Waandishi makanjanja na hatma ya Tanzania | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Waandishi makanjanja na hatma ya Tanzania

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kaa la Moto, Sep 6, 2008.

 1. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #1
  Sep 6, 2008
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,668
  Likes Received: 166
  Trophy Points: 160
  Ukanjanja na changamoto inayoukabili uandishi nchini
  Na Prudence Karugendo

  Zimekuwepo juhudi za makusudi zinazodaiwa ni za kutaka kuilinda taaluma ya uandishi zinazoonekana kufanywa na wana taaluma wakereketwa. Wanataaluma hao wanaona kwamba ni kama taaluma yao inaingiliwa. Majina mbalimbali ya kibaguzi yamebuniwa yakiwalenga wanaodaiwa kuivamia fani. Yanatajwa majina kama makanjanja, makanjakanja nakadhalika, bila shaka mengine yako mtamboni yanaundwa.

  Binafsi nakubaliana na hoja ya kuwepo kwa taaluma ya uandishi na umuhimu wa kuiheshimu taaluma hiyo. Kinachonipa utata, na mahali ninapotofautiana na wanataaluma, ni katika namna taaluma hiyo inavyopaswa kulindwa. Sikubaliani na wanaotaka taaluma hiyo ilindwe kwa mabavu na vitisho dhidi ya wale wasiotakiwa ambao kwa namna moja au nyingine ndio wanaoonekana kuivamia taaluma, japo wao wanajiweka karibu kutokana na mapenzi yao kwenye taaluma hiyo na hivyo kuamua kuiunga mkono.

  Ili taaluma iheshimike haina budi kujilinda yenyewe kwa wana taaluma kuonyesha kile kinachoifanya ikaitwa taaluma, ambacho kwa tafsiri nyingine kinapaswa kiwe nje ya upeo wa wale wasio na taaluma. Mathalan, maadishi yenye kufikirisha ambayo si kila mmoja mwenye kuelewa kuandika anaweza kuyarukia na kujaribu kuyaandika.

  Kinyume chake wana taaluma ya uandishi wanashindwa kukifanya kile ambacho kingeifanya taaluma yao ikaheshimika na kuogopeka, badala yake wanafanya mambo ambayo kila mmoja anajiona ana uwezo nayo. Kwa hilo wa kujilaumu ni wana taaluma ya uandishi wenyewe. Wanapaswa wajiulize kwa nini taaluma nyingine hazivamiwi? Badala ya wana taaluma kutumia ujuzi wa kitaalamu kuihami taaluma yao wanaishia kupiga piga makelele ya kuvamiwa kwa kutaka kuishawishi dola itunge sheria ya kuwalindia taaluma yao. Wana taaluma wameshindwa kuilinda taaluma, wanataka ilindwe na sheria na bunduki (?).

  Kushindwa huko kwa wana taaluma kutumia njia za kitaalamu kuilinda taaluma yao kunaifanya taaluma ya uandishi kubaki kama haina mwenyewe, na matokeo yake ni kila mtu mwenye kujiona ana uwezo wa kuandika kushawishika kujiingiza kwenye taaluma hiyo kwa vile wahusika wanakuwa hawawezi kujitofautisha na wasio wahusika.

  Haitoshi kuilinda taaluma kwa kutaja tu muda ambao mtu anakuwa ameutumia kuisotea taaluma husika au mrundikano wa shahada. Kinachotakiwa ni kuonyesha mabadiliko katika taaluma kwa kuifanyia vitu ambavyo hasiye mwana taaluma atajionea aibu kuisogelea taaluma ya watu. Hapa nchini ni wana taaluma wangapi wanafanya hivyo?

  Wapo watu ambao naamini kwamba wanaendelea kuilinda taaluma ya uandishi bila kutumia mabavu pamoja na kwamba watu hao hawapo tena duniani, ingawa kulingana na mpangilio wa madai yanayotolewa na watetezi wa taaluma wa kipindi hiki, watu hao wanaweza wakaonekana nao hawakuwa wana taaluma kwa vile wasingeweza kutaja miaka waliyotumia wakiisotea taaluma hiyo ya uandishi wala kuonyesha vyeti vya kuwatambulisha kama wana taaluma.

  Mmoja wa watu ninaoamini kuwa bado wanailinda taaluma ya uandishi ni marehemu Shaaban Robert. Uandishi wa mzee yule, ambao mwingine aliufanya zaidi ya miaka 50 iliyopita, bado mpaka sasa unailinda taaluma ya uandishi kwa kumfanya kila mtu aliye makini asiweze kujipendekeza kuwa anaweza kuimudu taaluma hiyo. Wala Shaaban Robert hatumii majivuno, vitisho na majigambo katika kuilinda taaluma yake. Yeye anaiwezesha taaluma kujionyesha uadhimu na uzito wake na kisha yenyewe kujijengea heshima.

  Uandishi wa Shaaban Robert wa kuonya, kuhadharisha, kukanya, kusifia pamoja na kuelimisha, bila kukosa kuhabarisha kwa namna ya pekee ni kielelezo tosha cha uadhimu wa taaluma ya uandishi na manufaa inayoyachangia katika jamii.

  Aina ya uandishi wa Shaaban Robert inawafanya watu kuitamani taaluma ya uandishi. Hii ni kwa sababu wapo watu wanaotumia aina ya uandishi wake kama mwongozo wa maisha yao. Hivyo ndivyo taaluma inavyopaswa kuinufaisha jamii. Na papo hapo jamii inajenga heshima kwa taaluma hiyo kwa wanajamii kuamini kwamba si wote wenye uwezo wa kufanya kama alivyofanya yeye. Kwa mantiki hiyo sitegemei kama zingekuwepo kelele za kutaka taaluma ya uandishi iheshimiwe. Yenyewe ingekuwa inajitosheleza.

  Mtu mwingine aliyeitumia taaluma ya uandishi kuinufaisha jamii ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere. Tangu kabla ya uhuru wa Tanganyika, alipoingia kwenye harakati za kutafuta uhuru, alitumia zaidi taaluma ya uandishi na kuifanya silaha yake kuu katika mapambano yale. Tunakumbuka alivyonusurika kwenda jera baada ya kudaiwa kuwakashfu wakoloni akiwa mhariri wa gazeti la chama cha TANU. Hata baada ya uhuru bado Nyerere aliendelea kuitumia taaluma hiyo kuwaelimisha wananchi juu ya maana ya nchi kuwa huru. Tunafahamu machapisho aliyoyatoa, sina haja ya kuyataja hapa. Na alipokuwa ameisha staafu uongozi bado Mwalimu aliendelea kujikita katika taaluma ya uandishi na kuitumia kufikisha nasaha zake kwa jamii. Mwanzoni mwa miaka ya 1990 pale lilipoibuka kundi la wabunge la kuidai serikali ya Tanganyika, Mwalimu alitumia taaluma ya uandishi kuutuliza mzuka huo. Aliandika vitabu viwili kwa mkupuo navyo vikawafanya wabunge wale kufyata mkia. Ni taaluma ya uandishi iliyofanya kazi.

  Ingekuwa sasa hivi si ajabu Mwalimu angetakiwa aonyeshe vyeti vya uandishi kwanza na wale wanaoamini kwamba taaluma hii ni mali yao, kabla ya maandishi yake hayajakubalika kwa wana taaluma. Na nisingeshangaa kama naye angekumbwa na jina la ukanjanja.

  Nataka nieleweke, nilichokilenga hapa ni uandishi kama waleta hoja wanavyopendelea kuliweka. Maana najua kuna watakaonibadilikia wakidai kwamba kinachopaswa kulengwa ni uandishi wa aina fulani, mfano uandishi wa habari. La uandishi wa habari linaeleweka ila kwa makusudi kabisa wameamua kulipanua suala hilo ili liweze kuwameza wote wanaojihusisha na uandishi kwa lengo la kutaka kuwadhibiti. Ndiyo maana hata mimi hoja zangu nikawa nazielekeza kwenye uandishi kwa ujumla.

  Kwa mtizamo wangu, wapo baadhi ya waandishi ambao wangependa kuihodhi taaluma ya uandishi, bila shaka kwa kutaka iwanufaishe wao tu bila jamii kuambulia chochote. Hawa ndio wanaowaona wale wanaojitokeza kuipanulia wigo taaluma hiyo kama wavamizi katika fani. Huko ndiko mashambulizi yanayoongozwa na majina yenye kila dalili za matusi, kama hilo la makanjanja, yanakoanzia, lakini bila wenyewe kuyaweka bayana manufaa yanayotokana na wale wasio makanjanja katika jamii yetu.

  Majuzi mwandishi mmoja mkongwe hapa nchini alikuwa anajaribu kunipa darasa la uandishi baada ya mimi kuwa nimemchokoza. Alisema kwamba mwandishi anapaswa kuwa kama mwamuzi wa mchezo, kwamba hapaswi kuhukumu nani ashindwe ila kuuachia mchezo wenyewe ndio utoe hukumu. Akasema kwamba mwandishi anatakiwa kutoa kitu jinsi kilivyo bila dalili za upendeleo hata kama anao upande anaoupendelea. Nilipomuuliza juu ya waandishi wanaokiuka kanuni hiyo wakati wakijidai kuwa mahiri katika fani, akasema yeye sasa anatamani kufanya kazi katika vyombo vya ughaibuni maana kwa hapa nchini watu hawaambiliki. Kwa maana hiyo inaonyesha kwamba yanayofanywa na waandishi wa hapa nchini mengi hayaungi mkono, na si ajabu anawaona wale wanaowaita wenzao makanjanja ndio makanjanja wenyewe ila hasemi kwa kubanwa na kanuni za taaluma anazoonekana kuziheshimu na kuzizingatia, anaiachia jamii itoe hukumu.

  Zimetafutwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasakama hao makanjanja, ila ukweli ni kwamba kudorora kwa taaluma ya uandishi hapa nchini kunachangiwa zaidi na baadhi ya wana taaluma kukubali kuzianika wazi bei zao, kitu kilichoifanya taaluma ipimwe thamani yake kulingana na inavyotaka kutumiwa. Watumiaji ndio wamebaki wameishikilia thamani nzima ya taaluma Kwa hapa kuwasakama makanjanja ni kuwaonea.

  Mwandishi anayeandika kwa maelekezo ya kumchafua mtu fulani au kumpamba mtu fulani tayari anakuwa ameishabandika alama ya bei yake usoni mwake. Na kamwe siwezi kuamini kama anafanya hivyo kwa malengo ya kuboresha taaluma. Dhahiri huko ni kuiua taaluma. Thamani ya taaluma inabaki mikononi mwa wale wanaotaka kuitumia taaluma kwa manufaa yao. Hivi kweli waandishi wa aina hii wanataka tuamini kwamba wanapowashambulia wanaowaita makanjanja wanakuwa wamedhamiria kwa dhati kuisafisha taaluma yao? Ni kitu gani cha kutufanya tusiwaone wao kuwa ndio makanjanja?

  Tumewashuhudia wahariri kadhaa, ambao baadhi yao ndio vinara wa kuushambulia unaoitwa ukanjanja, ama wakitishiwa kuburuzwa mahakamani au wakati mwingine kulazimika kuomba misamaha nje ya mahakama kutokana na vyombo wanavyovihariri kutowatendea haki baadhi ya watu, kama vile kuwakashfu, kuwapaka matope nakadhalika, ili kuzifurahisha nafsi fulani ambazo zinakuwa zimewatuma au kuwanunua. Katika hali hiyo nani anayo haki ya kusimama na kumnyooshea mwingine kidole kuwa ni kanjanja? Kwa nini ukanjanja usionekane kuanzia hapo?

  Hii inapaswa itukumbushe kwamba vita inapokuwa ngumu wasio na fani ya kijeshi hulazimika kuingia katika mapambano hata kama ni kwa kutumia silaha duni kama manati, ili kujaribu kuokoa jahazi. Wanaoitwa makanjanja inabidi tuwatambue kwa kukiona kile kinachofanywa na wasiokuwa makanjanja na kiwe kimejitofautisha, vinginevyo siuoni ubora unaowasababishia watu viburi vya kuwapachika wenzao majina ya ajabu ajabu.

  Inabidi tujenge utamaduni wa kuifanya taaluma ya uandishi kujisimamia, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeijengea heshima inayoistahiki.

  prudencekarugendo@yahoo.com

  0784 989 512
   
 2. Kuhani

  Kuhani JF-Expert Member

  #2
  Sep 6, 2008
  Joined: Apr 2, 2008
  Messages: 2,945
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 135
  Mbona hajasema hizo juhudi zinataka nini ?

  Zinataka nani au nini na uandishi wa aina gani udhibitiwe? Ukiandika kitabu cha maisha yako au cha kujisifia wakati sio mwandishi pia kinakatazwa katika hizo juhudi za wanataaluma wakereketwa? Unasema kitabu cha Nyerere nacho kingeitwa kanjanja na wanataaluma wakereketwa kwa sababu hakuwa mwana taaluma wa uandishi. Ina maana hizo juhudi zinataka kila uandishi upigwe marufuku kwa yeyote ambae sio mwandishi. Mwandishi ni nani? Hao wanataaluma wakereketwa ambao unawapinga wanasema mwandishi ni nani? Kuandika matundiko JF nako kungeguswa na hizo sheria mpya? Vipi kuandika aya za miziki ? Na kuandika ujumbe wa mchoro kwenye ukuta wa nyumba ? Na kuandika na kusambaza mtaani barua ya wazi kwa baba mkwe wako?

  Uandishi wa nini, kila kitu?

  Ndugu Karugendo, anza tena.
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  Dec 31, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,394
  Trophy Points: 280
  Mwandishi Wetu ( Gazeti la Sauti Huru) Disemba 30,2008

  YUKO wapi bilionea Robert Maxwell? Nani anasikia tena tambo, nyodo na majigambo yake? Amefutika. Amebaki historia.

  Maxwell alikuwa ni bilionea mwenye kumiliki magazeti makubwa kama Daily Mirror na Daily News na pia alikuwa mchapishaji wa vitabu. Alivuma mno kwenye miaka ya themanini kutokana na utajiri wake.

  Kamwe hakuna aliyefikiria kama itafika siku Maxwell atafilisika na kuwa kapuku hadi kushindwa kumudu kulipa madeni yaliyomkabili.

  Hii ni hulka ya watu wengi wakiwemo matajiri na hata baadhi ya viongozi wa ngazi za juu. Wanapofika kwenye mafanikio, wanajisahau na hawafikirii kama kuna kuanguka. Wanadhani wataendelea kula raha milele.

  Kiichomponza Maxwell ni uamuzi wake wa kuchanganya biashara na siasa na haswa siasa za malumbano. Alitumia vyombo vyake vya habari kuhubiri kile alichotaka na kufanya alichojisikia.

  Alifanya hivi kwa kuwa hakukuwa na wa kumzuia, alimshambulia kila aliyemtaka huku akijiweka kwenye tabaka la juu zaidi na kujiona kama ni mungu mtu hadi kufikia hatua ya kulazimisha kila asemalo liwe.

  Maxwell akageuka mwiba. Malumbano yakapamba moto akayaingiza magazeti yake kwenye mapambano – yakandika kile chenye maslahi kwake na kusahau matatizo ya wananchi.

  Hapo wasomaji wakaanza kugawanyika kutokana na mabadiliko ya mfumo wa magazeti yake. Yalijaa habari za majisifu yake na mapambano, wakaamua kuacha kuyanunua.

  Kuanzia hapo akaanza kuyumba kibiashara, mauzo yakashuka, madeni yakamzonga na mwishowe alifilisika.

  Maxwell akakosa pa kushika, hakupata tiba ya matatizo yake akawa ni kama mtu aliyechanganyikiwa na hatimaye 5, Novemba, mwaka 1991 akakutwa amefariki ndani ya boti ya kifahari iliyoegeshwa kwenye ukanda wa Tenerife , kisiwa cha Canary nchini Hispania na alizikwa kwenye mlima Olives, Jerusalem .

  Kila mmoja alizungumza lake juu ya kifo chake, wengine walisema ameuawa na wapo walioamini amejiua kutokana na msongo wa mawazo yaliyosababishwa na kuanguka kibiashara.

  Badaa ya kifo chake, mabenki yakaanza kuuza mali alizokuwa anamiliki yakiwemo makampuni ili kufidia madeni, mwanae hakuwa na la ziada naye alilazimika kuuza hisa zake na mali kuwa mikononi mwa watu wengine.

  Huo ndio ukawa mwisho wa zama za bilionea Robert Maxwell aliyeishia kupata ubunge badaa ya purukushani zake za kisiasa na kutumia fedha nyingi kudhamini Chama cha siasa.

  Hakika huu ni mfano tosha unaofaa kumpa somo Reginald Mengi, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP. Kwani naye anaonekana kushindwa kujigawa na kubaki mguu mmoja kwenye siasa mwingime kwenye biashara.

  Mengi amejitosa kwenye siasa za malumbano. Kama ambazo alianza nazo Maxwell, hajui ashike wapi, bado anatamani kuendelea na biashara na huku wakati huohuo anatamani na amegeuka mshika mbili.

  Ukimsikiliza kwa makini kauli zake utagundua anaweweseka na kujikaanga kwa mafuta yake mwenyewe. Ni dhahiri anahitaji msaada. Si msaada wa kifedha bali ni wa maombi na ushauri.

  Wanatakiwa watu wenye busara wamuweke chini na kumshauri kuacha moja na kuendelea kuweka nguvu kwenye jambo moja vinginevyo atakosa moja ama yote.

  Kwanini tusianza kuhisi kwamba hata yowe analopiga hivisasa la kuhujumiwa ndio ishara ya kuporomoka kwake?

  Kwamba mambo yameanza kumuendea kombo na sasa anaamua kusaka mchawi. Anatafuta wa kumshushia lawama pale atakapoishia ukingoni na kubaki kwenye ukapuku.

  Hakuna haja tena ya kurudia orodha ya malumbano aliyowahi kuingia na watu wa kada mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na viongozi wa serikali huku kila kukicha akilia kuonewa ila anaonekana kutamani kuwa mwanasiasa.

  Kama ilivyokuwa kwa Maxwell, Mengi naye anatumia kwa kasi vyombo vyake kuhubiri kile anachotaka kiwe. Akitumia kigezo cha kupambana na ufisadi kupenyeza hoja zake anazozitaka kwa lengo la kuwashambulia anaowalenga.

  Mengi leo amegeuka mwanasiasa na si mfanyabiashara tena kama tulivyomzoea kwa miaka mingi. Anarukia kila hoja ambazo nyingine hazimuhusu.

  Pia anatumia vibaya kofia ya kuongoza vyombo vya habari kama mwenyekiti wa wamiliki wa vyombo vya habari mchini (MOAT) kuamua anachotaka.

  Mamlaka hiyo anaitumia kuviongoza na kuvipeleka anapopataka vyombo vya habari hata ambavyo havimiliki na kuvitumia kama kipaza sauti cha kusema lolote analojisikia.

  Hii ni hatari kwa usalama wa nchi. Mtu mmoja akiachwa awe na nguvu kiasi hiki na hata kuwa na ujasiri wa hali ya juu wa kuwashambulia viongozi wa juu serikalini.

  Tujenge mashaka sasa, Mengi anafanya harakati hizi kwa maslahi ya nani? Je, ni kweli ana uzalendo kiasi hiki ama ana lake jambo ?

  Kama ni kweli angekuwa mzalendo na muungwana kama anavyotaka aonekane, angetumia njia stahili, kufikisha kile anachotaka kuliko kutumia njia hii ya mapambano na malumbano alizozoea kutumia.

  Kwanini tusiamini kile kinachozungumzwa kwamba anataka kuwania Urais? Ingawa miezi kadhaa iliyopita, alishuka waraka mrefu na kutumia fedha nyingi kulipia kurasa za magazeti kukanusha habari hizi.

  Bado hajatushawishi tuamini kwamba hana mpango na ikulu au kama si yeye basi amemua kuweka nguvu kusaidia mtu au kundi fulani liweze kuingia ikulu.

  Kama anaitamani ikulu basi atumie utaratibu unaoeleweka kuliko kuingia na mtindo huu wa kuchafua na kulumbana na watu, labda atuambie kama bado anafanya mazoezi kwanza.

  Na kama anajiamini ajitose tuone umwamba wake, alumbane na wanasiasa wa kweli tuone kama anaweza kuweka hoja nzito na si kulalamika kila kukicha.

  Mengi awe huru na si kuendeleza siasa za kujificha na kupiga kelele mitaani – siasa za porini huku akishusha malalamiko yasiyokwisha miaka nenda rudi.

  Watu wamechoka malalamiko na tuhuma zisizoeleweka, wanataka kusikia mambo ya msingi yatakayowasaidia wengi zaidi kuliko kile kinachomuhusu mtu binafsi anayetaka ufalme huku akipigia debe maslahi yake.

  Mengi anapaswa kuchagua moja, biashara ama siasa ingawa inabidi akichagua siasa afikirie mara mbili; siasa haziwezi kwa kuwa ana jazba.

  Akumbuke kwamba ili abaki na nafasi yake aliyonayo asijihusishe na masuala ya siasa kwani mwisho wake ni mbaya na duniani kote hakuna mchanganyiko huu ambao labda sasa tumuite ni ‘mfanyabiasiasa.’
   
  Last edited by a moderator: Dec 31, 2008
 4. M

  MkamaP JF-Expert Member

  #4
  Dec 31, 2008
  Joined: Jan 27, 2007
  Messages: 7,313
  Likes Received: 1,452
  Trophy Points: 280
  Mwanakijiji
  Nawewe msimamo wako unamashaka ,Tangu IPP ifoji sahihi ya mtikila na Wao kuamua kukaa kimya toka siku ile wajanja walibainisha Mengi ni mfuasi wa nani na anafuata nyayo zipi.
   
 5. G

  Game Theory JF-Expert Member

  #5
  Dec 31, 2008
  Joined: Sep 5, 2006
  Messages: 8,571
  Likes Received: 93
  Trophy Points: 0
  I WONDER KATIKA VITA YA masha VS mengi bwana FREEMAN MBOWE atakuwa upande gani...japo hapo awali alikuja dhahiri kummaliza na madongo Mengi humu JF halafu jioni kenda kukopa pesa! siasa kweli mchezo mchafu


  how about ukatafuta ile thread ya ANATOMY OF STUPIDITY? Majibu kuhusu R.MENGI yalishajitosheleza
   
 6. Kite Munganga

  Kite Munganga JF-Expert Member

  #6
  Dec 31, 2008
  Joined: Nov 19, 2006
  Messages: 1,298
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 145
  Huwezi tenganisha Biashara na siasa, Angalia Karamagi,RA,Kapuya,Masha,Marehemu Nyaulawa, Mkapa, etc........
   
 7. B

  Bulesi JF-Expert Member

  #7
  Dec 31, 2008
  Joined: May 14, 2008
  Messages: 6,447
  Likes Received: 414
  Trophy Points: 180
  Mwanakijiji heshima mbele, nadhani kumfananisha Robert Maxwell na Reginald Mengi kunaweza kuwa sio sahihi kwani ingawa kweli Mengi ni newspaper magnate kama alivyokuwa Maxwell lakini Maxwell hakuwa anatetea wanyonge na kupiga vita ufisadi kama anavyofanya Mengi. Mpaka sasa Mengi hajaonesha kuwa anataka kuingia kwenye active politics isipokuwa hao mafisadi anaowaumbua ndio wanawatumia vikaragosi wao kuspin hata kumfananisha na marehemu Maxwell. Mbona hamuandiki kumfananisha na successful newspaper magnates kama Rupert Maddox au hata belucsson wa Italia? Haya yote ni majungu na spin za mafisadi na Mungu yupo wote mtaangamia!!
   
 8. Chakaza

  Chakaza JF-Expert Member

  #8
  Dec 31, 2008
  Joined: Mar 10, 2007
  Messages: 23,680
  Likes Received: 21,942
  Trophy Points: 280
  Mwanakijiji hilo gazeti la sauti huru linamilikiwa na nani? Maana mimi napata harufu fulani sio nzuri juu ya yaliyosemwa na huyo mwandishi.
  Mengi kufanya biashara kunamzuia kujiunga na wengine kukemea Rushwa na ufisadi? Sidhani kama ni hivyo hata kidogo. Hata hayo yanayoitwa malumbano yaliyo jitokeza baina yake na viongozi na baadhi ya wafanya biashara ambao rekodi zao ziko wazi kila mtu anaelewa kitu gani kiko hapo.
  Mimi nafikiri Mengi anayohaki ya kukemea Rushwa na ufisadi pia kujitetea na kujilinda anapoona anataka kuhujumiwa na viongozi wachafu/mafisadi wasio fuata maadili ya uongozi bila woga kama raia huru. Kumfananisha na Maxwell si kumtendea haki. Au tumefikia mahali tunataka wafanyabiashara wanafiki na wanaojipendekeza kwa viongozi wa serikali ili washirikiane kuhujumu wanyonge? Mengi anaweza kuwa na mapungufu yake, LAKINI TUNAHITAJI WAKINA MENGI WENGI ZAIDI.
   
 9. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #9
  Dec 31, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,394
  Trophy Points: 280
  Jana magazeti kama manne hivi yalitoka na habari zinazohusiana. Na kimsingi bado zimeshikilia suala la Mengi na Masha! Hiyo ni makala mojawapo niliyoipta kutoka kwenye gazeti hilo... Nimeiweka ili watu wachambue kama suala la Mengi linaweza kufananishwa na Maxell au ni over stretching..?

  Siyo maoni yangu hayo ni ya mwandishi wa gazeti hilo!
   
 10. Invisible

  Invisible Admin Staff Member

  #10
  Dec 31, 2008
  Joined: Feb 11, 2006
  Messages: 9,091
  Likes Received: 237
  Trophy Points: 160
  Gazeti la Sauti Huru ni la nani mkuu?
   
 11. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #11
  Dec 31, 2008
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Kumjua mwenyewe kunaweza kuongeza dimension ya discussion, lakini Mkuu hudhani kuwa kwa hatua hii, tuzame zaidi kuchambua ujumbe uliomo kabla hatujawajua watuma ujumbe?
   
 12. Sajenti

  Sajenti JF-Expert Member

  #12
  Dec 31, 2008
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 3,673
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 0
  ...Mkuu kwa nini mnauliza mwenye gazeti au ndio kilichoandikwa gazetini kinapimwa kutokana na mmiliki wake???:confused:
   
 13. Invisible

  Invisible Admin Staff Member

  #13
  Dec 31, 2008
  Joined: Feb 11, 2006
  Messages: 9,091
  Likes Received: 237
  Trophy Points: 160
  Certainly, nilitaka kwanza kufahamu hili gazeti linamilikiwa na nani. Inawezekana liko chini yake (Mengi) au likawa chini ya kina Rostam & Co. Kujadili ujumbe ndani ya hoja ndio msingi wa majadiliano ila frankly gazeti hili ndiyo mara yangu ya kwanza kulisikia. Kuna link ambayo inaweza kunipeleka katika tovuti ya gazeti husika?

  Kumfananisha Robert Maxwell na Reginald Mengi kwangu naona kuna mwelekeo ulio mbali na uhalisia wa mambo japo kuna mantiki katika hoja ya mwandishi. Ndiyo mawazo huru!

  Afterall alichokichambua mwandishi hakina tofauti kubwa na yale mawazo huru ya wadau mbalimbali waliyoyaainisha katika "The Mengi vs Masha Saga" thread.
  Just assume unakuta gazeti hilo ni lake mwenyewe (yani liko chini ya IPP), ni ujumbe gani utapata? Bado nadhani kuna umuhimu wa kumjua mmiliki wa gazeti hilo ama Mhariri mkuu wake ni nani. Kuna watu ambao siku hizi hata huwa sipendi kuumiza kichwa kusoma wameandika nini; Manyerere mmojawapo!
   
 14. M

  Mtanzania JF-Expert Member

  #14
  Dec 31, 2008
  Joined: May 4, 2006
  Messages: 4,818
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 145
  Huyu mwandishi inaelekea hata hamjui Robert Maxwell. Kuanguka kwa huyu fisadi wala haikuwa kwasababu ya kuchanganya biashara na siasa.

  Ina fact kwa UK ni kawaida kwa wafanyabiashara wanaohusika na vyombo vya habari kuchanganya siasa na biashara.

  Ukiangalia UK na USA, Rupert Murdoch na vyombo vyake (SKY NEWS, FOX NEWS, SUN etc) wanafikia hata kuamua nani awe rais au PM. Hivyo hivyo Italy kwa Berlusconi na vyombo vyake anaendelea na biashara pamoja na siasa.

  Kuanguka kwa Maxwell ilikuwa sio kwasababu ya kujihusisha na siasa, ilikuwa kwasababu ya ufisadi. Muda wote alikuwa anatumia njia za mkato kujitajirisha kwa cost ya wafanyakazi wake na wanyonge wengine.

  Mwandishi hajafanya homework ya kutosha labda kwasababu yuko biased na lengo lake lilikuwa kumshambulia mengi. Ukiandika makala ukiwa na chuki na mtu sio rahisi kuja na arguments ambazo ni balanced.
   
 15. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #15
  Dec 31, 2008
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  - Hapa habari muhimu ni kwamba kwa kugombana na Mengi, Masha amekanyaga pabaya sana in the last five days nimepata habari nyingi sana za dataz ya kampeni za wananchi wanaomuunga mkono Mengi, kukasirishwa sana na kitendo cha Masha kumgusa Mengi, kwa hiyo the kampeni ni kumuondoa Masha by any means necessary na ninaamini kwamba hizi artcile ziko kwenye hiyo avenue. On top of the agenda inatakiwa kuwa Masha sio raia wa Tanzania, nafikiri tembo wakubwa wakipigana sisi nyasi ni kukaa pembeni tu na kuwatakia heri.
   
 16. Invisible

  Invisible Admin Staff Member

  #16
  Dec 31, 2008
  Joined: Feb 11, 2006
  Messages: 9,091
  Likes Received: 237
  Trophy Points: 160
  Halafu ni waziri wa Wizara nyeti... Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi!

  Hili mimi nilisita kulisema, heri umeligusia mkulu!
   
 17. G

  Game Theory JF-Expert Member

  #17
  Dec 31, 2008
  Joined: Sep 5, 2006
  Messages: 8,571
  Likes Received: 93
  Trophy Points: 0
  kumelewa MENGI basi inatakiwa mjiulize kwa nini ile ripoti ya tume pamoja na hansard za ile kamati iliyoundwa kumchunguza kwenye ugomvi wake na MALIMA

  kule ndiko mtaelewa who is REG MENGI na nia yake ni nini hasa

  haya mengine ni sidelines tuu
   
 18. k

  kananyayo Member

  #18
  Dec 31, 2008
  Joined: Dec 15, 2008
  Messages: 7
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Vita dhidi ya ufisadi, ni ngumu na mafisadi lazima wajihami kwa matumaini ya kuokoka mkono wa sheria. Na miongoni mwa mbinu zitumikazo ni pamoja na kuanzisha vijigazeti vyenye mlengo wa kufifisha vita hivyo na kuwaandama majemedari wa vita hivyo, kwa matumaini kuwa watakaa kimya. Cha kusikitisha hata wanandishi waliodhaniwa kuwa na sifa za kutukuka walishaingizwa katika line, tangu walipokubali kutumiwa kuikingia kifua Richmond.
   
 19. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #19
  Dec 31, 2008
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Mkuu, hapo kwenye highlight pana nipa shida kidogo. Mwelekeo wa article ni kumponda Mengi, inakuwaje sasa wewe unatuhabarisha kuwa kumbe it is the other way around?
   
 20. Invisible

  Invisible Admin Staff Member

  #20
  Dec 31, 2008
  Joined: Feb 11, 2006
  Messages: 9,091
  Likes Received: 237
  Trophy Points: 160
  Najijibu:

  Gazeti la Sauti Huru ni la Subash Patel na Yusufu Manji! Well, sasa inakuwa rahisi kuweza kung'amua kinachoendelea.
   
Loading...