Lunyungu
JF-Expert Member
- Aug 7, 2006
- 8,873
- 1,898
2008-04-12
Na John Ngunge, Dodoma
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa jana bungeni, imependekeza Wabunge waondolewe kwenye nafasi za ujumbe wa bodi za mashirika ya umma.
Kadhalika, ofisi ya CAG imebaini ukiukwaji wa taratibu za Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 katika ofisi mbalimbali na katika Kitengo cha Kupakia na kupakua Kontena Bandarini (TICTS).
Mapema akiongea na waandishi wa habari jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Ludovick Utouh, alisema utaratibu uliotumika kuongeza muda wa mkataba huo kutoka miaka kumi hadi 25 ulikiuka taratibu.
Mbali na kupendekeza wabunge kuondolewa kwenye Bodi za Mashirika ya Umma, pia imependekeza kuboreshwa kwa nidhamu katika matumizi ya serikali.
Mapendekezo mengine kwa mujibu wa Bw. Utouh ni kupitia upya mfumo wa ubakizaji mapato yatokanayo na makusanyo katika mafungu na kurekebisha vipengele vya Sheria vinavyokinzana na kuimarisha ukusanyaji wa mapato utokanao na vyanzo vya ndani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Bw. Zitto Kabwe, ambaye alihudhuria mkutano huo, aliunga mkono pendekezo la wabunge kuondolewa kwenye bodi za mashirika ya umma.
Alisema kuwepo kwa wabunge katika bodi hizo kunakiuka dhana nzima ya utawala bora na kwamba atahakikisha taratibu zinabadilishwa ili kuwaondoa.
Alisema anafanya mawasiliano na Spika wa Bunge, Bw. Samwel Sitta, ili watoe tamko kuhusiana na suala hilo ambalo alisema limekuwa likisababisha lawama kwa muda mrefu.
``Kuna Waraka wa Rais unaokataza wabunge kuwa wajumbe wa bodi za mashirika ya umma lakini inashangaza hautekelezwi.
Hata hivyo, sasa kamati yangu itawataka mawaziri walifanyie kazi hili mara moja,`` alisema Bw. Kabwe ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA).
Alisema hata katika hoja yake binafsi atazungumzia umuhimu wa wabunge kutokuwepo kwenye bodi hizo.
Kwa upande wake, Bw. Utouh, alisema kati ya mashirika na taasisi 91 zilizokaguliwa, 80 zilipata hati zinazoridhisha, 10 zilipata hati zenye shaka na shirika moja lilipata hati mbaya.
Alisema mashirika manne ambayo ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Shirika la Posta Tanzania, Bodi ya Biashara ya Nje na STAMICO, hayakuwasilisha kwa wakala husika makato ya kisheria yanayofikia Sh. bilioni 29.3.
Alisema hali hiyo inaweza kusababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi wanaohusika wakati wa kudai mafao yao wanapostaafu.
Alisema maagizo ya Rais Jakaya Kikwete, yamesaidia kuboreshwa kwa hesabu na utunzaji wa kumbukumbu katika sehemu nyingi.
Alitoa mfano kuwa halmashauri nyingi mwaka huu zimepata hati zinazoridhisha kulinganisha na mwaka jana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), Bw. John Cheyo, alipendekeza muswada wa kuipa nguvu Ofisi ya CAG uwasilishwe bungeni ili iweze kufanyakazi zake kwa ufanisi zaidi.
Alisema walishawahi kutoa pendekezo hilo muda mrefu lakini inashangaza halifanyiwi kazi.
``Huwezi kwenda kumkagua mtu halafu ukamwomba akupe nyenzo za kufanyia kazi, hiyo haiingii akilini hata kidogo,`` alisema Bw. Cheyo, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Mashariki.
Alisema Kamati yake ilikuwa ikiisubiri ripoti hiyo kwa hamu ili iweze kuifanyia kazi.
Ofisi ya CAG iliwasilisha bungeni jana Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na ile ya Ukaguzi wa Serikali Kuu.
SOURCE: Nipashe