Wabunge waipa NHC siku saba kubana wadaiwa sugu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,298
33,083
james%20lembali.jpg

Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli,

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, imetoa siku saba kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuzibana wizara tano za serikali pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ambao ni wadaiwa sugu wa kodi za upangaji wa majengo yake, zieleze lini zitalipa madeni yao yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 2.1.


Wakati agizo hilo likitolewa, mtu mmoja anadaiwa kumilikishwa eneo katikati ya ua wa nyumba za NHC, jijini Dar es Salaam katika mazingira ya kustaajabisha.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, alitoa agizo hilo wakati kamati yake ilipotembelea makao makuu ya NHC, jijini Dar es Salaam.


Alisema majibu ya wadaiwa hao yawe yamepatikana kabla ya hotuba ya Bajeti Kuu mpya ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 haijasomwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa katika mwaka huo wa fedha.


Lembeli alisema kwa mujibu wa kumbukumbu za NHC, mdaiwa mkubwa ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambayo inadaiwa zaidi ya Sh. milioni 734 zikiwa ni malimbikizo ya miezi 57.


Alisema wadaiwa wengine sugu ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inayodaiwa zaidi ya Sh. milioni 439 ambazo ni malimbikizo ya miezi 17; na Wizara ya Uchukuzi inayodaiwa Sh. milioni 240 zikiwa ni malimbikizo ya miezi minne.


Nyingine ni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (Sh. milioni 239 malimbikizo ya miezi 10); Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) (Sh. milioni 310 malimbikizo ya miezi 74 na JWTZ inayodaiwa Sh. milioni 182 zikiwa ni malimbikizo ya miezi 42.


Lembeli alisema inasikitisha kuona wizara hizo zikidaiwa kiasi hicho cha fedha katika vipindi hivyo wakati zilikuwa zinapata bajeti kila mwaka, huku serikali ikiihimiza NHC kujenga nyumba za wananchi.


"Naona hili jambo ni aibu kwa serikali. Mtoto wako anakudai halafu unazunguka unamwambia ajenge nyumba za wananchi. Tatizo serikali ndiyo inayoua mashirika yake," alisema Lembeli.


Kutokana na hali hiyo, aliitaka NHC kuhakikisha inazibana wizara hizo kulipa malimbikizo ya madeni yao yote ili kuiwezesha kujiendesha, vinginevyo shirika hilo litakufa kama ilivyotokea kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).


"Ndani ya siku saba tupate majibu lini wizara hizi watalipa haya madeni. Ni jambo la kusikitisha unamziba mtoto wako pumzi.Ni ufisadi mwingine huu.


Machinga anakamatwa barabarani akiuza vitumbua, wenyewe wanadaiwa," alisema Lembeli na kuongeza:


"Mheshimiwa Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wizara yake ndiye mdaiwa mkubwa, tutaonana naye bungeni na asipolipa tutajua la kufanya."


Alisema wakati wa operesheni ya NHC ya mwaka huu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, vitu vyao vilitolewa nje kutokana na kudaiwa na kuhoji: "Walirudije?"


Kutokana na hilo, aliitaka NHC kuhakikisha wapangaji wake wote, zikiwamo wizara na taasisi za serikali wasiolipa watolewe katika nyumba walizopanga kama wanavyofanyiwa wapangaji wengine wa kawaida.


Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu, alithibitisha serikali kuwa ni mdaiwa sugu kupitia wizara zake hizo ambapo alisema madeni hayo ni asilimia 70 ya madeni yote ambayo NHC inawadai wateja wake.


Lembeli alisema watu hao hawataki nyumba hizo, bali wanachokitaka ni viwanja, hivyo akawataka wasubiri nyumba 15,000 zinazojengwa na NHC ili wakaombe kama watu wengine.


"Hivi ukipanga kwenye nyumba ya mtu binafsi miaka 30, utakwenda mahakamani kudai uuziwe? Msimamo wetu zile nyumba zisiuzwe," alisema Lembeli.


Awali, Mchechu aliieleza kamati hiyo kuwa kuna mtu aliyemtaja kwa jina moja la Ladwa, kwamba amemilikishwa eneo lililo katikati ya ua wa nyumba za NHC, eneo la Temeke, Chang'ombe, jijini Dar es Salaam.


Alisema walibaini hilo baada ya kuweka uzio, ambapo alijitokeza mtu huyo na kudai kuwa eneo hilo amemilikishwa yeye.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom