Wabunge Iwajibisheni Serikali Sasa Au Muwajibike Wenyewe

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,136
Leo Mkutano wa 18 wa Bunge unaaza mjini Dodoma ambao pamoja na kujadili na kupitisha miswada kadhaa, pia ripoti za utekelezaji wa maazimo mbalimbali ya Bunge itawasilishwa na serikali.

Mkutano huu ni muhimu kwa maana kwamba ndiyo unaotarajiwa kuhitimisha hoja ambazo zimevuma nchini kwa zaidi ya miaka miwili sasa juu ya mkataba tata wa kufua umeme wa dharura wa megawati 100 ulitolewa kwa kampuni ya Richmond kabla ya kuchukuliwa na mrithi wake, Dowans.

Ni mkataba ambao ulisababisha mtikisiko mkubwa wa kisasa nchini Februari 2008 baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu wadhifa wake kwa kuwajibika kisiasa baada ya kutajwa kuhusika kwenye mkataba huo na kamati teule ya Bunge ya iliyochunguza mchakato wa utoaji wa zabuni hiyo.

Serikali inatarajiwa kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya watumishi wake waliozembea hadi mkataba huo ulioiletea hasara kubwa taifa ukafungwa kati ya Shirika la Umeme nhini (Tanesco) na kampuni hiyo tata, Richmond, Juni 23, 2006.

Mkutano huo pia utapokea ripoti ya utekelezaji wa azimio jingine la Bunge la kuurejesha kwenye mikono ya serikali mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, ambao Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na aliyekuwa Waziri wa Nishari na Madini, Daniel Yona, walijimilikisha katika njia ambazo ziliacha maswali mengi.

Mkutano huu unafanyika wakati joto la kisiasa likiwa linazidi kuopanda siku baada ya siku hasa kutokana na mwaka huu kuwa ni wa uchaguzi. Baada ya mkutano huu, wabunge watakuwa na fursa ya kukutana tena mara mbili, yaani mkutano wa 19 utakaofanyika Aprili na ule wa 20 utakaofanyika Juni kupitisha bajeti ya serikali kabla Bunge kuvunjwa na Rais tayari kwa uchaguzi mkuu wa rais na wabunge.

Hatuna sababu ya kuchochea wabunge wachukue msimamo fulani kuhusu hoja zote hizi, yaani ya Richmond na Kiwira, kwa kuwa tunaamini kwamba ni watu wazima wanajua wajibu wao na kwamba wakati wote wa uwakilishi wao watakuwa wanaongozwa na utetezi wa maslahi ya umma kwa moyo wa dhati.

Hata hivyo, kama serikali ilivyokwisha kusema ndani ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, hakuna hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya watumishi wa serikali kama Bunge lilivyotaka, kwa kile kilichoelezwa kwamba hatua zilizokwisha kuchukuliwa zinatosha.

Lakini la ziada zaidi ni kauli ya serikali kwamba si kila kitu kinachotamkwa na Bunge ni lazima kitekelezwe na serikali kama kilivyo. Serikali kwa njia moja au nyingine imelikaripia Bunge kwa kuliambia kwamba kazi yake ni kuishauri tu! Basi!

Kwa hili tungependa kuikumbusha serikali jambo moja, kwamba katika dunia ya leo serikali inabidi ijifunze kuishi kama nyakati zinavyotaka; uwajibikaji ni tunu muhimu katika kufikia mafanikio yoyote iwe katika sekta binafsi au hata ndani ya serikali.

Mathalan, kama uzembe uliotokea kuhusu mkataba wa Richmond ungekuwa unahusu uzalishaji wa nishati ya umeme kwa ajili kampuni binafsi, hakika sasa hivi kampuni hiyo ingekuwa ni marehemu kwa sababu ingekuwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa kukosa umeme; ingekuwa imeshindwa kuzalisha, ingeshindwa kulipa wafanyakazi na kwa kweli ingekuwa imeshtakiwa na wateja wake kwa kushindwa kuwasilisha kwao nishati muhimu kwa ajili ya uzalishaji.

Kwa maneno mengine hasara ambayo ingesababishwa kwa wateja wake ni kubwa kupita kiasi, kwa kifupi uzembe wa kushindwa kuzalisha nishati hiyo kwa muda uliopangwa ungesukuma wateja wake kwenye umufilisi! Ni hasara kubwa mno!

Sasa kwa kuwa Tanesco ni mali ya umma kwa asilimia 100 na kwa kuwa serikali inataka umma usadikishwe kwamba hasara haikuwapo, basi hata suala la kuwachukuliwa hatua watumishi wake waliozembea halionekani ni la muhimu kwa kuwa umma unataka kusadikishwa kwamba hakuna hasara iliyopatikana kwa kuwa tu eti Richmond haikulipwa fedha yoyote.

Tunajua kuwa makali ya mgawo wa umeme yalikuwa yaliumiza uchumi, tunajua kwamba kuna viwanda vilipunguza kama si kusimamisha kabisa uzalishaji; uchumi wa makampuni na viwanda hivi uliyumba, ajira za watu ziliathirika na mwisho wa yote kodi zao kwa serikali hazikulipwa kadri ilivyotarajiwa.

Kutokuanza kuzalishwa kwa umeme wa dharura kama ilivyopangwa taifa liliathirika kama ilivyo kwa mteja mmoja mmoja wa Tanesco; hili serikali inataka kuona ni jambo la kawaida ndiyo maana inakuwa na ujasiri wa ajabu wa kutetea uzembe na kulibeza Bunge kwamba lenyewe wajibu wake ni wa kuishari tu.

Tunatambua kwamba wabunge wetu ni werevu vya kutosha, wataongozwa na uzalendo wao kwa taifa lao na hivyo wataangalia taarifa hizi za serikali kwa macho ya kizalendo ili kuvunja kabisa utamaduni huu wa kulinda na kulea uzembe wa wazi kama huu uliojitokeza kwenye Richmond. Tunaomba wabunge wakumbuke wanawakilisha wananchi, wasikubali kutishwa!
 
Back
Top Bottom