Wabunge wameanza kutuzimia simu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
ILE tabia ama tunaweza kuiita kuwa ni hulka iliyozoeleka kila baada ya uchaguzi mkuu unapokaribia na wakati wa mchakato mzima wa kampeni haishangazi kuwaona wagombea wakijisahau na kutoa shikamoo za bure kwa watoto wadogo na kwa kila mtu bila kuona aibu.
Wagombea wetu kipindi hicho hujishusha na kujifanya wanyenyekevu wa hali ya juu kwa wananchi wanaowaomba kura, hawajali rika, umri au umaskini wa mtu kwa wakati huo, kila mmoja hujivika unyonge wa hali ya juu kwa lengo la kuomba kuchaguliwa.

Mbinu mbalimbali za kuwavuta wapiga kura huonekana kipindi hicho huku kukiwa na ahadi lukuki zinazotolewa ili kuushawishi umma ujue kuwa wakombozi wanaohitajika wamefika na hakuna ubishi kuwa ujuzi na propaganda nyingi hufinyangwa wakati huo.

Wapo waliokuwa wakipiga magoti kwenye majukwaa, wengine wakiomba kura huku wakitoa machozi kwa maana ya kuwaonea huruma Watanzania na umaskini wao, wanaongea mambo mazuri ya faraja kwa ahadi kuwa wakipewa madaraka tu shida zote zitakwisha.

Maskini Watanzania hawa kwa kuwa ni watu watii, wanyenyekevu nao huanza kulia machozi eti wanashukuru kumpata kiongozi aliyepiga magoti kuomba kura na yule anayelia kwa uchungu jukwaani akiwalilia, watoto yatima, wanawake wajane, walemavu na wale wasiojiweza.

Analia kweli na machozi yanatoka mengi kuliko alivyoweza kulia wakati wa msiba wa mama yake mzazi, anatamka maneno ya uchungu kupinga ukatili na mauaji wanayofanyiwa walemavu wa ngozi (albino), wananchi wanatikisa vichwa, wanatamka kwa imani kuwa huyo ndiye kiongozi.

Wanawasifia viongozi wa namna hiyo na namna wanavyopiga magoti na kutoa shikamoo kwa kila mtu, hawaangalii huyu ni mzee au kijana na hawapimi idadi ya kutoa shikamoo mtu mmoja anaweza kupewa shikamoo tatu kutwa, asubuhi, mchana na jioni ni shikamoo, shikamoo, shikamoo.

Hapo ndipo nilipoanza kushikwa na hofu na kujiuliza hivi hizi shikamoo zilizokuwa zikitolewa na waheshimiwa hawa kweli zilikuwa zikitoka moyoni au mdomoni na kweli hata hayo magoti na machozi waliyokuwa wakiyatoa kila siku yalikuwa yanatoka moyoni au machoni, nilijiuliza sana.

Baada ya mchakato mzima wa kampeni kumalizika na siku ya kupiga kura ilipowadia watu wengi walivutiwa na zile tabia ama vitendo vya ulaghai vilivyokuwa vikionyeshwa na wagombea wetu kila mmoja kwa mtindo wake, watu walipiga kura na matokeo yakatangazwa.

Matokeo yalipotangazwa kila mmoja aliweza kushuhudia jinsi washindi hao walivyoweza kubebwa juu juu, sasa walikuwa hawalii tena machozi ya uchungu kama awali wengine walikuwa wakilia machozi ya furaha na sasa walipiga magoti ya kweli kumshukuru Mungu kwa ushindi huo na kutamka bayana kuwa Mungu mkubwa.

Mungu hapo alichukua nafasi kubwa kwenye vinywa vyao lakini mwanzo alikuwa hatajwi, waliokuwa wakinyenyekewa muda wote walikuwa wananchi ambao kimsingi ndio waliokuwa na dhamana kubwa ya kupiga kura, ghafla wamegeuza migongo yao na kuanza kuwabeba wagombea waliokuwa wakitoa shikamoo mara tatu kwa siku.

Siku ya pili baada ya matokeo kutangazwa na shamrashamra zote kukesha usiku mzima, siku iliyofuata waheshimiwa hao walizima simu zao huku ndugu zao wa karibu wakitoa majibu ya mkato: “Mheshimiwa amechoka anapumzika hawezi kuongea na mtu yeyote, jaribu kesho mchana.”

Kwa nini iwe hivyo, mbona ni jana tu mheshimiwa huyo alikuwa na nguvu zote, mbona nyie mliomchagua kwa kura nyingi na kukesha naye usiku na mchana hamjazima simu zenu wala hamjaenda kulala kwa ajili ya uchovu, sasa iweje huyu mheshimiwa aanze kuchoka kabla ya kazi aliyoiomba?

Hapo ndipo maswali na hoja ya mjadala wangu unapoanzia na hapo ndipo ugumu wa kuwapata waheshimiwa hao unapoanzia, eti walikwenda Dodoma wakala kiapo, Rais akazindua Bunge na baada ya muda mfupi, Rais akawateua wengine kuwa Mawaziri na Naibu Mawaziri hivyo ni vigumu sasa kuonana nao wana kazi nyingi mno hebu wangojeni tena hadi mwaka 2015 ndipo watakaporudi.

Hicho nilikiona kizungu mkuti kumbe zile shikamoo zilizokuwa zikitolewa hovyo hovyo sasa zimegeuka shubiri kwa wapiga kura, sasa imekuwa zamu yenu kuwaamkia waheshimiwa hawa eti shikamoo mheshimiwa, sasa wananchi wameanza kuwapigia magoti waheshimiwa hao waliokuwa wanyenyekevu awali.

Ndipo hapo unapoanza kuonekana ufa mkubwa kati ya wapiga kura na waheshimiwa hawa, hawakamatiki tena, hawapokei tena simu za vijana na wazee waliokuwa wakiwaheshimu kupita kiasi wakati wa kuomba kura na waliporudi na magari yao tinted (vioo vya giza), wanajifanya hawawaoni watu waliogeuza migongo yao kuwabeba.

Tangu siku ya kwanza ya kuapishwa kwao na ndio siku hiyohiyo walipofuta machozi, hawawaliliii tena yatima na wanawake wajane, hawawalilii walemavu na wale wanaoishi kwa umaskini mkubwa, wamesahau yale waliyokuwa wakiyasema majukwaani wakati wa kampeni.

Wamesahau kabisa kuwa machozi waliyokuwa wakiyatoa kupinga ukatili na mauaji ya albino, sasa wamewageuka na hawazungumzii tena suala hilo na majibu yanayotolewa sasa ni yale yanayokatisha tamaa kupita kiasi, zile ahadi na propaganda zilizowachemsha watu hazina nafasi tena, sasa mabwana hawa ni waheshimiwa wanaamkiwa.

Awali ahadi zao zililenga utendaji na ufuatiliaji wa masuala muhimu na kero walizonazo wananchi, ukiuliza kuhusu watoto yatima na wajane utajibiwa kuwa yeye sio Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii hivyo ni vyema kero hizo zimsubiri waziri mwenye dhamana atazijibu wakati wa ziara zake.

Hata jibu la kupewa uhakika wa kupambana na mauaji ya albino utamsikia mheshimiwa akijibu hilo ni suala la polisi na mahakama, siwezi kuingilia kesi zilizopo mahakamani huku akiwaomba na kuwasihi wananchi wasimuulize maswali ambayo yapo nje ya uwezo wake, yupo kwa ajili ya kusikiliza kero lakini sio hizo.

Ndipo hapo inapokuja hoja iweje waheshimiwa hawa wawe watu wa kutoa ahadi tele bila mipaka, wakilia na kupiga magoti bila kujua kuwa huko mbele waendako hawana uwezo wa kutekeleza ahadi zote walizokuwa wakizitoa, wanacheka sasa kwa kuwa walikuwa wakizitoa kwa watu wajinga ambao hawakuwa na uwezo wa kupambanua mambo.

Na kwa ujinga huohuo bila kujua athari za kudanganywa wananchi wengi hawajui kuwa propaganda nyingi za siasa ni uongo na sasa mmegeuka wanyonge na wanyenyekevu, wenye utii wa woga, msioweza kuhoji mapema ahadi hizo, mnarudisha mikono nyuma mkiwaamkia waheshimiwa shikamoo.

Wananchi mnapaswa kujivunia dhamana kubwa mliyonayo ya kuwapata viongozi wenu na hakuna haja ya kusubiri muda, mliwachagua na kuwapa majukumu ya kufanya, msigeuke watumwa kwa watu mliowapa uongozi, msianze kulia wakati kisu mlichonacho mmeshika kwenye mpini hakitawakata.

Mwanzo wa ushindi ndio mwanzo wa uchaguzi mwingine unaofuata, miaka mitano sio mingi hakuna muda wa kuteteleka, viongozi hawa walioanza kuzima simu mapema mjue kuwa ndio hao hao mnaopaswa kuanza kuwapunguzia kura mapema.

Kwa kuwa unyonge unahesabiwa kwa umaskini mlionao, msithubutu kuuza utu wenu, uhuru na haki ya kutoa maoni kwa kumuogopa mtu mliyempa uongozi kwa ridhaa yenu, vinginevyo shikamoo hizi hazitaweza kuleta mapinduzi ya uchumi isipokuwa zitaendeleza umaskini na unyonge wa fikra, zindukeni sasa.
 

Nonda

JF-Expert Member
Nov 30, 2010
13,372
2,000
Mkuu,

Walikuja kwenu kuomba "kula" na muliewapa sasa ni lazima wameanza kuvimbiwa, usubirie harufu mbaya tu ( ya u.shuzi, mja.mbisho). Ndio malipo hayo mkuu! Aliyeshiba hamjui mwenye njaa! Watarudi baada ya miaka 5, wasubiri hapo hapo ulipo, watarudi..
 

Lizzy

JF-Expert Member
May 25, 2009
24,912
2,000
Wameshapata walichokitaka...hawana cha kunyenyekea tena mpaka uchaguzi ujaoo!
 

pori

Member
Mar 12, 2010
86
0
jamani, wabunge kunyenyekewa ili wachaguliwe ni sahihi. kwani mngekua nyie msingefanya hivyo? mnajua, pengine wanazima simu kutokana na demands nyingi toka kwa wapiga kura ambazo si rahisi kwa mbunge kutekeleza. mkimchagua mbunge mnataka awatimizie matakwa mengi binafsi kama kulipia ada za watoto wenu, kukulipieni kodi za nyumba, na pengine hata kukujengeeni nyumba! kazanieni maendeleo ya jumuia!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom