Wabunge wa CHADEMA wameboronga au wamelonga?

Bhbm

JF-Expert Member
Oct 31, 2009
715
208
WANASHERIA wote walio na maarifa timamu hapa Tanzania na duniani kwa ujumla wanakubaliana angalau katika jambo moja muhimu kuhusu uendeshaji wa nchi.
Jambo hilo ni kwamba agizo kutoka mamlaka iliyo katika ngazi ya chini kuhusu utekelezaji wa jambo fulani linaweza na linapaswa kususiwa endapo agizo hilo linapingana au kusigana na agizo jingine kutoka mamlaka iliyo katika ngazi ya juu kuhusu utekelezaji wa jambo hilo hilo.
Hii ndio sababu agizo la Mwenyekiti wa Kijiji (mamlaka iliyo katika ngazi ya chini) hutenguliwa na Katibu Kata (mamlaka iliyo katika ngazi ya juu); agizo la Katibu Kata (mamlaka iliyo katika ngazi ya chini) likatenguliwa na Mkuu wa Wilaya (mamlaka iliyo katika ngazi ya juu); agizo la Mkuu wa Wilaya (mamlaka iliyo katika ngazi ya chini) likatenguliwa na Mkuu wa Mkoa (mamlaka iliyo katika ngazi ya juu); na agizo la Mkuu wa Mkoa (mamlaka iliyo katika ngazi ya chini) likatenguliwa na Mkuu wa Nchi (mamlaka iliyo katika ngazi ya juu).
Hii ndio sababu hukumu ya Mahakama ya Mwanzo hutenguliwa na Mahakama ya Wilaya; hukumu ya Mahakama ya Wilaya ikatenguliwa na Mahakama ya Mkoa; hukumu ya Mahakama ya Mkoa ikatenguliwa na Mahakama Kuu; na hukumu ya Mahakama Kuu ikatenguliwa na Mahakama ya Rufaa.
Aidha, hii ndio sababu Sheria iliyotungwa na Bunge (mamlaka iliyo katika ngazi ya chini) hutamkwa kwamba ni batili pale inapokuwa inapingana au kusigana na kifungu chochote kilicho katika Katiba ya nchi (mamlaka iliyo katika ngazi ya juu). Na hii ndio sababu ibara ya 13 kifungu cha 6(a) katika Katiba ya Tanzania (1977) inatamka bayana kwamba, mtu yeyote ambaye hajaridhia uamuzi uliofanywa na chombo chochote cha maamuzi kilicho katika ngazi za chini anayo haki ya kukata rufaa katika ngazi za juu dhidi ya uamuzi huo.
Lakini sio hivyo tu. Pia, hii ndio sababu pekee iliyowafanya watunzi wa Katiba ya Tanzania (1977) waseme kwamba, “Iwapo mgombea [wa kiti cha Rais] ametangazwa na Tume ya Uchaguzi (mamlaka iliyo katika ngazi ya chini) kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake” isipokuwa “Mahakama” ya “dhamiri” za wananchi (mamlaka iliyo katika ngazi ya juu).
Ukweli huu kuhusu “Mahakama” ya “dhamiri” za wananchi, ni kwa mujibu wa maudhui ya Katiba ya Tanzania (1977) katika ibara ya 9(f), ibara ya 19(1), na ibara ya 41(7) kama ikisomwa sambamba na ibara ya 18 ya Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu. Ibara hizi zinatufundisha kwamba “kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa dhamiri…” Neno la msingi hapa ni “dhamiri”.
Na kwa mujibu wa Katiba na sheria zetu hapa Tanzania, “mahakama” ya “dhamiri” za wananchi ndiyo “mahakama” pekee yenye mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwa mgombea wa kiti cha Rais baada ya kuwa ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais.
Wabunge wa CHADEMA waliosusia hotuba ya Jakaya Kikwete majuzi kwa kuondoka ndani ya bunge pale Dodoma waliamua kupeleka manung’uniko yao ya haki dhidi ya Tume ya Uchaguzi kwenye “mahakama” ya “dhamiri” za wananchi. Kukata rufaa kwa njia hii dhidi ya uamuzi wa Tume ya Uchaguzi wa kuyatangaza matokeo ya uchaguzi wa rais isivyo halali, ni haki yao ya kikatiba na hakuna anayeweza kuipokonya.
Nimeyasoma maoni ya Samwel Sitta, Zitto Kabwe, Mabere Marando, Mchungaji William Mwamalenga, Amosi Makalla, Kapteni Mstaafu John Chilligati, Beno Malisa, Dk. Haji Semboja, Dk. Benson Bana, Nathanaeli Mlaki, Ananilea Nkya, na wengine.
Amosi Makalla anasema kwamba wabunge wa CHADEMA wamejidhalilisha kutoka nje ya bunge. Beno Malisa anasema kwamba kitendo cha wabunge wa CHADEMA kinawanyima haki wananchi waliowachagua wabunge hawa. Na Kapteni Mstaafu John Chilligati anasema kwamba wabunge wa CHADEMA wasipobadili msimamo wao wataondolewa bungeni kwa kwa azimio la bunge mpaka hapo watakapokubali kubadilika kwa lazima.
Kauli za aina hii zinaonyesha bayana jambo moja: ugonjwa wa maarifa haba kuhusu umantiki wa “mahakama” ya “dhamiri” za wananchi. Na dawa ya ugonjwa wa maarifa haba ni elimu. Kwa hiyo, kupitia makala hii nimelazimika kutoa elimu ya uraia kwa njia ya gazeti kwenda kwa watu wote wanaosumbuliwa na ugonjwa wa maarifa haba kama ilivyo kwa Amosi Makalla, Beno Malisa na Kapteni Mstaafu John Chilligati.
Kusema kwamba “kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, kama ilivyoandikwa katika Katiba ya Tanzania (1977) ibara ya 12 kifungu cha 2, ni kutamka kwamba kila mtu anao wajibu wa kuukubali ukweli ufuatao:
Kwamba, binadamu wote, kwa maana ya wanyama walio na hazina ya uwezo wa kufanya mang’amuzi, hazina ya uwezo wa kufikiri, na hazina ya uwezo wa kufanya maamuzi yaliyo na msingi wake katika utashi huru, wanayo hadhi sawa (all human persons, as embodied individuals having congenital capacity for conscious, autonomous and rational actions, are equal in dignity).
Kuukubali ukweli huu ni kukubali kanuni kwamba ukitaka kushirikiana na binadamu yeyote mwenye akili timmau lazima ufanye hatua za makusudi za kuhakikisha kwamba binadamu huyo anatoa ridhaa huria na yenye kuzingatia taarifa sahihi (free and informed consent) kwa ajili ya kufanikisha ushirikiano huo. Kutoa ridhaa ni kusema ndio kuhusu pendekezo la kutekelezwa kwa jambo fulani, ambapo utekelezaji unaweza kumhusisha aliyesema ndio au mtu mwingine.
Na kimsingi, ridhaa huria na yenye kuzingatia taarifa sahihi inawezekana pale tu ambapo masharti manne muhimu yatatimizwa. Sharti la kwanza, mtu anayetarajiwa kutoa ridhaa lazima awe mtu mzima mwenye akili timamu (capacity to consent).
Sharti la pili, mtu anayetarajiwa kutoa ridhaa lazima apewe taarifa sahihi na kamilifu kuhusu pendekezo linalokusudiwa kutekelezwa (disclosure of relevant information). Taarifa hizi zitamwezesha kujiridhisha kwamba ridhaa yake haitakuwa na madhara ama kwa upande wake au kwa wadau wengine.
Sharti la tatu, lazima kuhakikisha kwamba mtu anayetarajiwa kutoa ridhaa ameelewa taarifa anazopewa (comprehension). Kwa mfano, kama ni taarifa zimepangiliwa kitaalamu lazima aliyezipanga atoe ufafanuzi kuhusu mpagilio alioutumia. Na sharti la nne, lazima kuhakikisha kwamba mtu anayetarajiwa kutoa ridhaa anafanya uamuzi huo kwa hiari yake mwenyewe (voluntary decision).
