Waandishi wa habari watakiwa kutumia vyema kalamu zao kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi katika ujenzi wa taifa

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,001
9,866
WAANDISHI wa habari wametakiwa kutumia vyema kalamu zao katika kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi inayotekelezwa na kuchangia maendeleo ya taifa na hiyo ni pamoja na kueleza mipango ya kuelekea uchumi wa viwanda, changamoto na namna ya kuzitatua ili wananchi waweze kujua kinachofanywa na Serikali.

Akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari za Uchumi, Biashara na Fedha katika tawi la Benki Kuu Mtwara,Kaimu Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mtwara ambaye pia ni Meneja wa Utawala na Fedha Bw. David Mponeja kwa niaba ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT,) Bwa. Julian Banzi, amesema nafasi na uzito wa vyombo vya habari ni muhimu katika kueleza ni nini Serikali inafanya katika sekta mbalimbali katika kufikia uchumi wa viwanda.

"Tumieni kalamu na vyombo vyenu kueleza agenda muhimu katika ujenzi wa Taifa, Wananchi wanataka kujua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo ikikamilika itachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa letu na hiyo ni pamoja na mchango wa kila mmoja katika kuyafikia mafanikio hayo." Amesema Mponeja kwa niaba ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT,) Bwa. Julian Banzi.

Ameeleza kuwa, kwa kiwango kikubwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT,) inaridhika na jinsi vyombo vya habari vinavyotoa habari zinazohusu sekta ya fedha na uchumi huku changamoto mbalimbali ikiwemo uwezo wa kutafsiri na kuchambua kwa kina taarifa mbalimbali za uchumi zinazotolewa na Benki kuu na taasisi nyingine za fedha na uchumi zikiendelea kufanyiwa kazi mara kwa mara.

Aidha amesema, wamekuwa wakitoa mafunzo ya mara kwa mara ili kukuza uandishi wa habari za uchumi na fedha na kuziandika kwa usahihi, kujenga uwezo wa kutafsiri na kuchambua taarifa hizo na kudumisha uhusiano wa kikazi baina ya BoT na vyombo vya habari.

"Ni imani yangu kuwa kupitia semina tutajifunza zaidi, baadhi ya misamiati na dhana mbalimbali zinazotumika katika habari na taarifa za kifedha zitajadiliwa na kufafanuliwa ili zitakapotumika zitumike kwa namna ambayo zitaeleweka vyema." Amesema.

Vilevile amewataka kusimama katika nafasi zao kwa kuandika masuala yenye tija katika wakati huu ambao taifa lipo mbioni kuelekea uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

"Katika semina hii pamoja na mada nyingine mtajifunza pia namna ya kutambua upatu haramu na yataendeshwa kwa ushirikiano wa BoT, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji Tanzania (CMSA.) hii itawasaidia kuwaepusha wananchi na kuwaonya namna ya kujiepusha na upatu haramu kupitia kalamu zenu."Amesema.

Semina hiyo ni mwendelezo wa Semina ambazo Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikiandaa kwa wanahabari kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Taifa.
 
Back
Top Bottom