Wabunge mlijisahau, rudini kwenye mstari

sammosses

JF-Expert Member
Jan 24, 2011
1,685
1,111
Nimestushwa na kauli ya mh Aeshi dhidi ya tuhuma nzito kwa mkuu wa mkoa kumtishia kumshughulikia mbunge huyo hatimaye kushindwa kwenda DSM kwa hofu ya kauli hiyo. Mkuu wa mkoa ni nani ana haki ipi ya kisheria kuwatisha raia mbaya zaidi mwakilishi wa wananchi.

Hapa ndipo tulipofika kama taifa, maisha ya wananchi name wawakilishi wao yapo mashakani lakini serikali na bunge lipo kimya. Sauti hii ya wawakilishi wa wananchi ni sauti ya mwana aliye nyikani akililia msaada ambao hajui wapi pakuupata.

Serikali na bunge vimekumbwa na nini kuruhusu mtu mmoja kuwa gumzo kwa usalama wa wananchi. Anayoyafanya mkuu huyu yana baraka za nani ikiwa si mwenye mamlaka ya uteuzi wala bunge lenye uwezo wa kumnyooshea kidole.

Ikiwa serikali inashindwa kuwajibishwa na chombo chenye mamlaka ya kuisimamia kwa kuwa chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi hakina chombo cha dola,kuna haja kwa wabunge wetu warudi kwenye mahakama yetu ya haki kuishitaki serikali hii.

Serikali yetu ni serikali ya watu itakanayo na watu ambayo mamlaka na madaraka yake yatatoka kwa wananchi,ikiwa serikali imeingiwa na ulevi wa madaraka kwa kufumbia macho walevi wa madaraka,hali ya nchi itapotea kama ambavyo tumeanza kuona viashiria vya ulevi huo.

Rais alianza kwa kauli za kutojaribiwa tukidhani amekosea atajirekebisha,lakini imeonekana hakuna chombo kinachoweza kumrekebisha rais kwa matendo na mwenendo wake wa kiuongozi hali inayo mtengeneza rais mbabe wenye nguvu na madaraka yanayopingana na katiba yetu.

Mamlaka tuliyompa ya kutuongoza yamegeuka shubiri,ndiyo maana hata baadhi ya wabunge wanasema tumechonga kinyago tumekiweka sebuleni sasa kimetugeuka kututisha tuliokichonga. Jeuri ya kutotaka kuingiliwa na kutojaribiwa kumepelekea wakuu wake nao kuwa marais wenye ndimi kali mithili ya moto ndo maana Leo si ajabu ukamsikia mteule wake naye akitema cheche bila kuonywa na chombo chochote kile.

Kamati ya maadili na mamlaka ya bunge ilimwita,kilichofanyika hajajulikana labda kama sijakisikia mpaka wakati naandika mada hii,lakini mamlaka hiyo inawezaje kuwa na nguvu ikiwa wajumbe wake wanatishiwa na kukaa kimya. Iko wapi nidhamu ya kazi ikiwa asimamiwaye anamtisha msimamizi.

Kuna mambo ya ajabu yanayoendelea kila siku ndani ya nchi hali inayoifanya nchi yetu kupoteza dira na mwelekeo kwa kuwa nidhamu ya utumishi wa umma ipo chini ya mtu mmoja na si taasisi,ndiyo maana kila alifanyalo mpendwa wa mkuu hawezi kuwajibishwa kwa kuwa uwajibishwaji ni utashi wa mtu mmoja na siyo taasisi.

Ikiwa wabunge wanatishwa,wananchi wa kawaida watafanywa nini. Kitendo cha wabunge kutishwa na inayosemekana serikali ni tuhuma nzito kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu na misingi ya utawala bora,hali hii haiwezi kuachiwa kama upepo upitao tukasema tupo salama.

Tumefika hapa kwa kuendeleza ushabiki wa kisiasa kiasi cha serikali kujiona iko juu ya sheria kuliko hata sheria yenyewe. Wapinzani walipokuwa wanatwezwa utu wao ngoma hii ilionekana hawahusu upande wa pili,walibweteka na kwa kuwa tabia huzaa mazoea hawakujua kisu kimchinjacho kuku ndicho hicho humchinjia ng'ombe pia.

Ukandamizaji unaofanywa na serikali dhidi ya mhimili mingine ni jeuri ya ushabiki wa kivyama ulifanya wingi wa wabunge wa chama tawala kusahau majukumu yao na kuligeuza bunge makutano ya vikao vya chama. Leo kibao kimegeuka na kisu kugusa mfupa ndiyo wanastuka,huku wakishindwa kujua nani atapewa jukumu la kumfunga paka kengele.

Manatishwa na serikali kuanzia wakuu wa mikoa mpaka mwenyekiti wa chama nanyi kwa nidhamu ya uoga mnaweka majukumu pembeni na kuwa upande wa serikali mkisahau kuwa mpo hapo bungeni kwa maslahi ya mwananchi.

Mchelea mwana kulia hulia yeye,poleni sana wabunge,mmeyataka wenyewe rudini tena someni wajibu wenu muache kulalamika,hatukuwatuma kufanya kazi kwa mazoea,mmepitia ridhaa ya chama kuwawakilisha walio wachagua,kwenda kinyume na malengo tuliyo wachagulia ni kuendeleza dhuluma dhidi ya tuliowachagua
 
Swala la wa bunge ninakuafiki kwa 100% Lakini huyo mwingine ni uongo kwa sababu mamlaka isiyojaribiwa au isiyoelekezwa au isiyolazimishwa ni moja tu. Nayo mamlaka hiyo ni Mungu pekee. Muulize anaijua idadi ya nywele zake? Anaijua siku ya kufa kwake? Anajua kuumwa kwake?Nenda umwambie nimesema hayo basi
 
Uvumilivu una kikomo,serikali ikishindwa kufuata katiba imevunja mkataba na wananchi wake,lakini pia imekiuka kiapo cha uti alichokula kiongozi wa serikali, ni vyema bunge likaitazama katiba kwa jicho la pili na umakini mkubwa ili serikali iliyoingia mkataba kwa kuifuta katiba yetu ilazimishwe kufanywa hivyo kwa mujibu wa sheria vinginevyo wabunge,sisi wapiga kura tunawataka kuiwajibisha serikali kwa ile torauti yenu,vinginevyo achieni ngazi kwa kuwa mmeshindwa kusimamia majukumu yenu kisheria kwa mujibu wa katiba
 
Ukosefu wa Posho umewachanganya sana Wabunge.
Muosha huoshwa,waliopoambiwa kuwa joto ya jiwe likitoka kwa wapinzani litafika kwao,sasa limefika na kisu kimegusa mfupa,wote wataongea lugha ya kibunge na siyo ya kichama
 
Back
Top Bottom