam ambalo limekuwa na migogoro mikubwa ya ardhi. Wananchi zaidi ya kaya 16000 zimewekewa alama “x” kwamba, kwenye mabonde, wanaenda kubomolewa majumba yao. Zaidi ya wananchi 99,000 watakuwa ni watu wasio na makazi. Changamoto ni kwamba serikali ilikuwepo, watendaji walikuwepo, Waziri Lukuvi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alifanya nini wakati wote ambapo wananchi wameishi katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 1998 yalitengwa maeneo ya Tegeta ili wananchi waliokuwa wanaishi mabondeni wahamie, hali kadhalika mwaka 2011 akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam. Wananchi wa Jimbo la Segerea, wananchi wa Ilala, wanataka viwanja vyao kwa sababu wanasema anahusika katika uporaji wa maeneo waliyopewa wananchi waliokuwa wanaishi mabondeni.”

2.2.5 Mheshimiwa Spika, katika malalamiko yake Mhe. William Lukuvi (Mb) Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alieleza kuwa tuhuma zilizotolewa na Mhe. Anatropia kumhusisha na uporaji wa maeneo waliyopewa wananchi wa Jimbo la Ilala na Segerea walokuwa wanaishi mabondeni siyo za kweli kwani mwaka 2011 alikuwa ni Waziri wa Nchi na hakuhusika katika tuhuma hizo na wakati huo hakuwa Mkuu wa Mkoa.

6.0 HADIDU ZA REJEA NA HOJA ZA MSINGI (ISSUES)
6.1 Mheshimiwa Spika, Katika Waraka wa Spika wa kuleta shauri kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ulirejea Kanuni ya 4(1) (a) na (b) ya Nyongea ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hiyo:

4(1) Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itatekeleza majukumu yafatayo:-
(c) Kuchunguza na kutoa mapendekezo khusu masuala yote ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge yatakayopelekwa na Spika;
(d) Kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya wabunge yatakayopelekwa na Spika

7.0 UCHAMBUZI WA KAMATI KUHUSU MALALAMIKO YA MHESHIMIWA WILLIAM LUKUVI (MB) DHIDI YA MHESHIMIWA ANATROPIA THEONEST (MB)
7.1 Mheshimiwa Spika, kwa mujibu waraka uliouwasilisha mbele ya Kamati na kwa kuzingatia maudhui yaliyo katika malalamiko ya Wabunge waliowasilisha malalalamiko yao Kamati inajukumu la kuchunguza kwa kujiuliza hoja mbili ambazo ni:-

(a) Iwapo Mheshimiwa Anatropia Theonest (Mb) alisema uongo au kutoa taarifa ambazo hazina ukweli kinyume na Kanuni ya 63 (1) na 64(1) (a) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.
(b) Ikiwa hoja (a) itathibitika, ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.

7.2 Mheshimiwa Spika, katika kufanya uchambuzi wake kuhusu suala hili, Kamati imefanya rejea zifuatazo;
(vi) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
(vii) Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
(viii) Kumbukumbu Rasmi za Bunge za Tarehe 3 Februari, 2016, tarehe 10 na 11 Mei, 2016.
(ix) Uthibitisho uliowasilishwa na Mbunge aliyetakiwa kuwasilisha uthibitisho huo.
(x) Mahojiano na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati.

7.3 Mheshimiwa Spika Kanuni za Bunge zilizotungwa chini ya Ibara ya 89(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeweka utaratibu maalum unaopaswa kutumika kwa mambo yote yanayohusu uendeshaji wa Bunge. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuweka Kanuni za majadiliano Bungeni.

7.4 Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Bunge zimeweka masharti kuhusu maneno au taarifa zinazoruhusiwa kutolewa Bungeni. Kanuni ya 63 (1) na 64(1)(a) za Kanuni za Kudumu za Bunge zimekataza Mbunge yeyote kutoa taarifa au kusema uongo Bungeni na zinamtaka Mbunge kusema au kutoa taarifa ambazo ana uhakika nazo. Kwa urahisi wa rejea nanukuu Kanuni hizo kama ifuatayo;-

“63(1) Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, ni marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge yeyote anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli na siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu”

“64(1) (a) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge:-

(b) Hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli”

8.0 MAHOJIANO KATIKA SHAURI LA MHESHIMIWA WILLIAM LUKUVI DHIDI YA MHE. ANATROPIA THEONEST

8.1 Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa William Lukuvi (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alifika mbele ya Kamati Mnamo tarehe 1 Juni, 2016 kama Hati yake ya Wito ilivyomtaka. Baada ya kufika aliieleza Kamati kuwa Mhe. Anatropia Theonest (Mb) alipokuwa akichangia katika Kamati ya Mipango, alilieleza Bunge na Umma wa watanzania kuwa yeye Mhe. Lukuvi (Mb) alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alihusika katika kupora viwanja vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya waathirika wa Mafuriko. Mhe Lukuvi aliieleza kamati kuwa jambo hilo si la kweli kwani Mwaka 2011 yeye hakuwa Mkuu wa Mkoa bali alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.

8.2 Mheshimiwa Spika, Aidha, Mhe. Lukuvi aliieleza Kamati kuwa taarifa zilizotolewa na Mhe. Anatropia si tu kwamba zilikuwa za uongo bali zimemfedhehesha sana kwa kuhusishwa na uporaji wa viwanja vya watu wanyonge na kwamba jambo hilo limemdhalilisha mbele ya jamii kwa kudhaniwa kuwa anajihusisha na uporaji wa ardhi.

8.3 Mheshimiwa Spika, wakati wa mahojiano na Kamati Mhe. Anatropia Theonest alikiri mbele ya Kamati kuwa alisema uongo Bungeni kwa kuwa, ni kweli Mhe. Luvuvi hakuwa Mkuu wa Mkoa Mwaka 2011 hivyo asingeweza kuhusika na uporaji wa viwanja vya waathirika wa mafuriko. Aidha, alieleza iwapo kama angeambiwa jambo hilo akiwa Bungeni, kuwa kauli aliyokuwa ameitoa siku hiyo ilikuwa ya uongo angeweza kuifuta. Alionesha kusikitika kuona kuwa suala hili limefika Kamati ya Maadili ambalo lingeweza kumalizika ndani ya Ukumbi wa Bunge ikiwa angepata fursa.

8.4 Mheshimiwa Spika, katika maelezo ya kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo kama alivyotakiwa kufanya alieleza kuwa utaratibu uliowekwa na Kanuni ya 63 haukufutwa. Kanuni ya 63 (3) inaelekeza kuwa ikiwa mbunge yeyote ataona kuwa Kanuni inakiukwa atasimama mahali pake na kusema “kuhusu utaratibu”akiruhusiwa atataja kanuni iliovunjwa.

Anaendelea kusema kuwa wakati anaongea hadi kumaliza hakuna Mbunge au Waziri aliyefanya hivyo. Aidha, alieleza kuwa hakuna Kanuni inayoelekeza kupeleka shauri kwa Spika ikiwa Mbuge ameshindwa kutumia Kanuni ya 63.

8.6 Mheshimiwa . Spika, baada ya maelezo hayo, Kamati ilijiridhisha dhahiri kuwa Mhe. Anatropia Theonest (Mb) alikiri kuwa alisema maneno yasiyo ya kweli ndani ya bunge. Kwa maneno yake Mhe. Anatropia aliieleza kamati kuwa Mhe.

William Lukuvi (Mb) Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi hakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam mwaka 2011, kwa hiyo, kwa vyovyote vile asingeweza kuhusika kupora maeneo ya waathirika wa mabondeni wa Segerea na Ilala.
Mheshimiwa Spika, kamati inamtia hatiani Mhe. Anatropia Theonest (Mb) kwa kusema uongo Bungeni kinyume na Kanuni ya 63(1) na 64 ya Kanuni za kudumu za Bunge.

8.7 Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo na ufafanuzi huo sasa tujielekeze katika hoja ya pili kuwa (b) Ikiwa hoja (a) itathibitika, ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa na Bunge kwa Mujibu wa Kanuni za Bunge.?
Katika Kanuni ya 63(8) inaeleza kuwa Mbunge aliyetakiwa kutoa uthibitsho kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge au atakataa kujirekebisha kwa kufuta kauli au usemi wake Spika atamwadhibu kwa kumsimamisha Mbunge huyo ili asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi vitano mfululizo kuanzia tarehe ambayo Taarifa hii itawasilishwa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilizingatia masuala yafuatayo katika kufikia mapendekezo ya adhabu:-

(i) Mbunge huyo alitoa ushirikiano kwa Kamati kwa maana alipoitwa alifika bila kukosa na alikiri kosa lake bila kupoteza muda wa Kamati.
(ii) Kutokana na maneno aliyoyasema na kuufikia umma ni dhahiri yalimdhalilisha Mhe. Lukuvi na kuharibu heshima yake katika jamii ya watanzania.
Kwa kuzingatia maelezo hayo Kamati inaliomba Bunge lako tukufu likubali pendekezo la Kamati la kumsimamisha Mhe. Anatropia Theonest (Mb) na asihudhurie vikao vitatu (3) vya Bunge mfululizo kuanzia tarehe 17 Juni, 2016 hadi tarehe 22 Juni, 2016.

Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza adhabu hizi ili iwe
fundisho kwake na kwa waheshimiwa wabunge wengine wasioheshimu na kutiii Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa, mapendekezo haya kuhusu adhabu kwa Waheshimiwa Wabunge hawa itaenda sambamba na masharti ya Kanuni ya 75 ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha, Kamati inapenda kueleza kuwa adhabu zilizopendekezwa kwa Wabunge hawa zinaenda sambamba na Masharti ya Kanuni ya 75 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inayoeleza kuwa Mbunge aliyesimamishwa kazi hataruhusiwa tena kuingia katika sehemu yoyote ya Ukumbi wa Bunge na Maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa, na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.

8.0 HITIMISHO
9.1 Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii kuwasilisha maoni ya Kamati kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na napenda nitumie nafasi hii tena kukupongeza kwa dhati kwa jinsi unavyoliongoza Bunge hili ambalo ni chombo cha uwakilishi wa Wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ili kuhakikisha kuwa ustawi wa wananchi unakuwa ndio kipaumbele cha kwanza.

9.2 Mheshimiwa Spika, kipekee, nawashukuru Wajumbe wote wa Kamati, kwa kazi nzuri ya kujadili na kuchambua kwa umakini mkubwa shauri hili kwani katika kutekeleza jukumu hili walizingatia utaifa mbele na misingi ya haki. Kwa heshima naomba niwatambue kwa majina kama ifuatavyo:-

(i) Mhe. Kapt (Mst), George H. Mkuchika, (Mb) - M/kiti
(ii) Mhe. Almas Maige, (Mb) - Makamu Mwenyekiti
(iii) Mhe. Rashid Ali Abdallah,(Mb)…………..Mjumbe
(iv) Mhe. Amina Nassoro Makilagi, (Mb)…….Mjumbe
(v) Mhe. Dkt. Christine G. Ishengoma,(Mb)……Mjumbe
(vi) Mhe. Othman Omar Haji,(Mb)……………Mjumbe
(vii) Mhe. Rose Kamili Sukum,(Mb)………………Mjumbe
(viii) Mhe. George Malima Lubeleje,(Mb)………Mjumbe
(ix) Mhe. Dkt. Suleiman Ally Yussuf,(Mb)……….Mjumbe
(x) Mhe. Susan Anselm Lyimo,(Mb) ……………Mjumbe
(xi) Mhe. Tunza Issa Malapo,(Mb)………………Mjumbe
(xii) Mhe. Asha Abdallah Juma,( Mb)………….Mjumbe
(xiii) Mhe. Augustino M. Masele,(Mb)……………Mjumbe
(xiv) Mhe. Hafidh Ali Tahir, (Mb)…………………..Mjumbe
(xv) Mhe. Innocent Sebba Bilakwate, (Mb)……Mjumbe
(xvi) Mhe. Adamson E. Mwakasaka(Mb)……….Mjumbe

Aidha, napenda kumshukuru kwa dhati Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas D. Kashililah, kwa kuisaidia Kamati kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Kipekee, nawashukuru Ndugu Pius T. Mboya, Kaimu Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria, kwa ushauri wa Kisheria walioutoa katika kuisaidia Kamati. Aidha napenda kuwashukuru ndugu Matamus Fungo, Maria Mdulugu, Makatibu wa Kamati, Lweli Lupondo, Sekretarieti upande wa Hansard na Editruda Kilapilo, msaidizi wa Kamati kwa kuratibu vyema kazi za Kamati na kuhakikisha kuwa Taarifa hii inakamilika mapema.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni matarajio yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge wataipokea na kwa kauli moja wataikubali hoja iliyopo mbele yetu ya matokeo ya taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ya uchunguzi kuhusu Mhe. Suzan Lyimo na Mhe. Anatropia kusema uongo Bungeni kwa nyakati tofauti kama tulivyoeleza katika taarifa hii ili kuimarisha nidhamu ndani ya Bunge letu Tukufu na kuhakikisha kuwa Kanuni za Majadiliano Bungeni, zinaheshimiwa na kuzingatiwa na Wabunge wote.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Kapt (Mst) George H. Mkuchika, (Mb.)
 
Haki imetendeka! Wapinzani wengi wana sifa kuu ya kuropoka na uchochezi!

Hii adhabu bado ni ndogo kulinganisha na madhara ambayo wanaweza sababisha!

Kama ingewezekana kungekuwa pia kuna adhabu ya viboko kabisa! Yani wanachukua story za mzee wa shanga wanazipeleka bungeni!

UKAWA msipo badilika mtaliona bunge chungu ...!
 
Wapate haki yao kama ilivyo. Nadhani watapunguza kejeli na ulopokaji.

Wasifanye watu wasio wabunge ndo hawana akili.
 
Bunge limewasimamisha wabunge wa Chadema Suzan Lyimo kutohudhuria vikao 5 na Anatropia Theonest vikao 3 kwa kosa la kusema uongo Bungeni.
Mpaka wanyoke. Maana walizoea kuka kwa majungu, huku wanamtuma Lusinde awasemee huku wanakanusha.

Leo asubuhi ndo wameoneka wakijichanganya. Mbowe waachieni watu wafikiri kwa akili zao.
 
Mpaka wanyoke. Maana walizoea kuka kwa majungu, huku wanamtuma Lusinde awasemee huku wanakanusha.

Leo asubuhi ndo wameoneka wakijichanganya. Mbowe waachieni watu wafikiri kwa akili zao.
Hakika. Ni emuona James Mbatia ingawa alikaa kiti cha mbele lakini alikuwa wa mwisho kuondoka. Wabunge walisita kutoka ni mpaka walipomuona Mbowe anainuka
 
Mpaka wanyoke. Maana walizoea kuka kwa majungu, huku wanamtuma Lusinde awasemee huku wanakanusha.

Leo asubuhi ndo wameoneka wakijichanganya. Mbowe waachieni watu wafikiri kwa akili zao.
For sure mijinga ndiyo itakayonyooka!! hasa wale walioenda Bungeni kufuata sitting allowances na kulala kwa sababu ya hangover za ulevi
 
Haki imetendeka! Wapinzani wengi wana sifa kuu ya kuropoka na uchochezi!

Hii adhabu bado ni ndogo kulinganisha na madhara ambayo wanaweza sababisha!

Kama ingewezekana kungekuwa pia kuna adhabu ya viboko kabisa! Yani wanachukua story za mzee wa shanga wanazipeleka bungeni!

UKAWA msipo badilika mtaliona bunge chungu ...!
Mkuu watabadilka vipi kama gear zenyewe wanafundishwa kubadilishia angani? Kwa Dkt. Tulia watatulia wenyewe watabadilisha gear angani, majini, matopeni, mchangani, n.k hawataweza. Kitu ni kanuni tu, unahisi kuonewa kata rufaa, na hilo limemshinda Lissuuu wala hana cha kusema tena.
 
Back
Top Bottom