Wabunge roho juu Dodoma

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Wabunge roho juu Dodoma

na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima

HALI ya mambo katika Manispaa ya Dodoma ni tete, baada ya taarifa kadhaa za kushtua kusambazwa miongoni mwa wabunge kuhusiana na mkataba wenye utata wa kuzalisha umeme kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na Kampuni binafsi ya Richmond.

Uchunguzi wa Tanzania Daima uliofanywa kwa siku nzima jana unaonyesha kwamba, kumekuwa na maneno mengi ya chinichini kuhusu nini hasa kitatokea leo, baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Kuchunguza Mkataba wa Richmond kusomwa bungeni na kisha kusambazwa kwa kila mbunge.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge na Serikali kilichokaa jana zinaeleza kwamba, tayari makubaliano ya suala hilo tete kujadiliwa bungeni wakati wowote kuanzia kesho yameshafikiwa.

Habari zaidi kutoka miongoni mwa wabunge, hususan wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaeleza kwamba, baadhi ya viongozi wamekuwa katika hali ya shauku kubwa kutaka kujua kile kilichogunduliwa na kamati hiyo ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

"Kamati ya Uongozi chini ya uenyekiti wa Spika, imekubaliana na serikali kuwapa wabunge ripoti ya uchunguzi ya Richmond ili waipitie kabla ya kujadiliwa rasmi," kilisema chanzo hicho cha kuaminika jana.

Aidha, kabla ya kujadiliwa kwa taarifa ya kamati hiyo, hoja ya kuchunguzwa kwa mkataba wa Richmond, joto la kulinda masilahi ya taifa na kuwafichua mafisadi limeonekana kupanda miongoni mwa wabunge wengi katika mkutano huu wa 10 wa Bunge.

Hata hivyo, kupanda kwa joto hilo na shauku ya wabunge kutaka kumbaini mhusika mkuu wa Kampuni ya Richmond kumetajwa kuwa sababu iliyomlazimisha Spika Samuel Sitta, kuahirisha ziara yake ya kikazi nchini Marekani iliyokuwa ianze Jumatatu wiki hii.

Aidha, habari nyingine zinaeleza kuwa, Sitta alilazimika kuahirisha safari hiyo kutokana na kutakiwa kufanya hivyo na Rais Jakaya Kikwete ambaye anatarajia kuwasili mjini Dodoma leo.

Chanzo kimoja cha kuaminika kimeieleza Tanzania Daima kwamba Kikwete akiwa Dodoma ataitisha kikao cha Baraza la Mawaziri na anatarajia kuondoka kesho kurejea Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, kuwapo kwa Kikwete hapa Dodoma kumekuwa kukitajwa kuwa na uhusiano na kuwapo kwa uwezekano wa kufanyika kwa mabadiliko katika Baraza la Mawaziri yanayoweza kuigusa pia nafasi ya waziri mkuu.

Kwa mujibu wa Katiba, rais anapofanya mabadiliko ya waziri mkuu analazimika kuwasilisha jina la mteule wake bungeni, ili liweze kuthibitishwa kwa kupigiwa kura na wabunge.

Hata hivyo baadhi ya watu wanaofuatilia masuala ya kisiasa wanayaona mabadiliko haya yanayovumishwa kuwa yasiyoweza kutokea japo kwa wakati huu.

Mbali ya suala hilo la waziri mkuu na Richmond, hoja nyingine inayotarajiwa kujadiliwa na wabunge wengi zaidi ni ile inayohusu wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA).

Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa baadhi ya wabunge ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao zimeeleza kuwa, awali kulikuwa mipango ya kuzuia kujadiliwa kwa mambo hayo, kabla ya shinikizo kubwa kubadili mwelekeo.

Kwa upande mwingine, gazeti hili lilielezwa kuwa baadhi ya viongozi wakubwa serikalini wamekuwa wakihaha kujua kilichomo ndani ya ripoti ya Richmond, iliyoandaliwa na kamati ya Dk. Mwakyembe.

Inadaiwa kuwa uvumi unaosambaa kuwa vigogo hao wametajwa kuhusika kimakosa katika mchakato wa kuipata kampuni hiyo, ndio uliowatia hofu viongozi hao, kiasi cha kubuni mbinu ya kuizima hoja hiyo kujadiliwa hadharani.

Lakini suala hilo linazidi kuchukua sura mpya kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa baadhi ya wabunge ndani ya CCM hawaridhishwi na baadhi ya masuala yanavyoendeshwa.

Inadaiwa kuwa kundi hilo linajumuisha wabunge ambao walibaguliwa kwa kutopatiwa fedha zinazodaiwa kuchotwa kutoka BoT, ambazo zinadaiwa kuingizwa kwenye mchakato wa kampeni za CCM.

Msukumo pia unatoka kwa baadhi ya wabunge ambao wanaamini kuwa wamepatwa na mikasa mikubwa wakati wa kampeni za uchaguzi ndani ya chama, ambao baadhi yao hivi sasa wana kesi mahakamani.
 
Back
Top Bottom