Luteni
JF-Expert Member
- Jan 9, 2010
- 2,274
- 301
Na Restuta James 10th January 2010
Baadhi ya wabunge ndani ya CCM wamedaiwa kujipanga kwa lengo la kuunda chama chao katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Habari za uhakika ambazo Nipashe Jumapili imezipata, zinaeleza kuwa wabunge hao wako mbioni kujiengua kwenye chama hicho, licha ya juhudi za Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kuunda Kamati ya kuchunguza mahusiano ya wabunge na serikali ili kunusuru mpasuko ndani ya chama .
Kamati hiyo ambayo inaongozwa na Rais mstaafu, alhaj Ali Hassan Mwinyi, ilipewa jukumu na NEC kutafuta dawa ya mpasuko uliopo miongoni mwa wabunge hao jambo ambalo linahatarisha mshikamano miongoni mwa wanachama wa chama hicho tawala.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa bunge na wanachama hao wameazimia kuunda chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, iwapo CCM haitawawajibisha mafisadi wanaoitafuna nchi.
Chanzo cha uhakika kimeliambia gazeti la Nipashe Jumapili kuwa maamuzi mazito ambayo chama kinapaswa kuyachukua ni pamoja na kuwawajibisha viongozi na wanachama waliohusika kwenye ufisadi wa Richmond, Kiwira, Benki Kuu ya Tanzania na katika ufisadi mwingine ulioliingizia taifa hasara.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa sababu kubwa iliyopelekea wanachama wameguke na kuunda chama kipya ni kutokana na CCM kutosimamia kikamilifu Katiba yake jambo linalopelekea kumomonyoka kwa maadili ndani ya chama na Serikali.
"Kwa sasa kutokana na hali ilivyo ndani ya CCM uwezekano wa kumeguka ni mkubwa lakini itategemea sana hatua zitakazochukuliwa na viongozi kutokana na taarifa ya kamati ya Mwinyi na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya ufisadi unaokithiri nchini," alisema mbunge mmoja wa CCM.
Mbunge mwingine wa CCM alisema, "kupasuka kwa CCM na kuundwa chama kingine kutawezesha kuwepo upinzani utakaoleta faida kwa wananchi kwa kuwawezesha kuchagua Serikali mbadala kuliko hali ilivyo sasa."
Alisema ili kuepuka kuundwa kwa chama hicho kipya, uongozi wa juu wa CCM unapaswa kufanya vikao na kuchukua maamuzi magumu.
"Mfano, wale waliotuhumiwa kwa ufisadi na kuchukuliwa hatua kwenye Serikali ya CCM kama Waziri Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, Rostam Aziz, Andrew Chenge na Nazir Karamagi, inabidi wawajibishwe," kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilinukuu Katiba ya CCM toleo la 2007 sehemu ya kwanza kifungo 3, 4, 7 na 14 inayokemea ufisadi nchini.
Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu suala hilo, Mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe alikiri kuwepo kwa mpasuko ndani ya chama hicho na kutabiri uwezekano wa suala hilo kutokea.
Alisema hali ya chama si shwari kuanzia ngazi ya juu hadi shina kutokana na kushamiri kwa rushwa katika chaguzi nyingi, jambo alilosema linazidi kukibomoa chama.
"Na hali hii itaendelea kuleta mpasuko ndani ya chama hasa baada ya kura za maoni, na hivyo upo uwezekano chama kikadhoofika...lakini viongozi wanapokuwa na msuguano maana yake chama hicho hakiwezi kutoa uongozi uliotarajiwa," alisema Mpendazoe.
Alisema mpasuko uliopo ndani ya CCM unatokana na namna chama kinavyoendeshwa na kwamba wapo viongozi wanaotaka chama hicho kiendeshwe kwa mujibu wa Katiba ya chama na wengine wanataka kiendeshwe kwa matakwa ya wachache.
"Upo uwezekano kwamba kuwaondoa wanaotuhumiwa na ufisadi ndani ya chama itashindikana, basi wale wanachama wanaopendelea hatua zichukuliwe watafakari kwa makini sana pendekezo la mwasisi wa CCM Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwamba upinzani wa kweli wa CCM utatoka ndani ya CCM, hatua hii itakuwa yenye tija kwa taifa," alisema na kuongeza kuwa "Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa 'watu wengine wakiamua kutoka ndani ya CCM tutafanya makosa tukiwaona ni wasaliti, kwa sasa CCM ikinganganinia umoja wa bandia itaununua umoja huo kwa kupoteza itikadi yake na wananchi kupoteza imani kwa CCM.
Mpendazoe aliwataka wananchi kuepuka tabiri na kauli zinazotolewa na watu mbalimbali na kuwasihi wamtegemee Mungu ili aweze kuwapatia viongozi watakaojali maslahi ya nchi.
Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu taarifa hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC, John Chiligati, alijibu kwa ufupi "sina taarifa hizo na mimi sio mmoja wa wabunge hao."
Chiligati ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliahidi kufuatilia taarifa hizo ndipo chama kiyatolee tamko.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI