Wabunge wapambanaji wa ufisadi wajibu mapigo

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
WASEMA RAIS KIKWETE ATABEBA MSALABA WA RICHMOND


Sadick Mtulya

WABUNGE wanaojipambanua kwa kupambana na vitendo vya ufisadi nchini, wamesema hawajashindwa vita ya ufisadi , hawaogopi mtu na kwamba, utekelezaji wa maazimio ya kashfa ya Richmond sasa yapo mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, akishindwa atakumbana na hukumu ya wananchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, baadhi ya vinara hao wa vita dhidi ya ufisadi, walisema kufungwa kwa mjadala wa kashfa ya Richmond bungeni haimaanishi kwamba wameshindwa.

Walisema wataendelea kupambana na ufisadi na kusisitiza kuwa kilichobaki ni serikali kutekeleza maazimio ya bunge yaliyosalia kuhusiana na kashfa hiyo.

Walibainisha kuwa maazimio yote ya bunge kuhusu kashfa hiyo yalitekelezwa, isipokuwa mambo matatu ambayo walisema yako mikononi mwa Rais Kikwete, kwa ajili ya kuchukua hatua na kwamba, akishindwa watamshtaki kwa wananchi.

Wabunge hao walidai kuwa kufungwa kwa Richmond bungeni si mwisho wa mapambano ya ufisadi na kwamba, sakata hilo bado halijaisha badala yake limehamishiwa serikalini.

Hata hivyo, wamewataka wananchi nao kuchukua jukumu la kumshinikiza Rais Kikwete kuchukua hatua katika maazimio matatu yaliyobaki ikiwemo kuwawajibisha maofisa wa juu serikalini waliodaiwa kuhusika kwa njia moja au nyingine kubariki na kuitetea zabuni ya uzalishaji wa umeme wa dharura iliyotolewa katika mazingira tata kwa kampuni ya Richmond ambao bado hawajachukuliwa hatua, akiwemo Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hoseah.

“Nasema Bunge kufunga mjadala si mwisho wa mapambano ya ufisadi nchini," alisema Mbunge wa Kishapu Fred Mpendazoe na kuongeza: "Richmond ilikuwa ni moja ya kielelezo cha baadhi ya vitendo vya ufisadi vilivyofanyika nchini, ninaungana na Spika Sitta; mapambano bado yanaendelea. Tutapigana hadi hatua ya mwisho".

Mpendazoe alisema pamoja na watu kusema upo uhasama baina yao na kundi la wanaopinga uwepo wa ufisadi, imani yake inabaki kama ilivyokuwa awali na kusisitiza kuwa ataendelea kukemea ufisadi, rushwa na kama hilo ndilo litakuwa ni tatizo kwa CCM, basi atakuwa tayari kwa hukumu yoyote.

"Ninakemea ufisadi kwa maslahi ya wananchi hivyo ni lazima tuwe wakali zaidi na kama hilo litakuwa ni tatizo kwa CCM, basi nipo tayari kwa hukumu yoyote,” alisema.

Mpendazoe alifafanua kwamba, Bunge lilishindwa kumuwajibisha Dk Hoseah kutokana na Mkurungezi huyo wa Takukuru kuingiza hoja ya uchunguzi wa posho mbili kwa wabunge.

"Kutokana na hoja hiyo, wabunge waliona kuwa haitokuwa busara kwa Bunge kumuwajibisha Dk Hoseah ili isionekane kama tumelipiza kisasi. Ndiyo maana tumeitaka serikali iwajibike kwa kuwa ina uwezo huo," alisema Mpendazoe.

Naye Mbunge wa Kahama, James Lembeli pamoja na mambo mengine aliwataka wananchi kujitokeza hadharani ili kumshinikiza Rais Kikwete achukue hatua za kuwawajibisha watendaji wa serikali pamoja na Dk Hoseah.

"Wabunge wanaopambana na ufisadi hawazidi 15, wakati wanaojihusisha na masuala hayo wapo wengi hivyo kulilaumu Bunge itakuwa si jambo la busara.

Ili kudhihirisha kuwa wananchi na wanaharakati wanachukia vitendo vya ufisadi sasa wajitokeze hadharani kuishinikiza serikali ichukue hatua katika maazimio matatu ya Bunge yaliyobaki," alisema Lembeli.

Lembeli alisema katika maazimo 23 yaliofikiwa na Bunge ni maazimo matatu tu ndiyo bado hayajatekelezwa.

"Bunge limefanya kazi yake lakini ni maazimo matatu tu likiwemo lile la kumuwajibisha Dk Hoseah, pamoja na baadhi ya watendaji wa serikali ambao wengine wemekwishastaafu," alisema Lembeli.

Lembeli alisema hawezi kubadili msimamo wa mapambano dhidi ya ufisadi.

"Msimamo wangu bado ni ule ule, ninapinga ufisadi kwa nguvu zote. Kwa hili la ufisadi nipo tayari kuwajibishwa na CCM," alisema.

Naye Mbunge wa Nzega Lucas Selelii alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ufisadi bado yanaendelea na kamwe hawezi kuchoka.

"Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi, tumekwisha ianza kazi ya kupambana na ufisadi kwa ufanisi mkubwa.

"Sisi kwa upande wetu hatuwezi kuchoka, kazi za kupambana na ufisadi zipo nyingi na si tu hii ya Richmond; mapambano yataendelea," alisema Selelii.

Naye Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro alisema Bunge kufunga mjadala wa Richmond sio mwisho wa mapambano ya ufisadi.

"Kuna kundi la watu wachache ndio wanaeneza uvumi huu, lakini ninakuhakikishia mapambano ya ufisadi yapo pale pale na tutaendelea kupambana hadi pumzi ya mwisho ya uhai. Ufisadi sio Richmond pekee, hata katika shughuli za kimaendeleo ufisadi upo,"alisema Kimaro.

Kauli za wabunge hao zimeonekana kumuunga mkono Spika Sitta ambaye Alhamisi iliyopita alinukuliwa akisema yupo tayari kuhukumiwa na CCM, iwapo msimamo wake wa kupinga ufisadi, utaonekana ni tatizo.

Sitta pamoja na baadhi ya wabunge waliojipambanua kama wapambanaji wa ufisadi amekuwa akitajwa na baadhi ya vyombo vya habari waziwazi kuwa na uhasama na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz huku ikielezwa kuwa chanzo cha uhasama huo ni kashfa ya Richmond.

Kashfa ya Richmond ndiyo iliyomfanya Lowassa na mawaziri wengine wawili, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha, kujiuzulu.

Uhasama ulisababisha CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kuunda kamati maalumu ya watu watatu kutafuta chanzo na suluhu ya mgogoro huo.
Kamati hiyo inaongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na wajumbe wake ni Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Pius Msekwa.
 
Hiyo kamati ya Mwinyi nayo ni usanii mtupu, tatizo linafahamika chanzo chake sasa hiyo kamati inachunguza nini. Ni sawa na kuuliza kinyeo cha mbwa wakati mkia unauona!!
 
Hiyo kamati ya Mwinyi nayo ni usanii mtupu, tatizo linafahamika chanzo chake sasa hiyo kamati inachunguza nini. Ni sawa na kuuliza kinyeo cha mbwa wakati mkia unauona!!

Mwinyi gani ni yule yule aliyeuza Loriondo? ailaani richmond????
kaazi kweli kweli.

damn them!!!!!!!
 
Wapinzani wanatakiwa wajaribu kuwakumbatia hawa wapambanaji toka CCM na kufanya nao kazi badala ya kulifanya hili ni jambo kama ni lao upinzani peke yao na hivyo kukosa nafasi ya kuvutia wananchi ili kumkabili JK.
 
Huu ni wakati muafaka kwa DR.Slaa na chama cha Chadema kuirudisha ajenda ya ufisadi chamani kwao kwani ilitekwa na CCM!! Sasa ndio wakati mzuri wa chadema kuuanika ufisadi wa CCM hadharani ili wananchi waelewe kuwa adui wa maendeleo yao ni mafisadi na chama chao na ndio maana wameuzima mjadala wa Richmond bungeni kiaina aina.
 
Wapinzani wanatakiwa wajaribu kuwakumbatia hawa wapambanaji toka CCM na kufanya nao kazi badala ya kulifanya hili ni jambo kama ni lao upinzani peke yao na hivyo kukosa nafasi ya kuvutia wananchi ili kumkabili JK.
Hakuna hata mmoja wapiganaji ndani ya CCM ila yalikuwa ni majungu tu na baada ya kusoma alama za nyakati ndio katika kipindi hicho waligeuka na kuanza kuimba mwimbo wa UFISADI kama ndio hivyo yangekuwa vile vile Dodoma, ila wamegeuka na sasa wanaimba mwimbo tofauti kabisa
 
Back
Top Bottom