Masharti haya manne yanapozingatiwa, basi kile kifungu cha katiba kinachosema kwamba “kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, huwa kimezingatiwa. Nje ya hapo, ibara ya 12(2) ya Katiba ya Tanzania (1977) inakuwa imevunjwa.
Na kitendo hiki cha kuvunja Katiba ya Tanzania ndicho alichofanya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi pale alipoandikiwa barua na mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA lakini akakataa kuchukua hatua mwafaka.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Lewis Makame alipaswa kufahamu kwamba mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Wilibrod Slaa, kwa kuandika barua ya malalamiko, alitaka Tume impe fursa ya kutoa ridhaa huria na inayozingatia taarifa sahihi kuhusu pendekezo la kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Lewis Makame alipaswa kufahamu kwamba Dk. Wilibrod Slaa ni mtu mzima mwenye akili timamu; kwamba, Dk. Wilibrod Slaa alistahili apewe taarifa sahihi na kamilifu kuhusu pendekezo lililokuwa linakusudiwa kutekelezwa na Tume; kwamba Tume ilikuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba Dk. Wilibrod Slaa ameelewa taarifa ambazo angepewa; na kwamba, Tume ilikuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba Dk. Wilibrod Slaa anafanya uamuzi wa kuyakubali matokeo kwa hiari yake mwenyewe.
Kwa kuzingatia kilichotokea tunalazimika kuamini kwamba ama Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi hakuyafahamu haya au aliyafahamu lakini akayapuuzia. Kwa kuyapuuzia alivunja Katiba ya nchi ibara ya 12(2).
Na sasa, kina Chiligati wanaosema kwamba wataandaa azimio la bunge ili “kuwalazimisha” wabunge wa CHADEMA kukubali matokeo wanaungana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi katika kuvunja Katiba ya nchi. Mtu yeyote anayevunja Katiba ya nchi kwa makusudi ni mtu wa kuogopwa kama ukoma. Kina Chiligati wanakusudia kuvunja Katiba ya nchi kwa makusudi. Hivyo, napendekeza kwamba hawa ni watu wa kuogopwa kama ukoma.
Baada ya kusema hayo, nimkubushe tena msomaji wa makala hii kwamba Katiba ya Tanzania inasema kwamba: “Iwapo mgombea [wa kiti cha Rais] ametangazwa na Tume ya Uchaguzi (mamlaka iliyo katika ngazi ya chini) kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake” isipokuwa “Mahakama” ya “dhamiri” za wananchi (mamlaka iliyo katika ngazi ya juu).
Kwa hiyo, nawahimiza wabunge wa CHADEMA, viongozi wa CHADEMA, wanachama wa CHADEMA, na wapenzi wa CHADEMA kuhakikisha kwamba “Mahakama” ya “dhamiri” za wananchi inatumiwa kikamilifu tangu sasa ili kwamba hatimaye hakimu aitwaye “umma” atekeleze majukumu yake ipasavyo.
Tunapinga Katiba inayotoa haki ya kukata rufaa kupitia mkono wa kushoto (ibara ya 136(a)) na kisha katiba hiyo hiyo ikaipora haki hiyo kupitia mkono wa kulia (ibara ya 41(7)). Tunaikataa Katiba inayosema kwamba mtu yeyote anaweza kutangazwa rais wa Tanzania hata kama amepata kura ambazo ni sawa na asilimia tano ya wapiga kura wote (ibara ya 41(6)).
Tunaichukia katiba ya nchi ambayo haitamki mahali popote nani ambaye ni raia wa Tanzania na yupi ambaye ni mlowezi. Na tunaishangaa Katiba ya nchi inayosema kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Kata lazima wawe ni wateule wa Mwenyekiti wa chama tawala.
Hivyo basi, wakati wa kuhakikisha kwamba “Mahakama” ya “dhamiri” za wananchi inatumiwa kikamilifu kuijenga Tanzania mpya ni sasa. Ni lazima mbinu zote za shinikizo la amani ambazo zimewahi kugunduliwa tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu zifukuliwe na kuwekwa katika vitendo kuanzia majuzi wabunge wa CHADEMA walipoisusia hotuba ya Jakaya Kikwete. Hakuna kulala mpaka kieleweke! SOURCE; RAIA MWEMA.
hs3.gif
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom